MWANASHERIA Mkuu wa kwanza mzalendo nchini, Jaji Mark Bomani, amewataka wanasiasa wanaotishia kwenda mahakamani kumshitaki Katibu Mkuu wa Chadema, Willibrod Slaa, kutokana na kuwashutumu kwa vitendo vya rushwa kutafakari upya iwapo kuna ulazima wa kuchukua hatua hiyo.
Bomani, mmoja wa wanasheria wanaoheshimika nchini, alitoa wito huo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam, kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu tuhuma za rushwa zilizotolewa na Dk. Slaa na viongozi wengine wa upinzani, takriban wiki mbili zilizopita.
“Kutokana na hali hii inayojitokeza, maombi yangu ni kwamba, tuwe wavumilivu wa kisiasa (political tolerance). Nawaomba ndugu zangu ambao wanatishana kushitakiana mahakamani wafikirie upya ulazima wa kufanya hivyo,” aliasa Jaji Bomani.
Alisema rushwa ni tatizo kubwa katika jamii ambalo linapaswa kupigwa vita kwa nguvu zote, na kwamba malumbano ya namna yoyote yanayoweza yakayumbisha jitihada hizi za kukabiliana na rushwa hayana budi kuepukwa kwa nguvu zote.
Alionya kuhusu kuwapo kwa uwezekano mkubwa kwamba malumbano haya yanayoendelea yanaweza kukua na kufikia kiwango cha kuleta mfarakano na uhasama katika jamii iwapo yatazidi kiasi.
Aidha, mwanasheria huyo aliyepata kuchukua fomu za kugombea urais wa Tanzania kupitia CCM mwaka 1995, alikiri kuhusu kupamba moto kwa malumbano kuhusu suala zima la rushwa.
Katika hilo, alisema hali hii ya kupamba moto inachangiwa kwa kiwango kikubwa na maamuzi ya watu kupinga kuwapo kwa rushwa hapa nchini, wakati hali halisi inathibitisha pasipo shaka kwamba tatizo hilo lipo.
Bila ya kutaja majina ya watu, Bomani alizungumzia kuhusu suala zima la Dk. Slaa kutaja hadharani watu wanaotuhumiwa kwa rushwa, alisema sheria inatoa uhuru kwa mtu kutoa maoni yake ama kwa maandishi au kwa mdomo.
“Labda tu niseme kwamba litakuwa ni jambo la kushangaza kwa mtu yeyote kutoa hisia kwamba uhuru huu haupo kisheria au haufai. Uhuru huu upo na unapaswa ulindwe,” alisema Bomani katika taarifa yake ya maandishi aliyoikabidhi kwa waandishi wa habari.
Kwa upande mwingine, Jaji Bomani aliwataka wananchi kuitumia Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 kukabiliana na vitendo hivyo kwa nguvu zote.
Akitoa mfano alisema chini ya sheria zilizopo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inao uwezo wa kumtaka kiongozi au mtumishi wa umma yeyote aeleze kuhusu mali zake zinazoonekana kutolingana na mapato yake halali.
Bomani anatoa kauli hiyo katika kipindi kisichozidi wiki moja tangu gazeti moja la kila wiki limkariri akisema kuwa hoja ya Dk. Slaa kuhusu tuhuma za rushwa zilikuwa ni legelege.
Katika hili, mwanasheria huyo alililaumu gazeti hilo kwa kumwekea maneno ‘legelege’ ambayo alisema hakuyatumia katika mahojiano yake ya maandishi aliyoyafanya na gazeti hilo linalochapishwa kila Alhamisi.
“Kwa mfano, sikumuonya Dk. Slaa na wala sikusema kuwa hoja zake ni legelege! Haya si maneno yangu, ni ya gazeti. Vilevile gazeti hilo limetaja jina la Zitto Kabwe, ambalo mimi sikulitaja katika mahojiano,” alisema Bomani.
Katika taarifa yake ya maandishi aliyosema ndiyo yaliyokuwa maswali na majibu aliyoyatuma kwa gazeti hilo, inaonyesha kuwa Bomani aliandika kuwa: “Shida kubwa ninayoiona ni kwamba, baadhi ya shutuma zilizotolewa na Dk. Slaa na wenzake ni za kijumla mno.”
Aidha, sehemu nyingine ya majibu yake hayo kwa gazeti hilo yanamkariri akisema kwa maandishi kuwa; Dk. Slaa na wenzake wana uhuru wa kutoa maoni yao kuhusu vitendo vya rushwa na ufisadi nchini.
Mwanasheria huyo pia amewalaumu wale wanaosema ni makosa kumtuhumu mla rushwa kabla ya kuwa na ushahidi wakati ukweli ni kwamba, sheria inasema bayana kwamba, mtu anayetuhumiwa kwa makosa hayo anahesabiwa kuwa mhalifu hadi hapo atakapojitakasa.
“Hivyo wanaosema kwamba ni makosa kumtuhumu mla rushwa mpaka kwanza ushahidi uwepo, wanaipotosha Sheria ya Kupambana na Rushwa. Sheria ya Rushwa ikitumiwa kikamilifu inaweza ikanasa wala rushwa wengi,” anasema Bomani katika maandishi yake hayo, yaliyotumwa kama majibu kwa gazeti hilo.