Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Wapinzani ndio wenye uchungu na taifa hili?
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Wapinzani ndio wenye uchungu na taifa hili?
By Marshy Abdu | Published  10/3/2007
Gervas Zombe


MCHAKATO wa kuboresha maisha kwa Watanzania unaoendelea miaka hadi miaka, ni kama hadithi inayofurahisha, kuhuzunisha na kufikirisha pia.

Wanaofuatilia ahadi za viongozi, hotuba za viongozi, wanasiasa na hata wabunge wakiwa bungeni watakubaliana nami.

Wingi wa kauli na ahadi za viongozi tayari ni maendeleo tosha kabla hata ya kufanya lolote.

Tumesikia kutoka kwa viongozi na wanasiasa nahau za kila namna, methali, vitendawili, hadithi, kejeli na hata ngojera, lakini bado dhiki za Watanzania wengi ziko palepale.

Wanasiasa na viongozi wa vyama na serikali kauli na matamshi yao, yanaonekana yanashabihiana kuwa na lengo moja la kuboresha maisha kwa Watanzania. Lakini utekelezaji wake kwa vitendo, hapo ndipo kila mmoja anatafuta njia yake.

Na kutokana na njia hizi kuwa nyingi, zinazaa mijadala isiyo kwisha. Huku wananchi wengi wakiogelea kwenye dimbwi la umaskini. Na inaonekana walio nje ya mfumo wa uongozi wanauona udhaifu wa walio ndani kwa jicho pevu. Je, jicho hilo pevu linawasaidia wao au wananchi?

Haya yote yanafanyika huku wananchi walio wengi maskini wanaendelea kutaabika. Wakipakwa mafuta kwa mgongo wa chupa kupitia vyombo vya habari.

Mwananchi mwenye njaa, anachohitaji ni chakula tu na si wingi wa maneno, nyaraka wala hotuba. Mgonjwa hospitalini anachohitaji ni huduma ili apone na si maneno wala pole za huzuni. Maana maneno hayatendi!

Inawezekana kumsaidia mgonjwa bila kuongea maneno mengi. Mtu mwenye njaa ukimpa chakula bila kusema neno hatashiba? Na kwa utamaduni wetu Waafrika, anayepatiwa huduma ndiye anastahili kutoa shukrani.

Lakini kwa sasa jamii, wakiwemo baadhi ya viongozi hawawezi kutoa huduma bila kuwepo vyombo vya habari au bila kuonekana kwamba wametoa huduma.

Wanachofanya hapa ni kwa manufaa ya nani? Vivyo hivyo, wakifanya ovyo, vyombo hivyo hivyo vya habari vinaonyesha udhaifu huo. Kama tunavyoendelea kuona.

Imenishangaza pia, siku za hivi karibuni. Masuala nyeti yanayogusa masilahi ya nchi mara nyingi yanachimbuliwa na wabunge wa upinzani.

Mfano mzuri ni hili sakata la ufisadi na hoja ya Buzwagi lilikoanzia na linaloendelea. Wanaopiga kelele ni wabunge wa upinzani na viongozi wao. Kwanini?

Hili linaleta maswali mengi yasiyo na majibu. Je, inawezekana wabunge wa upinzani wana uchungu na nchi hii kuliko wale wa chama tawala? Au wana agenda ya siri tusiyoijua?

Au kwa sababu wako nje ya uwanja hivyo wanauona vizuri mpira kuliko wachezaji waliomo ndani?

Lakini historia na uzoefu unaonyesha, kuna wabunge wa sifa hizi waliokuwa machachari pindi wako upinzani lakini baada ya kurudi chama tawala sasa hawasikiki. Je, kuna nini kilicho nyuma ya ukimya wao?

Nilivunjwa moyo na majibu dhaifu ya maswali nyeti ya wabunge kwa Waziri wa Miundombinu. Sijui kama ni mimi tu lakini pia wabunge wengi walivunjwa moyo, ndiyo maana wengine wakapendekeza muda uongezwe ili wapatiwe majibu mazuri.

Wengine walifikia hata kutishia kufanya kampeni hasi dhidi ya kiongozi huyo. Je, kama wabunge hawakuridhishwa inakuwaje wananchi wenyewe wanaozionja shida hizo warithike? Siamini kama wangekuwa wanajua wangerithika na majibu hayo.

Inawezekana wingi wa maneno bila vitendo ni miongoni mwa virusi vinavyo itafuna nchi hii. Na machungu ya dhiki na shida za wanyonge walio wengi haziwahusu viongozi hao wanaopigia siasa hata masuala ya muhimu.

Kama unakula na kushiba, unalala pazuri, unatembelea gari la kifahari, tena unapata mafuta bure, utaguswa kweli na shida za wananchi walio vijijini au maporini huko? Inawezekana aliyeshiba kumjua mwenye njaa? Ni wachache na wateule.

Lakini utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo unategemea fedha ambazo wananchi hao hao ndio waliolipa kodi.

Pamoja na kuwa wanalipa kodi na wao kuwa ndio tabaka la wazalishaji, bado dhiki na shida zinawaandama kweli kweli.

Tabaka dogo lisilozalisha ndilo linalofaidika na mapato yanayozalishwa na wanyonge pamoja na rasilimali za wanyonge hawa wengi.

Jaribu kufikiri. Nani ana kazi kubwa kati ya mkuu wa wilaya na daktari wa wilaya mwenye dhamana ya kuokoa maisha ya watu kwa kufanya upasuaji bila kuchoka hadi usiku wa manane?

Lakini uliza mshahara wa daktari, huzuni tupu! Tutayaota maendeleo hadi lini pamoja na wingi wa rasilimali zetu?

0773 - 960606.

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.