Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Kwa nini tunawapinga?
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Kwa nini tunawapinga?
By Marshy Abdu | Published  10/3/2007
M. M. Mwanakijiji


TAIFA letu liko katika kipindi cha mpito. Kipindi cha kutoka mawazo ya chama kimoja kuelekea mawazo ya vyama vingi, na kutoka ukiritimba wa hoja za chama kimoja kwenda kwenye wingi wa hoja za vyama na vyanzo vingi.

Kiini cha kipindi hiki cha mpito ni mabadiliko makubwa ya kiteknolojia hususan kuenea na kusambaa kwa mtandao wa kiintaneti na upatikanaji wa simu za mkononi. Mabadiliko haya yamechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kisiasa ambayo hivi karibuni yamekuwa yakiwasha moto wa kizalendo ndani ya mioyo ya Watanzania.

Katika hili CCM wamechelewa na wako nyuma. Tatizo lao kubwa lililowafikisha walipo sasa ni kujiamini kuwa "ushindi wao wa kishindo" wa 2005 umewapa leseni ya kusema na kufanya lolote kwani wao ndiyo "chama kinachopendwa" ni "safi", na "wana ridhaa ya wananchi".

Walipomfungia Zitto kushiriki vikao vya bunge kwa kosa la "kusema uongo", walijihukumu wenyewe na sasa wanalipa gharama ya hukumu hiyo. Kwa miongo minne na miaka sita sasa, CCM na viongozi wake hawajawahi kupata changamoto kama wanayoipata sasa, na bila ya shaka "wakulu" wa chama hicho wanajiuliza "tumekosea wapi?" na bila ya shaka wanajiuliza "kwanini tunapingwa namna hii? Hatua ya kwanza kutatua matatizo yoyote yale ni kukubali kwanza kuwa kuna tatizo. CCM hadi hivi sasa hawajakubali kuwa wanakabiliwa na tatizo au matatizo licha ya ushahidi wote uliopo.

Matukio ya rushwa, kashfa za mikataba, ukiritimba wa chama n.k. ni miongoni tu mwa matatizo tunayoweza kuyataja hadharani na kwa haraka. Kwanini wananchi wanawapinga? Kwanini watu hawaogopi tena na wanaanza kuwahoji? Kwanini hadi vijijini wanakijiji wenzangu wameanza kuuliza "maswali ya ziada" ambayo huko nyuma majibu yake yalikuwa "yanafikirika?".

Tunawapinga kwa sababu moja kubwa – tunatofautiana nao. Msingi wa kulumbana na serikali na kufunua na kuchambua matendo yao ni tofauti iliyopo kati yetu na wao. Tofauti hiyo ni tofauti ya msingi (fundamental difference). Ni tofauti inayolingana na tofauti ya rangi nyeusi na nyeupe, usiku na mchana, mvua na jua, na Mashariki na Magharibi. Tofauti hiyo kubwa inatokana na tofauti katika mambo yafuatayo:

  • Tofauti ya kimtazamo

    Wakati CCM bado wanaiangalia Tanzania kwa mtazamo wa "wao ni watawala wasiopingika" na sisi wengine tumeanza kuiangalia Tanzania kwa mtazamo wa "CCM ni watawala wanaopingika". Katika hili wao wanapozungumza au wanapotenda sisi tunaangalia na kupima wanachozungumza na wanachotenda. Wanapotoa maelezo ya "kihuni" sisi tunawaambia kama maelezo yao ni "ya kihuni" hilo linawashtua!

  • Tofauti ya maoni

Wakati wao huko nyuma walijiambia kuwa maoni yao ndiyo maoni pekee ya kusikilizwa Tanzania, siku hizi wanashtuka kuwa maoni yao yana thamani kiduchu na yanachambuliwa kama maoni mengine yoyote yale. Huko nyuma walipoitisha waandishi wa habari au kutoa "taarifa kwa waandishi wa habari" basi mjadadala uliisha.

Sasa hivi, mjadala hauishi kwa vile "Rais kasema" au "Waziri Mkuu kasema". Wasipotoa majibu ya kueleweka au majibu yenye utata, watarajie kuwa watu watauliza maswali ya ziada. Ule ukiritimba wa mawazo ambao CCM ilikuwa nayo kwa muda mrefu kiasi cha kuamini kuwa wao pekee ndiyo wenye mawazo bora katika kuongoza taifa letu leo, unathibitishwa kuwa haukuwa na msingi wowote ule. Kashfa zinazowaandamana viongozi wake na watendaji wake ni ushahidi wazi kuwa kipindi cha utawala wa mawazo ya CCM kimekwisha na kipindi kipya cha mwamko wa kimawazo kimefika.

  • Tofauti ya mwelekeo

CCM inataka kuongoza kama ilivyoongoza huko nyuma na kwenda ilikotaka kwenda miaka 20 iliyopita.

Inasikitisha kuwa kwa chama kilichowahi kuwa cha "mapinduzi" leo hii kinashindwa kubadilika kwa haraka na kwenda na wakati mpya wa machipuko mapya ya kisiasa yanayoendelea Tanzania.

Kiini cha machipuko hayo ni mchango mkubwa wa waandishi na wajenga hoja mbalimbali ambao siku za hivi karibuni wamefungua kwa namna ya pekee mawazo ya Watanzania kuangalia ni wapi tunataka kwenda na ni wapi tunapaswa kwenda.

Uzembe, kulindana, kufichana na kubebana kulikokuwa kunafanywa na CCM kwa muda mrefu sasa kumeanza kuwatokea puani. Leo hii walipodhania kuwa "orodha ya ufisadi" ya muungano wa upinzani ilikuwa ni propaganda za kuchafuliana majina, na ambayo inapaswa "kupuuzwa", sasa wanajuta kwanini hawakuitilia maanani, na waliotajwa mmoja mmoja wanaanza kujaribu kujitetea na kati yao wengine hawajui kama ni waadilifu wamebakia kuwa na "imani" kuwa wao ni waadilifu.

Kuchanganyikiwa huku ni jambo jipya, na ni mwanga katika chumba chenye giza! CCM wamechanganyikiwa. Hata hivyo, huu ni mwisho wa CCM na anayedhania kuwa CCM imefika mwisho ni bora aamke. CCM bado ina uwezo na nia ya kufanya mapambano haya ya kifikra na kisiasa. Hata hivyo gharama kubwa itabidi wailipe kuweza kurudisha imani kwa wananchi. Sehemu kubwa ya gharama hiyo inahusu uwazi, ukweli, na kujisafisha.

Haitoshi kukanusha tuhuma au kuzipuuzia. CCM ijiangalie tangu ndani na kuona ni wapi kuna udhaifu na ni wapi kunakovuja kiasi cha kuhitaji kutengenezwa mara moja. Kwa kadiri ambavyo viongozi wa CCM bado wako kwenye hatua ya kukana ndivyo hivyo fikra za mabadiliko zinavyozidi kukita katika mioyo ya watu.

Kwenye hili CCM wameshindwa kuongoza na sasa wanajikuta wanafuata. Ni kiburi chao na ubabe wao ndio unaowaumbua sasa, na ni shimo hili ambalo wao wenyewe wamelichimba wakitumaini wapinzani watatumbukia. Bahati mbaya ni wao walioanza kutumbukia na walipotarajia kuwa wapinzani wataanza kuwafukia, wanajikuta ni wao wenyewe ndio wanaoanza kufukiana huku wapinzani wakikaa pembeni wakicheka kuwa "CCM wamelikoroga wenyewe na sasa wanalinywa".

Kwa kadiri siku zinavyoendelea ndivyo hivyo vuguvugu la mabadiliko ya kisiasa linavyozidi kupamba moto. CCM wako kwenye kona ya ulingo wa kisiasa huku wapinzani wakiendelea kurusha makombora ya ngumi. Kama wapinzani wanadhania kuwa CCM imeanguka chini na iko tayari kwa ‘knockout’.. wasijidanganye.

CCM itajikusanya na kujiandaa kujibu mapambano kwa nguvu na kwa haraka. Wakosoaji tujiandae for the ‘final showdown! I’m ready... are you?’

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.