Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Ziara za mawaziri mikoani ni ufujaji wa fedha
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Ziara za mawaziri mikoani ni ufujaji wa fedha
By Marshy Abdu | Published  10/5/2007
MAPEMA wiki hii serikali iliwatawanya mawaziri na manaibu mawaziri na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mikoani, kwa maelezo ya kwenda kuelezea wananchi ubora wa bajeti ya mwaka 2007/2008.

Uamuzi huo wa serikali kuwapeleka viongozi hao mikoani, umezua mjadala mpya hapa nchini, kwani wananchi wa kada mbalimbali wamekuwa wakihoji manufaa ya ziara hizo kwa umma, kwa kuwa zinatumia fedha za walipa kodi, ambao wengi wao ni walalahoi.

Baadhi ya wananchi wamesikika wakieleza kuwa ziara hizo zimedhihirisha ni jinsi gani serikali ilivyokumbwa na kiwewe kutokana na sumu iliyomwagwa na wapinzani waliofanya ziara katika mikoa mbalimbali nchini.

Kwa upande wetu tunapingana na hatua ya serikali kuamua kuwatawanya mawaziri mikoani kuelezea uzuri wa bajeti, kitendo hicho ni ufujaji wa fedha za walipa kodi.

Hatuna hakika kama ziara hizo zina lengo la kueleza uzuri wa bajeti ya mwaka huu, kwani kuna taarifa zinazodai kuwa ni njia mojawapo ya kujipigia kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ndani ya chama hicho (NEC) unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.

Kama ni uzuri na ubaya wa bajeti, tayari wananchi wameishaujua tangu ilipopitishwa bungeni Julai mwaka huu, kwani ni dhahiri kwamba baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo gharama za maisha zimepanda na hali ya maisha kuwa ya juu.

Hatuelewi hawa mawaziri sasa wanakwenda kuwaeleza wananchi kitu gani wasichokifahamu, angalau ingekuwa na maana kama ziara hizo zingefanyika muda mfupi baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo.

Hata kama kungekuwapo ulazima wa kufanya hivyo, jukumu hilo wangeachiwa wabunge ambao si mawaziri, kwani tunaamini wana nafasi nzuri ya kuwafikia wananchi na kuwaeleza kwa kinaga ubaga.

Hapa ndipo unapoonekana umuhimu na kuwapo kwa mgawanyiko wa madaraka na si kwa kiongozi mmoja kuwa na vyeo lukuki. Hebu Watanzania tujiulize, hawa mawaziri waliotawanywa mikoani hawana majukumu mengine ya kitaifa ya kufanya katika wizara wanazoongoza?

Ni dhahiri zipo nyingi, na kwamba iwapo mawaziri hao wangetumia nafasi hizo wangesaidia kupunguza misongamano ya kazi za kila siku zinazowakabili.

Ieleweke kwamba Watanzania hivi sasa wanauelewa mkubwa, hivyo kitendo cha serikali kushindwa kutoa majibu thabiti kuhusu hoja za wapinzani, na badala yake kuamua kutumia ujanja wa kuwatuma viongozi wake kupunguza sumu ya wapinzani, kwa maelezo ya kueleza uzuri wa bajeti na kuwaponda wapinzani, ipo siku italeta madhara kwa viongozi hao.

Katika akili ya kawaida mtu mwenye njaa hawezi kucheza ngoma hata kama ni ya mfalme, sembuse bendi ya TOT-Plus? Ni dhahiri wananchi hawataweza kushangilia mikutano hiyo kwakuwa tayari wameishaona hakuna dalili za maisha bora kuwafikia.

Katika kuonyesha kuwa wananchi wamechoshwa na ahadi hewa na ambazo hazitekelezeki zinazotolewa na serikali, wananchi wamefikia hatua ya kuwazomea baadhi ya viongozi wa serikali wakiwemo mawaziri walioko katika ziara hizo.

Mawaziri ambao wamo kwenye ziara hizo ni Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika Stephen Wassira, Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, John Chilligati na Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Mohamed Aboud, na baadhi ya makada wa chama hicho Shaibu Akwilombe, Tambwe Hizza na Salim Msabaha, ambao walijiunga na CCM wakitokea kambi ya upinzani.

Hakika zomeazomea kwa viongozi haileti picha nzuri kwa jamii, hivyo serikali na CCM wanapaswa kujiuliza ni kwanini wananchi wamefikia hatua hiyo ya kuwazomea viongozi hadharani?

Tunasisitiza na kutoa ushauri kwa serikali, dawa ya hoja za wapinzani si kuwatoa ofisini viongozi hao wa serikali katika ofisi zao na kwenda mikoani kuhutubia wananchi, tena kwa kutumia fedha za walipa kodi na fedha za CCM , dawa ni kujibu hoja hizo kwa vitendo na si maneno ya kila kukicha.

Ili serikali iendelee kuaminiwa na kuheshimiwa na wananchi ni lazima itimize ahadi zake kwa vitendo na si maneno, kwani hayawasaidii kuleta maendeleo kwa wananchi ambao wamekwisha kuanza kuonyesha kukata tamaa.

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.