TAARIFA za afya inayosuasua ya Rais Mstaafu wa Zambia, Frederick Chiluba, zinanifikirisha sana kuhusu hatima ya viongozi wa Afrika wanaotanguliza matumbo yao na ya rafiki zao.
Ninawawaza viongozi wangu Tanzania ambao kila kukicha wamekuwa wakihusishwa na tuhuma na kashfa zisizoisha, na zinazoibua maswali yasiyojibiwa.
Rais Mstaafu Chiluba yu mahututi. Anasumbuliwa na magonjwa ya moyo, ambayo yamemzidi nguvu tangu Mei mwaka huu alipopoteza fahamu na kuanguka chini. Hadi mwishoni mwa wiki hii, Serikali ya Rais Levy Mwanawasa ilikuwa inakamilisha taratibu za kumpeleka Chiluba Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu ya kina.
Wafuatiliaji wa mambo wanasema kwamba kudhoofika mno kwa afya ya Chiluba kumetokana na kashfa za rushwa dhidi yake na mkewe, Regina. Wengine wanakwenda mbali na kusema dhiki anazopata sasa ni malipo ya raha alizopata alipokuwa akitumbua ‘mapesa’ ya Wazambia akiwa Ikulu.
Wapo wanaodhani kwamba hii ni laana ya Rais wa kwanza wa nchi hiyo, Kenneth Kaunda, ambaye aliondolewa na Chiluba na akasumbuliwa na hata kutiwa ndani kwa sababu za kiitikadi akiwa mstaafu. Lakini hii ni sababu dhaifu.
Chiluba anaponzwa na wizi wake. Ametuhumiwa, na tayari ametiwa hatiani kuwa aliiba (akiwa madarakani) pesa za wananchi wa Zambia zinazokadiriwa kuwa dola za Kimarekani milioni 46 (USD 46,000,000) ambazo ni kama sh bilioni 47 (47,000,000,000) za Kitanzania.
Mahakama Kuu ya London, Uingereza, ilimtia hatiani tangu Mei 2007. Hivyo, hata mimi sioni shaka, wala siogopi, kumuita mwizi.
Wakati anamalizia ngwe yake mwaka 2001, Chiluba alijiona mzima sana, alitamani kuongeza muda abaki madarakani. Nguvu za kidemokrasia nchini humo, sikasema ‘hapana!’
Siku zote, hata sasa, amekuwa kiongozi mtanashati. Akivaa suti inamkaa vizuri. Na havai suti za hovyo hovyo. Ni maridadi kama hizi wanazovaa viongozi wetu. Lakini Jaji wa Mahakama Kuu ya London, Peter Smith, alisema wakati akitoa hukumu, kwamba suti hizo zilinunuliwa kwa pesa ya wizi! Na aliwataka Wazambia watambue hilo.
Simtakii mabaya Chiluba. Lakini kama alidhani miaka 10 Ikulu ni mingi, na akadhani kwamba sheria za nchi yake zingemlinda asichukuliwe hatua, na akadhani kwamba chama chake kingemlinda, alikosea.
Zambia imebadilika. Ina rais ambaye kauli na vitendo vyake vinaendana, walau katika vita dhidi ya rushwa. Anayemkaribia ni Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, aliyemfukuza kazi makamu wa rais kwa tuhuma za rushwa. Tutakapokuwa tunawakumbuka mashujaa wa Afrika katika karne hii, bila shaka atakuwamo pia Rais wa Malawi, Bingu wa Mutharika, aliyegundua kuwa chama tawala kinakwamisha jitihada za serikali, akaachana nacho.
Viongozi wengi waliobaki katika Afrika ni dhaifu. Ni watanashati wa mavazi na kauli tamu tamu, ni wajeuri wanapoguswa pabaya, lakini ni wanyonge katika dhamiri na maadili ya utumishi wa kazi yao.
Juzi nilipokuwa nasoma makala ya Makwaia wa Kuhenga katika gazeti hili, iliyokuwa na kichwa cha habari: Tuwashitaki au tusiwashitaki marais wastaafu? nilikuwa nawaza yanayotokea Zambia na Tanzania.
Mwandishi aliandika vizuri sana na akajenga hoja na kuhitimisha kwamba tusiwashitaki bali tuweke misingi ya kuwachunga wanapokuwa madarakani. Naamini kama angekuwa anafanya utafiti kwa kuwauliza wananchi swali hilo, angepata majibu tofauti.
Wakubwa wana madaraka makubwa. Wana maslahi manono. Na wanapoiba wanaiba kweli kweli. Tazama kiasi hicho cha Chiluba. Ipo orodha ndefu ya viongozi walioibia nchi zao, na wakaachwa hadi walipokufa wenyewe wakiwa maskini kama walivyozaliwa, lakini nchi zao zikiathirika mno kwa wizi wao na maswahiba wao.
Ikumbukwe kuwa rais anapoiba, haibi peke yake. Wala haibi kwa mikono yake. Anaiba kwa mtandao, tena wa siri sana.
Na wengi wao hawagunduliki kuwa wameiba hadi wanapokuwa wameondoka madarakani.
Kwa sababu hiyo, hata wasaidizi wake wanapogundua kwamba mkubwa anaiba, nao wanaiba kweli kweli, maana wanajua kuna kinga.
Katika nchi yetu tumeweka kinga ya ziada hata baada ya rais kustaafu.
Hawezi kushitakiwa kwa wizi huo. Wanaojenga hoja za kukubaliana na kinga hiyo, wanaamini kwamba kwa kufanya hivyo tunadumisha amani na utulivu. Wanasema, kama alivyodokeza Makwaia, kwamba rais aliye madarakani akianza kumfuatafuata rais mstaafu Hatutafika!
Hatutafika wapi? Kwenye ufisadi? Kwenye uadilifu?
Hoja hii inajenga misingi ya wizi. Mtu anaiba kijua kwamba hakuna litakalomtokea.
Anajua kuwa hata akishastaafu hakuna atakayemshitaki. Ni hoja inayojenga jeuri na kiburi. Na ndiyo maana viongozi wetu wanafanya lolote watakalo na kupuuza maoni ya wananchi. Wanajua hakuna tutakalowafanya.
Na ndiyo maana baadhi yao hupenda kuongeza muda ili waendelee kuwapo na kufaidi zaidi au inapobidi waondoke, wanatafuta kumwachia mtu atakayelinda maslahi yao. Nchini kwetu, masilahi haya ya wizi, siku hizi yanaitwa amani na utulivu!
Mimi nadhani ndiyo maana watawala wetu wanakataa katakata kuiondoa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU au PCB) ofisini mwa rais. Wanaifanya taasisi ya kuwasafisha wakubwa na kuwabana wadogo wa kutolea mfano wa vita dhidi ya rushwa.
Ndiyo maana serikali inaweza kuwakingia vifua watuhumiwa wa wizi au ubadhirifu wa pesa za umma, kama inavyotokea sasa katika sakata la Benki Kuu. Serikali inasema italichunguza suala la Benki Kuu kwa kuwatumia wataalamu wa nje, ambao inaweza kuwaajiri na kutolazimika kufuata uhauri wao. Kwanza, hawana madaraka nayo. Ni waajiriwa wa muda ambao wakati wowote wanaweza kufukuzwa, kama ilivyotokea Zanzibar mwaka 2005 zilipoonekana dalili kwamba kampuni ya Afrika Kusini ingefichua siri iliyomo katika daftari la wapiga kura. Wakaifukuza. Na hadi leo tunajua kuwa daftari la Zanzibar limejaa majina ya ndugu zetu waliochukuliwa kutoka Bara kwenda kupiga kura kujazia ‘ushindi’ wa Karume.
Kauli za viongozi wa serikali zinaanza kutufanya tuwe na imani ndogo nayo. Ndizo zinampa jeuri hata Gavana wa Benki Kuu, Daudi Balali, kutamba hadharani kwamba hawezi kujiuzulu kwa kutuhumiwa. Sasa anataka ajiuzulu kwa kitu gani? Hata kama ni ushahidi, utapatikanaje akiwa ofisini humo humo? Nani ataamini uchunguzi wa serikali inayojichunguza, huku ofisa anayechunguzwa akiwa bosi?
Hivi tujiulize, Balali akijiuzulu taifa litakosa nini? Ni wazi kwamba kujiuzulu kungelinda heshima ya taasisi anayoiongoza na heshima yake binafsi.
Maana angetuonyesha kuwa hana anachoogopa wala anacholinda, lakini kwa kuwa tuhuma zimekuwa nzito, na kwa vile yeye ndiye kiongozi mkuu, hata kama hahusiki moja kwa moja, anapaswa kuwajibika.
Kauli ya Balali imenikumbusha ile iliyotolewa na Idd Simba alipokuwa Waziri wa Viwanda na Biashara mwaka 2001. Alipobanwa kuhusu sakata la tuhuma za rushwa katika vibali vya sukari, akaombwa ajiuzulu alisema hakuwa tayari kujiuzulu hadi aliyemteua atakapoamua kumwondoa.
Wakosoaji walisema jeuri ya Simba ilikuwa na kitu nyuma yake. Ikaja kudhihirika baadaye. Alipojiuzulu Novemba 6 mwaka 2001, lakini bosi wake Rais Benjamin Mkapa alimwomba abaki na uwaziri wake hadi Novemba 16, ili kwanza aliwakilishe taifa katika mkutano wa WTO huko Doha, Qatar.
Hatua hii ilitushangaza wengi ambao hatukujua kilichokuwa kinaendelea hadi miaka miwili iliyopita Simba alipoamua kusema kilichotokea, kwamba si yeye aliyeruhusu utoaji wa vibali vya sukari bali ni uamuzi wa kikao maalumu kilichomhusisha Rais Mkapa, Simba na Mwanasheria Mkuu wakati huo, Andrew Chenge.
Hivyo, tunapoona jeuri ya sasa ya gavana wa Benki Kuu, tunapata tafsiri kwamba anajua Rais Jakaya Kikwete hawezi kuchukua hatua yoyote kumwondoa kwenye nafasi yake, sana sana atamkingia kifua ili astaafu kwa amani hapo mwakani.
Ni kauli inayoonyesha kuwa ana ubia katika uongozi wa nchi, ingawa Rais Kikwete alishasema kuwa urais wake hauna ubia na mtu yeyote isipokuwa makamu wa rais. Ni kauli, si vitendo.
Kauli ya Balali inaleta hisia kwamba anajua wakubwa watamkingia kifua; maana wasipomlinda naye hatakuwa tayari kuwalinda, kwani anajua wanaohusika.
Lakini jeuri hii inakuzwa na kinga waliyopewa wakubwa kutoshitakiwa. Maana kama huwezi kumshitaki rais mstaafu, ni wazi kuwa huwezi kuwashitaki walioshirikiana naye.
Hebu tafakari jinsi mtu mkimya na mpole wa aina ya Daudi Balali anapojitokeza hadharani kwa mbwembwe na kusema: “Sing’atuki ng’o!”
Mtu wa namna hii ameshasoma upepo, ameshawasiliana na wahusika wengine, anajua msimamo wa wakubwa, na ameshasoma mazingira.
Si ajabu anajua hata matokeo ya uchunguzi utakaofanyika.
Simwelewi Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, kwa kuligomea Bunge kuunda kamati ya kuchunguza tuhuma zinazomkabili gavana wa Benki Kuu.
Simwelewi Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kuwa kunyong’onyea mara na kushindwa kuunda kamati ya Bunge, eti kwa vile serikali imesema haipendi kuundwa kwa kamati hiyo. Yaani spika alikuwa anasubiri ruhusa ya waziri mkuu kuunda kamati ya kuichunguza taasisi ya serikali? Bunge linaongozwa na spika au waziri mkuu?
Kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni anaweza kulizuia Bunge kufanya kazi yake, basi hatuna sababu ya kuwa na Bunge.
Namna hii tunauvalisha ufisadi suti maridadi kama za Chiluba, lakini tujue kwamba watu wanaona na hawaridhiki, na ipo siku ‘maradhi mabaya’ yatatufika na sisi. Tutambue kuwa watu hawa wana nguvu ya ajabu ambayo hawajaamua kuitumia, na kwa matendo yetu wenyewe tunawahamasisha kujikusanya.
Tutambue kuwa kwa kiburi na jeuri yetu, tunajenga taasisi mpya katika hulka za watu wetu, katika kizazi tofauti ambacho kina uhusiano na shida na dhiki wala si itikadi za vyama.
Tujue kwamba watu hawa wanajua kwamba wanaibiwa, na wanaowaibia wanajiwekea sheria za kutoshitakiwa, au wanawakingia kifua watuhumiwa wengine, huku dola ikiwatia hatiani na kuwafunga maisha wanaoiba kuku na mikufu ya dhahabu ili kukidhi njaa.
Ni kizazi kinachotaabika, kilichozungukwa na rasilimali nyingi, huku tukiambiwa nchi yetu ni maskini, serikali haina uwezo; lakini tunaona wakubwa wanavyotumbua raha na starehe kama vile hawatakufa.
Ni kizazi kinachoelekea kukata tamaa, kinachoanza kupoteza imani na viongozi wetu kwa sababu maneno yao na matendo yao; bajeti zao na maisha yao, havifanani.
Ni kizazi kisichoridhika na maelezo ya serikali inayoweza kumlipa mwalimu, au nesi, au sekretari, au askari polisi, mshahara wa mwezi mmoja (siku 30) unaolingana na posho ya mbunge ya siku moja?
Hata wafanyakazi wa CCM makao makuu wananung’unika kwa kulipwa shilingi 30,000 kwa mwezi, huku wakijua kuwa chama chao kinapokea ruzuku ya takriban shilingi bilioni moja (1,000,000,000) kwa mwezi; na wanashuhudia baadhi ya maofisa wa chama wakilipwa posho nono ya safari ya siku moja inayolingana na mishahara ya wafanyakazi 10 kwa mwezi?
Kama tungewauliza walalahoi hawa iwapo kuna haja ya gavana wa Benki Kuu kujiuzulu ili ufanyike uchunguzi huru na wa haki, jibu linafahamika. Wanamshangaa Balali anayesubiri kujiuzulu baada ya kutiwa hatiani? Utatiwaje hatiani bila kuchunguzwa? Na utachunguzwaje kwa haki ukiwa ofisini?
Je, tumshitaki rais mstaafu anapotuhumiwa kutuibia? Ndiyo. Ndiyo njia pekee ya kuthibitisha usafi au uchafu wake.
Ndiyo njia pekee ya kurejesha imani na amani miongoni mwa wananchi wanaoanza kukata tamaa na hata kuwachukia watawala wao. Ndiyo njia ya kurejesha utawala bora na misingi ya haki.
Kama rais mstaafu anafariki dunia na nchi inabaki na amani, kwa nini ivurugike kwa sababu ya yeye kushitakiwa kwa makosa aliyotenda? Tukiweka utaratibu huu wa kuwashitaki wastaafu waliotenda maovu makusudi wakiwa madarakani tutakuwa na hakika kwamba hata walio madarakani leo watajihadhari, wataongoza kwa uangalifu na uadilifu wakijua kwamba hawako juu ya sheria kwa kuwa nchi si mali yao, ni ya wananchi, wao ni watumishi.
Watajua kuwa yanayompata Chiluba leo yanaweza kuwapata na kuondoa fahari ya miaka 10 ya mbwembwe zitokanazo na ufisadi ndani ya mfumo unaotawala, unaowalinda wakubwa na kuwamaliza wadogo.
Nina hakika kwamba huko tunakoelea, sheria tunazotunga hizi za kulindana zitafutwa, ama kwa nguvu au kwa hiari.
ansbertn@yahoo.com www.ngurumo.blogspot.com