Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Tatizo si HakiElimu ni wanasiasa waoga
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Tatizo si HakiElimu ni wanasiasa waoga
By Marshy Abdu | Published  07/12/2007

MIAKA zaidi ya 10 iliyopita, msomi maarufu nchini na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kisheria, Profesa Issa Shivji, alisema: “Wanasiasa hawapendi siasa, wanapenda madaraka.”

Mwanazuoni huyo alitoa kauli hiyo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka ya mwanzoni mwa 1990 wakati Tume ya aliyekuwa Jaji Mkuu, Francis Nyalali ilipokuwa ikikusanya maoni ya Watanzania kuhusu mfumo wa kisiasa waliokuwa wakiutaka; vyama vingi au chama kimoja.

Kabla ya kutoa maoni hayo, Shivji aliyekuwa akizungumza katika hadhara ya wasomi waliokuwa wamekusanyika katika Ukumbi wa Nkrumah chuoni hapo, alisema wasomi ndio wanaopenda siasa, ingawa kwa kawaida wamekuwa ni watu wasio na tamaa ya madaraka.

Miaka zaidi ya 15 leo, tafakuri ya msomi huyo inabakia kubeba ujumbe mzito unaojidhihirisha katika maisha ya kila siku, hasa kwa upande wa wanasiasa wetu.

Limekuwa ni jambo la wazi kabisa kwamba, hulka ya wanasiasa kupenda madaraka kupita kiasi, imekuwa ni chanzo kikuu cha matatizo makubwa yanayolikabili taifa hili kwa miaka nenda, miaka rudi.

Ushahidi wa ukweli huo uko bayana kabisa na unajidhihirisha kwa namna mbalimbali miongoni mwa wanasiasa wetu ambao wengi wao wamejijengea mwiko wa kulinda madaraka yao kwa gharama zozote zile.

Leo unapoliangalia tatizo la Zanzibar ambalo vyama vikuu viwili, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) wanalitafutia ufumbuzi, utabaini sababu kuu iliyovilazimisha vyama hivyo vikutane na kujadili ni madaraka.

Mwenendo wa chaguzi tatu za vyama vingi unathibitisha pasipo shaka kwamba, ugomvi baina ya vyama hivyo ni kila mmoja kujiona akiwa na haki kuliko mwingine ya kutawala na kuwa na madaraka.

Kwa sababu hiyo basi, kikubwa kinachozua mzozo na mivutano isiyokwisha baina ya vyama hivyo viwili nje na ndani ya majadiliano yao hayo ni shauku ya kila mmoja kujiona akipata fursa ya kunyakua madaraka.

Hulka hiyo hiyo ya wanasiasa kuamua kuyalinda madaraka yao kwa gharama zozote zile ndiyo zimekuwa chachu za kukithiri kwa rushwa, wizi wa kura na ubadhirifu wa mali ya umma katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Kimsingi ni sababu hizo hizo za wanasiasa kupenda madaraka ndizo ambazo leo hii zimekuwa zikisababisha viongozi wa kisiasa serikalini na wakati mwingine wabunge kufikia hatua ya kuiona taasisi isiyo ya kiserikali ya HakiElimu kuwa ni tishio, si la maendeleo ya taifa hili, bali la madaraka ya kundi fulani la watu.

Uamuzi wa wabunge wawili wa CCM, kuishambulia taasisi hiyo bungeni, hata kufikia hatua ya kuionya serikali kuwa inaweza ikawa katika hatari ya kuangushwa, ni matokea ya wanasiasa kuweka mbele madaraka kuliko madhila yote mengine ya kijamii.

Kauli za Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai (CCM), anayebeza matangazo yanayotolewa na HakiElimu na ile ya Janet Masaburi (Viti Maalumu-CCM) kuungana naye ni ushahidi unaoonyesha namna wanasiasa wetu walivyo tayari kulinda masilahi ya kiutawala kuliko ugumu wa maisha wanayokabiliana nayo watoto wa Kitanzania kielimu.

Sisi tunaamini kwamba matangazo na machapisho mbalimbali ya kielimu yanayotolewa na HakiElimu yanapaswa kuwa changamoto kwa wanasiasa kufikiri sawasawa kwa ajili ya maendeleo ya elimu ya watoto wao katika misingi sawa na isiyopendelea kundi fulani tu la watu.

Pamoja na kutambua na pengine kukubali kuwa matangazo ya HakiElimu yanaweza yakawa ama hayajitoshelezi, hayaelezi ukweli kamili au yana upungufu mwingine, bado mtazamo wa kuyapima kwa namna yanavyoweza yakawa na athari kwa serikali iliyo madarakani tu na kusahau mahitaji mengine muhimu ya kijamii, ni jambo ambalo halipaswi kukubalika.

Tunasema hivyo tukiamini kwamba, iwapo kweli matangazo au machapisho ya taasisi hiyo yatakuwa na nguvu ya kujenga ushawishi unaoweza kuiondoa serikali madarakani kwa njia ya kidemokrasia, hilo wala halipaswi kutafutiwa ufumbuzi kwa kuifuta taasisi hiyo.

Iwapo kweli wabunge wa CCM kama kina Ndugai na Masaburi wanaamini kuwa HakiElimu inao ushawishi mkubwa kiasi hicho, basi wanachopaswa kufanya wao ni kuisaidia serikali kufanya marekebisho ya mambo ya kielimu yanayolalamikiwa kupitia katika matangazo na machapisho ya taasisi hiyo.

Kwa sababu hiyo basi, jibu zuri kwa wabunge wa CCM na serikali yao ambayo mara mbili huko nyuma imewahi kupiga marufuku machapisho ya taasisi hiyo ni kuyafanyia kazi kwa kina yale yote yanayotolewa na HakiElimu badala ya kuanza kujenga mazingira ya kuipiga marufuku na pengine kuifungia kabisa taasisi hiyo.

Wabunge na wanasiasa wengine kwa ujumla wanapaswa kutambua kuwa, jukumu la kuikosoa serikali iliyo madarakani si dhamana ya vyama vya siasa peke yake, bali inapaswa kubebwa na kila mmoja anayeitakia mema nchi hii.

Hii hulka ya baadhi ya wanasiasa wa CCM ya kutaka HakiElimu ikajisajili kama chama cha siasa cha upinzani na wakati mwingine kuvifananisha vyombo vya habari na vyama vya upinzani inapaswa kukemewa kwa nguvu zote.

Wanasiasa wenye mtazamo hasi wa namna hiyo wanapaswa kutambua kuwa taasisi zisizo za kiserikali kama HakiElimu, zina wajibu mkubwa wa kisheria wa kufanya kazi za kuisaidia serikali kwa njia ya kuionyesha njia, lengo likiwa ni kuliondoa taifa katika uduni wa kielimu na kimaisha na kwamba wajibu huo si wa wabunge na wanasiasa walio madarakani.

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.