Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Dk. Shein vitani urais Zanzibar
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Dk. Shein vitani urais Zanzibar
By Marshy Abdu | Published  07/16/2007
FITINA za Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Zanzibar kwa mwaka 2010, zimeanza ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar.

Tayari wafuasi wa makundi matatu yenye nguvu yaliyo ndani ya chama hicho wameanza kutambiana huku mabingwa wa propaganda wa makundi hayo wakieneza sumu dhidi ya vigogo wa siasa za Zanzibar wanaotajwa kuwa wanajiandaa kumrithi Rais Abeid Amani Karume.

Makundi hayo yamejidhihirisha wazi wakati wa upitiaji majina ya wana CCM wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi wa chama visiwani Zanzibar.

Kazi kubwa inayofanywa sasa na mabingwa hao wa propaganda kutoka kila kundi ni kuhakikisha wanaibuka na viti vya kutosha katika Halmashauri Kuu (NEC) katika Uchaguzi Mkuu wa chama unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Wafuasi waliojitokeza wazi kuanza kazi hiyo rasmi ni wale wa Rais mstaafu, Salmin Amour, ambao sasa wanampigia debe Waziri Kiongozi mstaafu Mohamed Gharib Bilal, kundi la pili ni Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Mohamed Aboud na kundi la mwisho ni la Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein.

Mchuano mkali wa makundi hayo ulianza kuonekana jana katika kikao cha siku mbili cha kupitia majina ya wagombea, wakati wajumbe wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar walipoanza kikao Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui.

Ajenda kuu katika kikao hicho ilikuwa kupitia majina ya watu waliojaza fomu kuwania ujumbe wa NEC, wenyeviti wa CCM wa mikoa na wilaya, makatibu wenezi wa mikoa na makatibu wa uchumi na fedha wa mikoa.

Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho cha siku mbili, walisema kwamba mtihani mgumu utakuwa katika zoezi la utiaji alama za wagombea katika nafasi za ujumbe wa halmashauri kuu, kwa vile watu waliojitokeza ni wengi na wenye ushawishi mkubwa ndani ya chama, ikilinganishwa na nafasi zinazohitajika. wakiwemo wanaowania nafasi hizo kwa kutegemea viongozi waliopo madarakani kama kinga yao kutokana na uchanga wao katika siasa za CCM.

Lakini kikubwa katika kikao hicho ni harakati za baadhi ya wagombea na wapambe wao za kuhakikisha wanapata idadi kubwa ya wajumbe, kwa madai kuwa ndiyo turufu itakayotumika katika safari ya uteuzi wa mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, huko Dodoma mwaka 2010.

Aidha, baadhi ya wajumbe walieleza kuwa wingi wa wajumbe katika vikao mbalimbali vya chama hicho unasaidia kurahisisha mikakati ya kuwaangusha baadhi ya wagombea wenye mitazamo ya kugombea urais kwa kujenga hoja kwamba hawakubaliki miongoni mwa wanachama walio wengi muda wa kutafuta mgombea utakapowadia.

Jana, Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alieleza kuwa kikao hicho kilikuwa na jukumu la kujadili majina ya wana CCM waliomba nafasi za uongozi ndani ya chama na kuwasilisha mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, na baadaye orodha hiyo kupelekwa Kamati Kuu ya CCM.

Kikao hicho ambacho kiko chini ya uenyekiti wa Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais Amani Karume, kilitanguliwa na kikao cha Sekretarieti kilichoketi chini ya Mwenyekiti wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz.

Baadhi ya wafuatiliaji wa siasa za Zanzibar wanaeleza kuwa kundi la Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein lina nafasi nzuri zaidi ya kupitisha wajumbe wengi kwa sababu linaweza kutumia nafasi ya uenyekiti ya Rais Karume kuhahakisha hilo.

Kwa upande mwingine, kundi la Dk. Salmin nalo linajigamba kwamba hadi sasa ngome yake ni imara kwa vile katika kipindi cha uongozi wa Rais Karume limekuwa karibu na serikali zaidi kuliko chama na hivyo kuchelewa kujenga ngome ya kisiasa.

Hata hivyo ukweli usiopingika ni kwamba kundi la Dk. Salmin ambaye ameondoka madarakani kwa muda mrefu, bado linaonekana kuwa na nguvu na mvuto kwa upande wa Zanzibar.

Kundi hilo hivi sasa inadaiwa kuwa litamsimamisha kwa mara nyingine Dk. Mohammed Gharib Bilal, limezidi kuwa na nguvu katika siku za karibuni baada ya kurejea nchini kwa Dk. Salmin Amour akitokea nchini China kwa matibabu.

Lakini kinachonogesha zaidi mchuano huu ni baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ambao wapo ndani ya makundi hayo kuonekana Zanzibar wakati huu kikao cha Bunge kikiendelea, wakiwapigia kampeni baadhi ya wagombea.

Baadhi ya wajumbe hao wamekuwa wakieleza kushitushwa kwao na ziara za wazee wa CCM na jumuiya za chama za mikoa mitano ya Zanzibar waliokuwa wakimtembelea Rais Karume kwa kile kinachoitwa kumjulia hali tangu kurejea nchini akitokea Ujerumani alikotibiwa macho.

Mjumbe mmoja wa NEC katika kikao hicho alisema kwamba ziara hiyo pamoja na kumjulia hali lakini ilikuwa na malengo ya kujiimarisha kisiasa, kwa vile imekuja siku chache kabla ya kufanyika kikao hicho cha kupitia majina ya wagombea Zanzibar.

Kundi la mwanasiasa kijana, Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Mohammed Aboud, ambalo linaonekana kuungwa mkono zaidi na siasa za Tanzania Bara, nalo linaoneka kufanya vema kampeni zake.

Hoja kubwa ya vigogo kutoka Bara wanaompigia debe Aboud ni ile ya kupata mgombea kutoka Pemba ili kupunguza nguvu za kambi ya upinzani Pemba.

Hoja hii inaonekana kuwa nguvu kwa baadhi ya Wazanzibari, huenda ikatumika kama ajenda kuu ya kupitisha muda utakapofika kwa kufunika madai ya Wapemba kutengwa katika nafasi ya kuteuliwa kugombea urais wa Zanzibar.

Mtazamo huo hauna tofauti na ule uliojitokeza sasa wa watu wanaompigia debe Makamu wa Rais, Dk. Sheni ambaye pia anatoka Pemba, anayedaiwa kuwa chaguo la Rais Karume kama mrithi wake kutokana na kipimo cha ukimya na busara.

Hata hivyo, baadhi ya wajumbe wamesema hawana wasiwasi na maamuzi ya Zanzibar, kwa vile ni mapendekezo yasiyokuwa na nguvu za maamuzi, kulingana na mambo yaliyojitokeza wakati wa mchakato ya kumpata mgombea urais wa CCM ambapo maamuzi ya mwisho hufanyika Dodoma.

Licha ya Waziri Kiongozi wa sasa, Shamsi Vuai Nahodha kutoonyesha dalili wala za iwapo anakusudia kuwania nafasi hiyo au la, kuna shinikizo kubwa la baadhi ya wanasiasa na wazee kutoka Mkoa wa Kusini Unguja la kumshawishi Nahodha kugombea urais kwa kile kinachoelezwa na baadhi wakereketwa wa chama hicho kuwa amepata uzoefu mkubwa na bado ni kijana hivyo anao uwezo mkubwa wa kihimili mikikimikiki ya uongozi.

Hata hivyo, wanasiasa wakongwe wa Zanzibar wanaeleza kuwa kugawanyika kwa wazee wa chama Zanzibar kunaweza kusababisha athari kubwa na kunufaisha baadhi ya makundi, hasa kama watathubutu kumtaka Rais Karume abadilishe katiba ili aendelee kuongoza katika kipindi kingine.

Kumekuwepo tetesi za wazee kumtaka Rais Karume aendelee kwa vile ameonyesha uwezo mkubwa wa kiutendaji, na kwamba hawaoni mtu anayeweza kuendeleza mafanikio makubwa aliyoyapata.

Rais Karume mwenyewe licha ya kukiri hadharani kwamba kuna wazee wanamshawishi afanye utaratibu wa katiba ili aendelee na wadhifa huo, anasema kwamba haoni sababu ya kufanya hivyo.

Katika uchaguzi mkuu wa CCM kuna kila dalili kuwa ushindani mkubwa utakuwa katika nafasi 20 za kapu Zanzibar, ambapo vigogo wengi wamekimbilia kundi hilo, wakiwemo hao wanaonyemelea nafasi ya urais.

Baadhi ya waliokimbilia kundi hilo ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz, ambaye katika uchaguzi uliopita aliangushwa kupitia mkoa na kuinuka kwa uteuzi wa mwenyekiti wa chama, baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar.

Katika kundi hilo pia wamo, Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein, Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Brigedia mstaafu Adama Mwakanjuki.

Viongozi wengine wanaogombea kupitia mkoa ni Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna, Kaskazini Unguja, Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Mohammed Aboud, Kusini Pemba na Naibu Waziri wa Miundombinu, Maua Daftari, Kaskazini Pemba.

Idadi kubwa ya wanachama wanaowania nafasi za mikoa imeelezwa ni mkakati maalumu wa kwenda kuwapunguza nguvu wanasiasa wanaojipanga kufikia malengo ya urais 2010.

Dk. Bilal hadi sasa anapewa nafasi kubwa na wanachama wa CCM Zanzibar chini ya kivuli cha Dk. Salmin, ambaye hadi sasa wanachama wengi wa CCM Zanzibar wanaamini kuwa kikwazo kikubwa cha kupitisha mtu wake, alikuwa Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Jambo kubwa linalomuweka Dk. Bilal katika nafasi hiyo kubwa ni kule kuongoza kura za maoni Zanzibar mwaka 2000 na baadaye likarudi jina la Rais Karume.

Pia umaarufu wake unachangiwa na kuondolewa kwa lazima jina lake usiku wa kuamkia siku cha kupiga kura huko Dodoma, jambo ambalo wafuatiliaji wa siasa za Zanzibar wanadai kuwa linazidi kuthibitisha nguvu zake, lakini amekuwa akianguka kimkakati.

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.