Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Tunahitaji kuwa makini Tanzania si salama
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Tunahitaji kuwa makini Tanzania si salama
By Marshy Abdu | Published  07/16/2007
Christopher Nyenyembe


MANUNG’UNIKO, hofu, woga na kutojiamini na kudhani kuwa Tanzania ndiyo nchi pekee duniani iliyojaliwa kuwa kisiwa cha amani kunaleta shaka na kudidimiza msimamo wa nguvu za wafanyakazi katika kudai maslahi bora.

Hivi sasa kuna vuguvugu zito lililotanda kwenye mawazo ya wafanyakazi tangu serikali ilipotangaza kuongeza mishahara na kuwafanya watu waone kuwa hicho ni kiini macho kutokana na bei mpya ya mafuta.

Kuna kila dalili na mwelekeo wa wafanyakazi kuanza kujipanga ili kujipima ubavu kama kweli wanaweza kuitisha mgomo wa nchi nzima wa kupinga nyongeza mpya ya mishahara ambayo haiendani na hali halisi ya maisha.

Nawakumbuka hao ndugu zangu wakati wa OTTU, Katibu Mkuu kwa wakati huo, Bruno Mpangala aliweza kujaribu kwa kiasi fulani kuandaa mgomo wa wafanyakazi nchi nzima nakumbuka kuwa mgomo huo haukufanikiwa sana.

Leo hii Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) kwa kauli ya Katibu Mkuu, Nestory Ngulla ametamka bayana nia ya vyama vyote vya wafanyakazi zaidi ya 12 kuwa vinajipanga kuandaa mgomo huo ili serikali iweze kuongeza kima cha chini cha mshahara.

Sipingani na ushujaa huo unaotakiwa kuonyeshwa na wafanyakazi wa nchi hii, wala sipingani na ujasiri alionao kila mfanyakazi katika kutekeleza uamuzi huo kama kweli kuna nia thabiti ya kuishinikiza serikali.

Ndiyo maana nasema hivi, manung’uniko, hofu, woga na kutojiamini inawezekana kikawa kikwazo kikubwa cha kuwafanya wanaharakati hawa wa kutetea maslahi ya wafanyakazi wasifike popote kwa kuhofia kuifanya Tanzania isiwe salama.

Nasema hivi tunahitaji kuwa makini kwa hilo ili Tanzania iwe salama nikiamini asilimia 100 kuwa si salama, usalama ninaouzungumzia si ule wa mahusiano ya nchi na nchi au usalama wa mipakani la hasha usalama ninaoumaanisha ni usalama wa haki na maslahi bora ya watumishi.

Huwezi kuzungumzia usalama wa ndani ya nchi kama watu wananung’unika na kunung’unika kwao kumejaa hofu, woga na kutokujiamini kuwa wanaweza kuishinikiza serikali ili iweze kusikia kilio chao na kujali mapendekezo ya Kamati ya Rais ya kuratibu nyongeza ya mishahara mipya.

TUCTA ilihusishwa kwa hilo na sijui ni namna gani walivyoweza kupigwa chenga na kujikuta wakipokea taarifa ya kuwashangaza ya kima cha chini kilichotangazwa na serikali ikiwa ni ongezeko la asilimia zipatazo 17 tofauti na matarajio yaliyokusudiwa.

Sasa hiyo ni ngoma inatakiwa ichezwe na wafanyakazi wote wenye mshikamano wa nguvu kama myororo wa chuma na ni wazi kuwa anatakiwa awepo kinara mahiri mwenye uwezo wa panya wa kuweza kumfunga paka kengele ili yale yaliyokusudiwa yaweze kutimia.

Kwa mtazamo wangu, Tanzania si salama kwa upande wa masilahi bora ya wafanyakazi na naamini kabisa katika nchi nyingi duniani kundi la wafanyakazi ndilo lenye nguvu katika utawala wa nchi kinyume na matakwa ya wanasiasa.

Kundi la wafanyakazi ni dogo likilinganishwa na makundi ya Wakulima na wafugaji hawa ni wengi lakini wamekuwa wakilitegemea sana kundi hilo kwa kuwa kundi hilo ndilo lililobeba wataalamu.

Wafanyakazi ndio usukani wa nchi ambao waliobeba utaalamu wote unaoifanya nchi mambo yake yaende sawa kwani hao ndio madaktari, wahandisi, wahasibu, walimu, marubani, wanajeshi, Polisi na ndio wenye ujuzi wa kila fani inayotegemewa katika uchumi na ujenzi imara wa nchi.

Hawa sasa wanalia, wanalalamika ni wasomi hawa wanaoshuhudia baadhi ya watendaji wa serikali na wanasiasa wakipata mishahara minono huku wao wakifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa Watanzania hawalali gizani wala wagonjwa hawafi hospitalini.

Nchi haiwezi kuwa salama sana kama kuna dalili hizo na dalili hizo ndiyo chimbuko mahususi la hujuma nzito ndani ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kupitia halmashauri zao kwa kuwa hawana njia mbadala ya kujiingizia kipato zaidi ya kufikiria kufanya vitendo vya ubadhirifu.

Mishahara midogo ndiyo inayomshawishi mtumishi wa serikali amwibie mwajiri wake kwa kuwa hana njia nyingine itakayoweza kumhakikishia kuwa anaweza akaishi mwezi mzima kwa kutegemea mshahara wa kima cha chini ugongane na mwingine wa mwezi unaofuata.

Tanzania haiwezi kuwa salama katika udhibiti wa mapato yake ya ndani kama wafanyakazi wataendelea kulipwa mshahara usiokidhi kabisa hali halisi ya maisha ya mfanyakazi mmoja mwenye familia ya watu watano, yaani baba au mama na familia ya watoto wanne hiyo ni ndoto.

Mahitaji halisi ya maisha hayaendani kabisa na utashi wa mtu ili aweze kuishi bila kuiba, kuhujumu ama kujiingiza kwenye vitendo haramu ili aweze kukidhi mlo halisi wa siku, usafiri, ada za watoto, mavazi, tiba, na starehe mambo ambayo ni ya msingi na mengine mengi.

Katika historia ya nchi nyingi duniani vyama vya wafanyakazi ndiyo chimbuko la vyama vya siasa na siasa imo ndani ya wafanyakazi na ndimo wanamotoka viongozi wa kisiasa na ndio hao wanaokuja kutawala nchi hivyo tunapaswa kuwa makini kwa hilo kwa kuwa nguvu kazi ya kutosha ipo, wataalamu wapo na wasomi waliobobea.

Wafanyakazi hawahitaji kugoma ili serikali iweze kuona fahari ya kuwaita wataalamu wengine kutoka nje wafanye kazi kuziba pengo la mgomo huo jambo ambalo ni ngumu kutekelezwa kwani yaliyotokea kwa madaktari kugoma bado ilikuwa homa iliyoitikisa nchi.

Mgomo siku zote una hasara kubwa kuliko faida na mgomo unaweza kuvuruga bajeti yote ya serikali endapo shughuli zote za uzalishaji mali na utoaji wa huduma zitaathiriwa na mgomo, kitendo ambacho kinapaswa kuepukwa mapema kwa njia ya kukaa na kukubaliana (collective bargaining).

Naamini kabisa na nasema bila shaka kuwa kama serikali itawalipa mishahara mizuri wafanyakazi wake, lazima uwajibikaji utaongezeka kwa kuwa wataacha tabia ya kutoroka maofisini kwenda kufanya shughuli mbadala ili kujiongezea kipato cha ziada.

Kama watalipwa vizuri wataheshimu kazi na watatoa huduma nzuri kwa wananchi bila kufikiria mambo mengine ukiwemo ushawishi wa wizi, ubadhirifu na vitendo vingine kwani kinyume cha utendaji bora ni haki ya serikali na vyama vyao vya wafanyakazi kuwatimua wale wasioridhika.

Nasema hivi, Tanzania itakuwa salama sana kama mishahara ya wafanyakazi itakuwa bora na si salama kama migomo inayokusudiwa itafanikiwa, nikiamini kuwa vuguvugu la migomo ya wasomi wa vyuo vikuu ilivyoweza kuitia hasara serikali.

Kundi la wafanyakazi ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi na ndio dira kama nilivyosema awali na hali bora ya maisha yao ndiyo chimbuko la mzunguko mzima wa shughuli za kijamii ambazo pia zinawahusu wakulima na wafugaji na kada nyingine ya wafanyabiashara.

Ndiyo maana Nasema hivi tunahitaji kuwa makini Tanzania si salama na usalama wa ndani utakuwa mzuri kama mishahara itakuwa mizuri itakayosukuma ukuaji wa tija, huku wafanyakazi wakitakiwa kufanya kazi kama ‘watumwa ili waishi kama wafalme’, Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki TUCTA.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0754 301 8648 au barua pepe cnyenyembe@yahoo.com

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.