Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Menejimenti na na uongozi katika vijiji, mitaa
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Menejimenti na na uongozi katika vijiji, mitaa
By Marshy Abdu | Published  10/1/2007

WATANZANIA sote tunaishi kwenye vijiji na kwenye mitaa. Hivyo uongozi wa vijiji na mitaa ni muhimu kwa kila Mtanzania. Kama tujuavyo maofisa watendaji wa vijiji na mitaa ndiyo wasimamizi na waendeshaji wakuu wa shughuli za serikali za mitaa katika ngazi ya kijiji na mtaa, hivyo ni vema kwao kuelewa dhana ya misingi ya menejimenti ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Lakini pia kwa vile Watanzania wote wanaishi vijijini na kwenye mitaa ni bora dhana hii ya menejimenti na uongozi ikaeleweka kwa wote.

Katika makala hii nitajadili mbinu za menejimenti na uongozi katika ngazi ya vijiji na mitaa. Zimetolewa tafsiri mbali mbali za maana ya menejimenti. Mfano, E.F.L Breach, katika kitabu cha ‘Misingi ya Menejimenti’ (Principles of Management) anaeleza kwamba menejimenti ni uwajibikaji katika usimamizi katika ofisi au kiwanda ili kufikia malengo fulani.

Naye Dynier katika kitabu chake kinachohusu ‘Utawala wa Ofisi’ (Office Administration) anaelezea kwamba menejimenti ni utaratibu wa utendaji kazi katika ofisi au kiwanda ili kufikia malengo fulani.

Tukizingatia tafsiri zote mbili zina uwiano kwa kiasi kikubwa, hivyo menejimenti ni utaratibu wa upangaji wa matumizi ya rasilimali zilizopo (watu, fedha, mitambo, majengo, ardhi, muda na kadhalika) utendaji kazi, usimamizi na uratibu wake ikiwa ni pamoja na uwajibikaji katika sehemu za kazi katika kufikia malengo au matarajio yaliyowekwa.

Utaratibu huu hujibu maswali kama:- Nini kitafanyika, lini na ni matokeo gani yanatarajiwa? Nani watafanya, watafanyia wapi na watafanya namna gani? Watatumia zana, vifaa, malighafi au fedha kiasi gani na zitatoka wapi? Usimamizi utafanyikaje na uwajibikaji na uratibu wa shughuli utakuwajie? Kila shughuli muhimu itachukua muda gani, na je, shughuli nzima itachukua muda gani kukamilika?
Hivyo misingi ya menejimenti imegawanywa katika maeneo ya kupanga, kuratibu watumishi, kuongoza na kudhibiti.

Upangaji wa shughuli zitakazofanyika ni muhimu ili kufikia malengo kikamilifu. Hivyo ofisa mtendaji wa kijiji au mtaa lazima aweke mpango mzuri wa kutenda shughuli zake ili malengo yafikiwe. Na ni muhimu kuwa na watumishi wenye ujuzi ili kazi zifanywe ka ufanisi. Ofisa mtendaji wa kijiji au mtaa si mwajiri, ni msimamizi tu wa utendaji wa watumishi katika eneo lake ili wote wafanye kazi kama timu moja.

Vivyo hivyo, watendaji hawa inabidi waratibu utendaji kazi wa wananchi ili wafanye kazi za kujenga taifa kwa ukamilifu. Ofisa mtendaji wa kijiji/mtaa, kama kiungo cha idara zote za halmashauri, anatakiwa kuzielewa barabara sifa za kiongozi bora na kuzihusisha na shughuli zake za kila siku ipasavyo. Uongozi ni mahusiano kati ya viongozi wa ngazi ya juu na wale wanaoongozwa. Wenye kuongozwa ni vema wapate kiongozi mzuri mwenye uwezo atakayehakikisha malengo ya ofisi/kiwanda yanafikiwa. Kwa hiyo, ofisa mtendaji wa kijiji/mtaa ni lazima awe ni mtu mwenye uwezo wa kuongoza ili malengo ya halmashauri, kata, kijiji na mtaa yafikiwe.

Pia ikumbukwe kwamba udhibiti ni muhimu katika utendaji kazi kwani unasaidia kuona kama kila mtumishi/mfanyakazi ametekeleza majukumu yake ipasavyo. Udhibiti unasaidia kufikia malengo yaliyowekwa. Mtendaji wa kijiji/mtaa anatakiwa adhibiti watumishi walio katika eneo lake ili kuona kama kila mmoja anatekeleza wajibu wake ipasavyo.

Mtendaji wa kijiji/mtaa, anayeifahamu kazi yake vizuri ni lazima awe na tabia ya kujiwekea utaratibu wa kutenda mambo, na baadaye kwa matumizi bora ya rasilimali zilizopo na kwa njia hii anaweza kupata ufanisi mkubwa zaidi.

Pia mtendaji bora wa kijiji/mtaa ni lazima awe na upeo wa kuunda vikundi na kuvikabidhi wajibu na majukumu ya kutekeleza malengo fulani. Faida ya mbinu hii ni kwamba mtendaji si lazima afanye kila kitu mwenyewe, bali anaweza kuwatumia watu alio nao. Baada ya kuunda vikundi vya kazi lazima kuweka uongozi wenye uwezo na wajibu wa shughulli hizo ili watoe usimamizi wa karibu. Vile vile, shughuli za usimamizi zinaweza kufanywa kwa kutumia uandishi wa taarifa za utekelezaji kwa vipindi maalum. Taratibu za usimamizi zinawajibisha watekelezaji.

Mipango, ratiba, makisio na taarifa mbalimbali ni mbinu za menejimenti katika kudhibiti shughuli za kiongozi. Njia hizi za udhibiti zinawezesha kupima utekelezaji na kulinganisha na malengo yaliyokusudiwa na kusaidia kueleza sababu za kushindwa kufikia malengo.

Mtendaji bora wa kijiji/mtaa ni lazima awasiliane na anaowaongoza kuhusu mambo yaliyokusudiwa kufanyika na pia lazima apate taarifa za utekelezaji. Mbinu ya mawasiliano inaweza kutumika kuwahamasisha wanaoongozwa kwa kutumia maelekezo ya mdomo au maandishi. Mtendaji anapaswa kuelewa kinachotendeka wakati wote na kuwafanya anaowaongoza waelewe kwamba anaelewa wanachofanya. Mawasiliano ni kigezo cha msingi katika kufanikisha malengo yote ya serikali.

Mtendaji bora wa kijiji/mtaa ni yule anayezingatia ushirikishwaji. Hii ni zana na mbinu ya msingi sana katika kufanikisha majukumu ya umma. Ushirikishwaji zaidi ya kutegemea kanuni na sheria rasmi hutegemea pia mwenendo wa kiongozi anayehusika. Ni muhimu pia wanawake washirikishwe kikamilifu katika uongozi – hii ni kwa sababu idadi yao ni kubwa na ndiyo wazalishaji wakubwa. Mbinu za kuwashirikisha ni pamoja na kuwahamasisha wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kuwapa majukumu, changamoto na misaada.

Ikumbukwe kwamba kuongoza ni kuonyesha njia, kutanguliza na kuelekeza katika utekelezaji wa majukumu ya umma. Kuongoza ni kujenga moyo wa pamoja miongoni mwa wanaoongozwa na kuwahamasisha ili watekeleze yale yaliyokusudiwa. Ili kiongozi aongoze, lazima apate wafuasi ambao wanamkubali na kumfuata. Hivyo, ni jukumu la kiongozi kujenga mazingira mazuri mahali pake ili kuhakikisha kuwa anakubalika.

Kuna aina mbali mbali za uongozi: Kuna uongozi wa kiimla, hii ni aina ya uongozi ambao mkubwa hutoa amri na kutekelezwa na anaowaoongoza bila ya wao kutoka kauli yeyote. Aina nyingine ya uongozi ni uongozi huria, aina hii hutoa madaraka makubwa kwa wanaoongozwa kufanya kila watakacho bila ya maelekezo yoyote kutoka kwa viongozi. Lakini sisi hapa uongozi tunaofuata ambao maofisa watendaji wa vijiji na mitaa wanalazimika kufuata ni uongozi wa kidemokrasia.

Uongozi huu umezingatia kwamba wanaoongozwa wanao uwezo wa kujiamulia mambo yanayowahusu. Kwa hiyo, kiongozi huwashirikisha na kuwashawishi wanaoongozwa wachangie kwa mawazo na vitendo mambo ya kufanya. Pale ambapo hawajaelewa, kiongozi huwaelimisha na kuwashauri mpaka watakapokubali.

Uongozi wa kidemokrasi tofauti na ule wa kiimla, unalaumiwa kwa kufanya mambo polepole na unachelewesha maamuzi. Uongozi huu una faida kwamba watu wakishakubaliana na jambo linalohusika wanalitekeleza hata wakati msimamizi hayupo maana tabia ya kulitekeleza imekuwa ndani ya mioyo yao.

Hivyo ili kupata ufanisi wa hali ya juu katika mfumo wa serikali za mitaa ni muhimu maofisa watendaji wa vijiji na mitaa kuzingatia na kufuata mbinu za menejimenti na uongozi, kwani wao ndiyo wasimamizi na watekelezaji wakuu wa shughuli za serikali za mitaa katika ngazi ya kijiji na mtaa.

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.