Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Njozi ya Karne: Tanzania baada ya CCM kung’olewa
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Njozi ya Karne: Tanzania baada ya CCM kung’olewa
By Marshy Abdu | Published  10/3/2007
Samson Mwigamba


NINA njozi ninayohitaji kuishiriki na Watanzania wenzangu. Njozi ni maono ya mambo yajayo, mambo yatarajiwayo katika siku za usoni.

Natamani wanasiasa wa kambi ya ushindani (si ya upinzani), waisome njozi hii kwa makini kwa kuwa ikikubalika kwa Watanzania walio wengi, wanasiasa hawa watakuwa na jukumu la kuhakikisha njozi hii inatimia.

Katika njozi hii ninaona Watanzania katika kila kona ya nchi yetu wakilia. Kilio chao wote kikiwa ni: “Watawala (si viongozi) wametutupa. Wamejitenga nasi. Wameweka pengo kubwa kati ya walionacho na wasiokuwa nacho. Tajiri wa Tanzania anazidi kuwa tajiri wakati maskini akizidi kuwa fukara.”

Naona Watanzania wakikata tamaa. Walio vijijini wanalia na kusema heri yenu mlio mijini. Wanafikiri watawala wamewekeza mijini, hivyo wanafanya bidii kuhamia mijini ili wapate hayo maisha bora wanayoyasikia kila siku kwenye vyombo vya habari.

Wanadhani ukifika tu mjini unapata kazi nzuri hata kama elimu yako ni Darasa la Saba maana mgombea urais aliyeshinda alitangaza kwamba akiingia madarakani atatoa ajira milioni moja kwa vijana (hakusema ni lazima wawe na elimu fulani).

Baada ya kupata kazi, nyumba nzuri ya umeme, kusafiri hata umbali wa kilometa mbili kwa gari, matibabu kwenye mahospitali makubwa na yenye hadhi kama Muhimbili, KCMC, Bugando, Ocean Road na raha nyingine za maisha, vinakuwa ni halali yako.

Walikuwa wamekosea. Walipofika mijini walikuta hali tofauti kabisa. Ajira milioni moja hazipo isipokuwa elfu kadhaa tu kwa vijana waliomaliza Kidato cha Sita waliopigwa msasa wa mwezi mmoja wakapelekwa kufundisha shule zinazoitwa za kata ambazo wengi wamekuwa wakiziita vituo vya kulelea watoto.

Kwa nini zisiwe vituo vya kulelea watoto ikiwa msichana niliyemfundisha twisheni mwaka 2003 akiwa Kidato cha Nne, mwaka 2006 akamaliza Kidato cha Sita. Mwaka 2007 akahudhuria hiyo voda fasta (kama wanavyoiita wao), alipomaliza akaripoti shule aliyopangiwa na wakajikuta wako walimu wawili tu tena wote ni wasichana na wote wametoka kwenye hiyo programu ya mwezi. Wakiwa wao tu na watoto wanachaguana, wewe uwe mkuu wa shule (headmistress) na mimi nitakuwa mkuu msaidizi (second mistress).

Vijana hawa kutoka vijijini wakakuta vijana wenzao wenye elimu za vyuo mbalimbali na hata vyuo vikuu wakizunguka na vyeti kila siku hadi soli za viatu zinaisha lakini kazi hawapati. Makampuni waliyotarajia yawaajiri yamebinafsishwa yote na kupunguza wafanyakazi wazalendo na kujaza wafanyakazi kutoka nje hata kwa nafasi za ngazi za chini kabisa. Hata shule za msingi zinazoitwa English medium zimejaza walimu kutoka Kenya na Uganda japo wengi wao wanachojua ni Kiingereza peke yake.

Vijana hawa wakaishia kuwa wamachinga na wapigadebe huku wakikumbana na virungu vya askari wa jiji kila uchao, kwa madai aidha ya kufanya kazi isiyotakiwa ama kufanya biashara maeneo yasiyoruhusiwa.

Wale waliojiajiri kwenye machimbo ya kokoto wakatimuliwa bila kupewa eneo mbadala au kazi mbadala. Wakaishia kuishi kwa mlo mmoja kwa siku ambao hata hivyo ni mhogo wa kukaanga (chipsi dume) na maji, na bado uhakika wa kuupata haupo.

Wakaishia kuishi kwenye nyumba za tope (mbavu za mbwa) zisizo na umeme na ambazo hata hivyo hawana pesa za kulipia kodi, hivyo ni kupanga hapa hadi mwenye nyumba amtimue kwa kutolipa kodi anahamia pale.

Ni vijana wa namna hii ndiyo ninaowaona wakiongoza na kuwa chachu ya mabadiliko. Ndiyo watakaoimba “Hakuna kulala mpaka kieleweke”. Sauti zao zinapokewa na wananchi wa kawaida kuanzia na wale walio katika maeneo yenye migodi ya madini hadi kwa wananchi wa hali ya chini mijini na vijijini.

Walio katika maeneo yenye migodi wanalia kwa kuhamishwa hovyo katika maeneo yao ili kupisha wawekezaji tena bila kulipwa fidia ya kueleweka. Kibaya zaidi hadi migodi itakapofungwa hakuna chochote watakachoambulia zaidi ya umaskini ulioongezeka na kazi ya kufukia mashimo.

Wakulima wakililia gharama za pembejeo zilizo juu wakati bei ya mazao yao ikishuka mwaka hadi mwaka na serikali ikiendelea kutumia mabilioni ya pesa kuendesha ‘mashangingi’ ya wakubwa na kuwapeleka wakubwa nje eti kuangalia tu afya zao badala ya kutumia pesa hizo kuwapatia wakulima pembejeo bure.

Wananchi wa hali ya chini mijini wanalia na ugumu wa maisha. Umeme hawana na walio nao hawamudu tena kuulipia, bei ya mkaa imepanda mara dufu huku mafuta ya taa nayo yakipanda. Nishati gani itakuwa kimbilio kwao?

Mbali na hilo, kutokana na bajeti muflisi iliyotangazwa na serikali yao, kila bidhaa imepanda bei. Wataishije? Kando yao wapo wafanyakazi waliodanganywa kwa tume ya kuangalia upya mishahara ya watumishi wa umma lakini wakaja kuongezewa sh,12,000 tu wakati mfumko wa bei ukipanda juu?.

Wananchi hawa walidanganywa kuwa ada ya shule za msingi imefutwa wakati michango wanayotakiwa kutoa ikiongezeka mara kumi ya hiyo ada waliyokuwa wanalipa.

Waliambiwa sasa ada ya shule za sekondari za serikali imepunguzwa hadi sh 20,000 kwa shule za kutwa na 70,000 kwa shule za bweni, lakini wakajikuta wakitakiwa kuchangia majengo, chakula, vitabu, n.k, na kufanya punguzo la ada waliloambiwa liwe ni ongezeko.

Wakaambiwa serikali itajenga shule kila kata, lahaula! kumbe wajenzi walikuwa ni wao tena sehemu nyingine kwa lazima kiasi cha kufungwa kamba kama wahalifu wa makosa ya jinai hadi hapo watakapotoa huo mchango wa sh 10,000, kiasi ambacho kwa baadhi ya wananchi wa vijiji vyetu ni zaidi ya pato lao la mwaka.

Naona sauti za kilio cha wananchi hawa maskini wa Mungu kikipanda kila siku mbele ya kiti cha enzi cha Muumba wao. Kisha kwa huruma Mwenyezi Mungu akaongea na wanasiasa wa kambi inayoitwa kimakosa ya upinzani na kuwaambia, “Ondoeni ubinafsi wa kila mtu kutaka kugombea urais maana nimewatuma kuwakomboa watu wangu wa Tanzania wanaoteswa na mafarao wa kisasa”

Ghafla wazo linawajia wapinzani wote wenye nguvu za kisiasa na wanaitana. Agenda ni moja tu, kulikomboa taifa. Njia ya ukombozi ni kuzunguka nchi nzima na kuwatangazia watu wote kwamba mwisho wa mateso yenu mbele ya mafarao umewadia. Sisi ndiyo kina Musa, Haruni, Joshua na Karebu wa leo tutakaowapeleka Kaanani ya leo. Wananchi wanaitikia kwa kishindo kikuu na kushangilia ujio wa akina Musa.

Vyama hivi vinashirikiana kwa kusaini mkataba utakaowaongoza katika mapambano haya mapya. Wanaanza kwa kuanika uozo wa viongozi wa serikali na chama tawala na madhila wanayowafanyia wabunge wa upinzani kwa kutetea ukweli japo ni wachache mno bungeni.

Kamati maalum iliyosheheni wataalamu wa mambo ya uchumi, siasa, utawala na sheria inaundwa. Kazi ya kamati hii ni kuunganisha sera za vyama vyote vilivyokubali kushirikiana na kutengeza sera moja itakayoongoza ukombozi wa kiuchumi chini ya serikali mpya ya umoja wa kitaifa.

Na wakati wa uchaguzi mkuu wanadhamiria kusimamisha mgombea mmoja katika kila ngazi kuanzia urais, ubunge hadi udiwani.

Naona muda wa kampeni ukiwadia. Kwa siku kama 70 hivi, bendera ya helikopta ya upinzani inapepea kila kona ya nchi yetu ikiwa imebeba tumaini jipya kwa watanzania zaidi ya milioni 35 wakati ‘mashangingi’ ya CCM yakivinjari maeneo yenye upinzani mkali ili eti kukomboa majimbo!

Kila mahali inapotua helikopta hii wananchi wanaipokea kwa shangwe na vifijo na kuimba kwamba helikopta pasua anga ya CCM, ukakisambaratishe kabisa chama kilichotekwa na matajiri na mafisadi.

Tangaza Azimio la Songea na katakata kamba za CCM zilizotufunga kwenye umaskini kwa miongo kadhaa. Wanaimba, “Mwaga CCM - mwaga, ahadi hewa mwaga – mwaga maisha bora hewa – mwaga na Kikwete mwaga, Kingunge mwaga na Lowassa -mwaga”

Siku ya uchaguzi kura zinapigwa. Jitihada zote za chama tawala kupata ushindi wa halali na usio halali (kwani kama waliibiana kura wao kwa wao kwenye uchaguzi wa ndani ya chama watashindwa kuiba za wapinzani wao?) zinashindikana kutokana na kiwango cha kura za upinzani na umakini wa wananchi kulinda kura zao.

Ndipo kwa kigugumizi kikubwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi analazimika kumtangaza kwa mara ya kwanza mgombea asiyetoka CCM kuwa mshindi wa urais na kuwatanganza wabunge kedekede kutoka kambi ya upinzani.

Baada ya kulihutubia Bunge, rais mpya anatangaza Baraza la Mawaziri dogo kuliko yote tangu tupate uhuru, lakini lenye sura ya kitaifa na lililojaa watu wenye uchungu na nchi hii. Baraza litakuwa na mawaziri sita tu na manaibu wao wasiozidi 10.

Wizara zitakuwa ni Uchumi na Mipango, Fedha, Mambo ya Ndani, Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Miundombinu. Kazi kubwa itafanywa na makatibu wakuu na wakurugenzi ambao ndiyo watendaji. Hivyo wizara za sasa hata zingeunganishwa tano kuwa moja bado inaweza kuongozwa vema na waziri mmoja.

Naona Tume ya Marekebisho ya Katiba inaundwa mara moja ikihusisha wajumbe kutoka kada mbalimbali kama vijana, wazee, akina mama, wanasiasa wa chama tawala na upinzani, walemavu, wanaharakati mbalimbali, wafanyakazi, wafanyabiashara, wachumi, wanasheria, wanataaluma na wakulima.

Lakini wakati tume hii ikiendelea kukusanya maoni, serikali inaanza kuchukua hatua za haraka za kurekebisha mambo yaliyokuwa yakilitia taifa hasara na ambayo hayahitaji marekebisho ya katiba, ikiwa ni pamoja na:

Kuuza kwa mnada ‘mashangingi’ yote ya serikali yapatayo 6,000 na kuwanunulia magari ya kawaida viongozi wa serikali, kurudisha nyumba zote walizojiuzia vigogo wakati wa Chukua Cha-umma Mapema (CCM) na kuondokana na gharama kubwa za viongozi wa serikali kuishi kwenye mahoteli.

Kupitia upya mikataba yote ya uchimbaji madini katika nchi yetu na kufuta vipengele vinavyoliibia taifa mapato, kuweka watendaji wa serikali kwenye vitengo vyote nyeti kwenye makampuni ya madini vya uzalishaji, usafirishaji na uuzaji madini ili kuhakikisha kile kinachoripotiwa ndicho hasa kilichopatikana, kupunguza idadi ya viongozi wanaoruhusiwa kutibiwa nje na wale watakaoruhusiwa itakuwa ni kwa magonjwa machache tu au katika mazingira maalum tu na kwa utaratibu mahsusi si daktari wa mhusika kuandika tu mapendekezo na mtu anachota pesa hazina. Matibabu hewa mwisho.

Kuweka udhibiti wa hali ya juu katika mapato yatokanayo na utalii na uvunaji wa maliasili zetu kama mistu, uvuvi, n.k. kuzidisha udhibiti wa makusanyo ya kodi na kufuta mara moja misamaha holela ya kodi kwa wafanyabiashara wakubwa, kupitia orodha ya watumishi wote wa serikali kwa umakini mkubwa ili kubaini wafanyakazi hewa ambao wamekuwa wakilipwa mishahara bila kuwa kazini.

Naiona katiba mpya ya nchi ikiwa imekamilika na kuridhiwa na Bunge maalum la Katiba. Katika katiba mpya mambo yafuatayo yamezingatiwa:

Kifungu kinachompa rais mstaafu kinga ya kutoshitakiwa kwa maovu aliyoyafanya wakati akiwa rais kimefutwa, madaraka makubwa aliyokuwa nayo rais ya kuteua mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa majiji,manispaa, miji na wilaya, makatibu tawala wa mikoa, mabalozi wa Tanzania nchi za nje, makatibu wakuu wa wizara, wakuu wa vyuo vikuu na taasisi nyingine za serikali, yamepunguzwa sana.

Watendaji wakuu wa vyuo vikuu vya umma na wa taasisi nyeti kama TANROADS, TBS, n.k, watateuliwa na tume ya utumishi wa umma kwa taratibu maalum na kwa kipindi maalum.

Uteuzi wa mawaziri, mabalozi, Jaji Mkuu, wakuu wa majeshi, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali, mkuu wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) na taasisi nyingine nyeti lazima uthibitishwe na Bunge na kuondolewa kwao kunalindwa na katiba, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa imekuwa huru, haiko tena chini ya ofisi yoyote ya Serikali na ni vivyo hivyo kwa Mahakama na Tume ya Uchaguzi.

Wenyeviti wote wa vyama vya upinzani vyenye wabunge wanakuwa moja kwa moja wabunge kikatiba na mwenyekiti wa chama cha upinzani chenye wabunge wengi ndiye anayekuwa kiongozi wa upinzani (safari hii atakuwa Mh. Jakaya Kikwete). Hii itaongeza demokrasia na mijadala iliyoshiba ndani ya Bunge.

Katiba imepitisha mfumo wa utawala wa majimbo na nchi imegawanywa katika majimbo yasiyozidi manane na kufanya vyeo vya ukuu wa mkoa na ukuu wa wilaya kufa kifo cha kawaida. Kila jimbo litakuwa na bunge lake na litaongozwa na gavana na timu ya watendaji.

Chini ya jimbo kuna halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji yenye mabaraza yake ya madiwani na kuongozwa na wakurugenzi watendaji na timu zao.

Kila jimbo linakusanya mapato kutokana na kodi, maliasili zake na vyanzo vingine na kupangilia matumizi yao kulingana na vipaumbele vyao kama elimu, miundombinu, mawasiliano, maji, umeme, viwanda, kilimo, n.k, baada ya kutoa asilimia 20 ya mapato yake kwa serikali kuu.

Mikataba yote itakayoingiwa kati ya majimbo na wawekezaji sharti iridhiwe na mabunge ya majimbo husika. Nafasi ya waziri mmoja kutoka sehemu moja ya Tanzania kwenda nchi za nje na kusaini mkataba unaohusu maliasili ya sehemu nyingine ya Tanzania ambayo huenda hajawahi hata kufika na hajui kiwango cha maliasili iliyopo pale na maisha ya watu wa pale, haipo tena. Ni wananchi wa pale kupitia wawakilishi wao (wabunge wa jimbo) ndiyo watakaoridhia ama kukataa mkataba husika.

Baada ya hayo naona majimbo yakiongozwa na wananchi wakazi wa majimbo husika na wenye uchungu na maliasili za majimbo yao. Wanazitumia vilivyo kujiletea maendeleo kwa sapoti ya serikali kuu ambayo hutoa ruzuku kubwa kwa majimbo yenye rasilimali kidogo na ruzuku kidogo kwa majimbo yenye raslimali nyingi kutegemeana na vipaumbele vya serikali kuu.

Tena ninaona majimbo yakishindana kuleta maendeleo kila moja likitaka kupata maendeleo kama jingine na lenye maendeleo zaidi likitaka kudumu kuongoza kwa maendeleo. Magavana wa majimbo ndiyo baadaye watakuja kuaminiwa na wananchi wa nchi nzima kuongoza taifa kutokana ma mafanikio waliyoyapata majimboni mwao.

Mikakati yote hii inaliongezea taifa mapato mengi na imani kubwa kwa nchi wahisani na kuongeza misaada kwa nchi. Hili linaiwezesha serikali kuongeza kima cha chini cha mishahara hadi laki tatu na ushee kwa mwezi, kutoa matibabu bure, kutoa pembejeo za ruzuku kwa wakulima bure, kutoa ufadhili kwa wanafunzi wote wasio na uwezo kwenye elimu ya juu, kusomesha watoto wa Tanzania elimu ya msingi hadi sekondari bure.

Pia serikali inapata uwezo wa kuwekeza katika tafiti mbalimbali na uhamishaji wa teknolojia (technology transfer).

Hili linafanyika kwa kuwatuma vijana wazalendo na wenye vipaji maalum kusoma na kutafiti katika mataifa yaliyoendelea.

Wanaporudi tunawapatia nyenzo ili waweze kubuni zana bora zaidi na za kisasa za kilimo, mifumo ya kilimo cha kisasa cha umwagiliaji, mitambo ya kusafisha madini, utengenezaji wa bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na vipuri vya magari, vifaa vya umeme na elektroniki, viwanda vya kusindika mazao, n.k.

Muda si mrefu tuna viwanda vyetu vikubwa vinavyoweza kutengeneza bidhaa mbalimbali na muhimu duniani na hivyo kuongeza thamani ya bidhaa tunazouza nje.

Tukifikia hapo tayari tutakuwa katika nchi za Dunia ya Pili – Tumepaa kutoka Dunia ya Tatu.

Kwamba Mungu wa mbinguni atusaidie Watanzania kuiona vema njozi hii na kutambua mabadiliko yaliyo ndani ya uwezo wetu na hatimaye tukaamua kuyafanya na kutimiza ndoto zetu kama taifa – ndilo ombi langu, Amen.

Makala hii imeandikwa na mwanaharakati wa mabadiliko anayesoma Chuo Kikuu cha Arusha.

Email: smwigamba@yahoo.com
Mob: 0784 815 499 au 0712 012 514

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Your Favorite Articles

View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
No popular authors found.