WANANCHI wa Wilaya ya Longido, mkoani Arusha, wameiomba serikali kutengua kibali cha uchimbaji wa madini cha Kampuni ya Mundarara Ruby Mining, kwa kuwa kampuni hiyo imeshindwa kuchangia maendeleo katika maeneo yanayozunguka mgodi huo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Mundarara, Diwani wa kata hiyo, Peter Sengui, wakati wa kikao maalumu na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Hawa Ghasia, alimwomba waziri huyo kufikisha kilio chao kwa Rais Jakaya Kikwete, ili afute mkataba huo.
Sengiu alimwambia Waziri Ghasia kuwa mkataba huo utaiwezesha kampuni hiyo kuchimba madini ya rubi yaliyopo katika kata hiyo kwa muda mrefu, huku wananchi wa wilaya hiyo wakiwa hawanufaiki na chochote kutoka katika mgodi huo.
Alisema hivi sasa madini ya rubi yana thamani kubwa nje kuliko hata dhahabu na yanapatikana kwa wingi katika mgodi huo, lakini kampuni hiyo haichangii kiasi chochote katika wilaya hiyo.
Aidha, Diwani wa Kata ya Kitumbeine, Joseph ole Saadira, alimwomba Waziri Ghasia kuangalia uwezekano wa kupeleka watumishi wa afya haraka katika wilaya hiyo, kwani licha ya kuhamasisha wananchi katika ujenzi wa zahanati lakini kumekuwa na ukosefu wa wahudumu.
Alitoa mfano wa kata yake ambayo ina vijiji vinne wamejitahidi kujenga zahanati katika kila kijiji, lakini ni zahanati moja tu ndiyo inafanya kazi na nyingine tatu zimefungwa kutokana na ukosefu wa wahudumu.
Alitaja vijiji vilivyoathirika na tatizo hilo ni Kijiji cha Noondoto, Elang'atadabashi, na Kitumbeine, huku Kijiji cha Kiseriani pekee ndicho kilicho na zahanati, hivyo kulazimu wananchi kutembea zaidi ya kilometa 40 kuifuata zahanati hiyo kupata huduma.
Waziri Ghasia, yupo katika ziara maalumu ya kutembelea wilaya zote za Mkoa wa Arusha kuzungumza na watendaji wa serikali na wa chama, kutoa ufafanuzi na kutoa maelekezo juu ya matumizi ya bajeti ya serikali ya mwaka huu.