Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Tanzania bila Kikwete, Warioba inawezekana
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Tanzania bila Kikwete, Warioba inawezekana
By Marshy Abdu | Published  10/1/2007

“TUNAWANYONGA vibaka na kuwachagua wezi wakubwa kuwa viongozi wa umma.” Kauli hii ilitolewa na mtumwa wa Kigiriki, Aesop, aliyeishi kati ya miaka 620 na 560 Kabla ya Kristo.

Aesop alifariki dunia miaka ipatayo 2,500 kabla ya Jaji Joseph Sinde Warioba, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania.

Mtumwa huyu wa Kigiriki ana ujumbe mzito kwa Watanzania wa leo. Kwangu mimi, ujumbe huu ni mzito kuliko kauli ya Jaji Warioba wiki hii katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Labda inaonekana ajabu kumlinganisha mtumwa na waziri mkuu mstaafu! Lakini hekima haina cheo. Mang’amuzi ya maisha yametudhihirishia kwamba wakati mwingine watu wasio na madaraka wana hekima kuliko hao wanaotawala.

Kosa tunalofanya, mara nyingi, ni kudhani kwamba mtu akipewa uongozi anapewa na hekima.

Hekima kuendana na uongozi imetokea mara chache maishani; na baadhi ya viongozi waliokuwa na hekima hawakuipatia madarakani. Walikuwa nayo awali, na mahali pengine, ndiyo iliyowashawishi watu kuwapa nafasi hizo za uongozi.

Tanzania imeshasahau enzi hizi, si katika uongozi wenye hekima tu bali pia uongozi unaozingatia uadilifu. Waadilifu tuliokuwa nao wamekufa, wengine wanaendelea kufa; hata waliobaki, tuliokuwa tunawategemea, wameanza kutukatisha tamaa.

Kwa nini nimemkumbuka Aesop? Nimesoma alichosema Jaji Warioba akiwalaumu wananchi wanaotoa shutuma na tuhuma kwa viongozi, wasaidizi wao na wastaafu. Vyombo vya habari vimemnukuu Warioba akisema:

“Unapomtaja rais kama fisadi unakuwa na unataka kufanya wananchi wakose imani na serikali yao, suala ambalo ni hatari, wananchi watakimbilia wapi kama wanayetaka kumkimbilia naye anachafuliwa?... Mengine yanashitusha. Umoja wa nchi hii unaweza kufika mahali pabaya. Yaani rais anaitwa fisadi kwa sababu hizi na zile tu.

Huyu ni mwanadamu kama wengine, lakini ndiyo symbol (alama) ya taifa, ukishamwita fisadi, na unakwenda unazungumza hivyo, hakuna uongozi wa taifa.

Hata Mkapa aliyemtangulia anaitwa fisadi, hivi hivi tu, habari hizi zinaleta picha gani? Kwamba alijitajirisha yeye na ndugu zake katika miaka yake 10. Mkapa kama binadamu alikuwa na weakness zake, lakini kwa nchi hii huwezi kufuta historia yake.

Watu wameacha kushughulikia matatizo ya wananchi, mambo ya msingi ya wananchi. Kwa mfano, mwaka jana, tumepata tatizo la chakula na umeme, lakini badala ya kuzungumzia jinsi ya kulikabili mwaka huu, watu wako busy kuzungumzia mambo ya uongozi. Wanazungumzia nani fisadi, kutueleza mambo yao ya uongozi. Vipaumbele vyetu vinaanza kupotoshwa. Maendeleo hayawezi kuletwa na viongozi na serikali.

Yataletwa na wananchi, serikali inatunga sera tu na kuzisimamia.”
Hii ni hekima mpya ya mzee Warioba. Ni wosia anaowapa Watanzania. Nimemsoma Warioba nikamkumbuka mlezi wake kisiasa, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Nikaona jinsi baadhi ya wanafunzi wake wanavyosahau mafundisho yake kwa kasi kubwa, na wanavyobadilika badilika kila kukicha na kupuuza misingi aliyowaachia. Walisema wangemuenzi. Nasi tunashuhudia jinsi wanavyomuenzi kwa kejeli.

Huyu si Warioba tunayemjua. Warioba ni mtu ambaye alistahili kupelekewa rufaa zote za rushwa nchini. Si mtu wa kusimuliwa jinsi rushwa inavyotafuna nchi yetu. Si mtu wa kuelezwa kuwa wala rushwa wakubwa ni wale wenye nafasi kubwa katika uongozi wa jamii.

Si mtu asiyefahamu jinsi vita ya rushwa imetushinda kwa sababu serikali inashughulika na rushwa ndogo na kuziacha kubwa kubwa zikitamalaki. Warioba si mtu wa kusema vita dhidi ya rushwa si kipaumbele cha kitaifa. Huyu huyu ndiye amekuwa analalamika mara kwa mara kuhusu kukithiri kwa rushwa nchini. Lipi limemsibu?

Au anataka kutueleza kwamba amezeeka kiasi hicho? Ameanza kupoteza kumbukumbu? Au anaanza kupakaribia pale ambapo Mwalimu Nyerere alipakataa aliposema anang’atuka akiwa bado na ‘akili nzuri?’
Sioni mantiki katika kauli ya kiongozi mstaafu, mwanasheria aliyebobea, mtu anayeheshimika kimataifa kudai kwamba mjadala juu ya ufisadi na uongozi si kipaumbele cha taifa!
Hizo huduma anazojadili, matatizo ya umeme anayozungumzia na mengine, yamegubikwa na rushwa ya wakubwa. Anatuambia tunyamazie hili, tuzungumzie utabiri wa hali ya hewa!
Warioba amepata ufunuo mpya. Sasa anadhani kwamba viongozi hawawezi kuwa mafisadi. Anataka kutuambia kwamba hata tunapopata shaka juu ya uadilifu wa kiongozi, tunyamaze ili wananchi wasikose imani na kiongozi huyo.

Nani amemwambia kwamba ufisadi wa viongozi ni nyenzo ya kudumisha imani na amani ya wananchi? Mbona anajua mifano ya viongozi wengi, ndani na nje ya Afrika waliojitumbukiza katika ufisadi kwa kutumia nyadhifa zao? Kwa nini anadhani kwamba hilo haliwezekani Tanzania?

Warioba anakumbuka hotuba ya Mwalimu Nyerere katika mkutano wake na waandishi wa habari Hoteli ya Kilimanjaro mwaka 1995 kuhusu sifa za rais anayefaa?

Hivi Mwalimu alitoa wapi wasiwasi wake hadi akaanza kuzungumzia ‘utakatifu wa Ikulu?’
Mbona Warioba hakuamsha kidole kumpinga Mwalimu Nyerere aliposema ‘kanchi kananuka rushwa?’ Alidhani ni rushwa ya makarani wa mahakama?

Hivi Warioba na Kingunge Ngombale-Mwiru wanaanza kuwa na uwezo sawa wa kufikiri na kujadili masuala ya kitaifa - kwa kuchezea akili za Watanzania? Mwalimu Nyerere ameshafariki, lakini tunu zimebaki. Hivi hata baada ya kusoma kitabu cha Mwalimu Nyerere: ‘Uongozi wetu na hatima ya Tanzania,’ bado anataka tuamini kwamba uongozi wa nchi si kipaumbele chetu?

Nyerere huyo huyo ndiye alisema ili tuendelee tunahitaji mambo manne. Ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Kinachojadiliwa hapa ni suala la uongozi bora. Warioba anasema si jambo la msingi kujadili uongozi unaohusishwa na ufisadi?

Anataka kutuaminisha kwamba umaskini wa Watanzania hauchangiwi kwa kiasi kikubwa na uongozi mbovu unaokumbatia ufisadi? Na hao wanaharakati wenye maisha bora anaowazungumzia, wanaishi maisha bora kuliko yake yeye? Tumwamini yeye tuwapuuze wao?

Watanzania wangetarajia Warioba awashauri watuhumiwa wajisafishe na wajiuzulu ili haki itendeke. Huu ndio uadilifu tunaoutarajia. Yeye na wenzake hao, walipaswa kujifunza katika tukio jingine la wiki hii lililotokea mkoani Kilimanjaro.

Mwinjilisti wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini alituhumiwa kumbaka mwanafunzi wa kidato cha tatu na kumsababishia ujauzito. Hata kabla hajafikishwa mahakamani, uongozi wa kanisa lake umetoa tamko kwamba mwinjilisti huyo amesimamishwa kazi hadi hapo tuhuma dhidi yake zitakapofikia tamati.

Huyu ametuhumiwa tu. Hajahukumiwa. Watumishi wetu (viongozi) wanaotuhumiwa kwa ufisadi wanasema eti hawawezi kujiuzulu kwa sababu ya kutuhumiwa tu! Wanataka wakae ofisini mwetu wabadili mafaili na kuharibu kumbukumbu huku wanatafuta namna ya kutumia mamlaka yao kuathiri mwenendo wa upatikanaji wa haki!
Hata bosi wao, hajawachukulia hatua. Wanakwenda mahakamani kupataje haki wakiwa madarakani?

Kama hawako pale kwa masilahi binafsi, kipi kinawazuia kujisafisha kwa kuachia ngazi? Kama Mwalimu Nyerere alivyowahi kuhoji na kutoa mfano wa mke wa mfalme, hata kama si kweli, ‘kwa nini mke wa mfalme atuhumiwe?’ Kwanini watuhumiwe wao si wengine? Wataturidhishaje kwamba ni waadilifu kama hawataki kukaa pembeni? Au wanadhani wakiondoka ofisini nchi inabomoka?

Warioba anasema: “Sikutumwa na mtu, simo katika siasa wala serikali, mimi ni mtu huru, hakuna mtu aliyenituma, nasema ninachokiamini.”
Napenda kuamini kwamba hakutumwa na mtu. Laiti angesema kuwa ametumwa. Tungemsamehe kwani tunajua kwamba mjumbe hauawi. Lakini kama hayo ndiyo mawazo yake, basi amejiingiza kwenye kundi jipya.

Na nikiyaunganisha na yale ya Kingunge Ngombale-Mwiru, sasa naanza kuelewa kwanini Nyerere alisema anang’atuka akiwa ‘bado na akili nzuri.’
Hayo mambo ya msingi kwa taifa ni yapi? Tutayafanikishaje? Huko tulikotoka tumekwama wapi?

Hivi bado Warioba anaamini kwamba ‘rushwa ni adui wa haki,’ halafu akiwa mwanasheria na kiongozi mstaafu, haoni uhusiano kati ya vurugu hizi anazoziogopa na haki isiyotendeka katika jamii yetu? Anaamini kwamba amani inawezekana bila haki? Na kama amani itatoweka, ni kwa sababu ya wanaosema ‘tumeibiwa’ au kwa sababu ya wale walioiba?

Warioba anaogopa kuona mtu muhimu kama rais akiguswa na tuhuma. Kwani Rais Jakaya Kikwete ni wa kwanza kuguswa?

Tena afadhali yeye kaguswa na tuhuma za zamani alipokuwa waziri. Mbona Warioba hakung’aka wakati mzee Ali Hassan Mwinyi aliporushiwa makombora?

Tena mengine yalirushwa na Mwalimu Nyerere akiwa amesimama mita 200 tu kutoka mlango wa ofisi ya rais! Mbona Warioba alikaa kimya?

Hivi Warioba anadhani kwamba Watanzania wa leo ndio wale aliokuwa anawatawala akiwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais? Anadhani wananchi wa leo wanapima ukweli kwa kutazama cheo cha aliyeutoa? Au anadhani hawana mamlaka ya kutoa ‘hukumu’ kwa uongozi ulioshindwa?

Bado anadhani wananchi wa sasa wanaweza kufugwa na kuchezewa akili, kwa kisingizio cha ‘amani na utulivu?’ Anadhani hawajui umuhimu wa nafasi ya rais kama nembo ya taifa na alama ya umoja wa kitaifa?

Na anadhani hawajui kwamba rais ni mtumishi wao na hapaswi kujizungushia watu wenye uadilifu wa mashaka au yeye mwenyewe kujihusisha katika mambo yatakayomletea kashfa kama hizi?

Watanzania wanajua. Lakini hawalazimiki kuumia kwa sababu ya kujua kwao. Wananchi wanataka viongozi wawe sehemu ya ufumbuzi wa matatizo ya taifa. Viongozi wakishiriki kusababisha matatizo yetu tutasema.

Wananchi wanajua pia kwamba wao na viongozi wao ni watu wa kupita, lakini taifa litadumu. Wanataka uongozi unaotazama mbele na kuweka misingi ya kudumisha taifa.

Wanajua kwamba viongozi wakijiingiza katika ‘kutafuna nchi’ nao watatatafunwa! Tusiwatishe wananchi kwa kusingizia amani na umoja. Tusiwalazimishe kuwa na imani na viongozi wasiojiaminisha.

Wananchi wanajua umuhimu wa rais, lakini wanajua kuwa maisha yao ni muhimu kuliko maisha ya mtu mmoja anayetukuzwa hata katika makosa. Wanajua kuwa yeye ni binadamu, atapita na taifa litabaki. Wanajua kuwa akishindwa yeye, wapo wengine wataweza.

Warioba asitudanganye wala kututisha kwamba bila rais fulani nchi hii haiendi. Nyerere alipotaka kung’atuka, watu wenye mawazo kama ya Warioba walimwendea kumshawishi aendelee, kwa kisingizio kwamba asingepatikana mwingine wa kuongoza Tanzania. Sasa yuko wapi?

Kwa hiyo, ni vema Warioba ajue kuwa tunatambua uwezo, udhaifu na mipaka ya viongozi wetu.

Ajue kwamba wananchi wanajua kuwa nguvu za rais leo ni sawa na mavazi ya mganga wa jadi. Ukimvua yale manyoya anayovaa kutisha na kutiisha wateja wake unagundua kuwa naye ni mtu wa kawaida kama sisi! Tena wakati mwingine viongozi wetu ni dhaifu kuliko sisi.

Warioba atambue kuwa kama wananchi wana haki ya kutokuwa na imani na Bunge, wana haki pia ya kutokuwa na imani na kiongozi mmoja mmoja – hata rais. Na katiba inawalinda.

Ajue pia hata viongozi wetu wanajua hilo, na ni waoga. Ndiyo maana wanatunga sheria za kuwalinda wakiwa madarakani na wakishastaafu. Hawatungi sheria hizi kulinda usafi wao, bali uchafu wanaoufanya wakiwa madarakani. Wananchi wa Tanzania hawawezi kukubali kufikishwa mahali pa kupiga makofi kushangilia uchafu wa viongozi wao kama Warioba anavyotaka kutulazimisha. Makosa yaliyofanyika katika nchi nyingine yamekuwa somo kwetu.

Warioba ajue kuwa kila mtu huandika historia yake mwenyewe. Wala hakuna anayeweza kuifuta. Hivyo, historia ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa, kwa mfano, imeshaandikwa na inaendelea kuandikwa. Imejaa mengi; mazuri na mabaya. Wanaotaka kuzungumzia mazuri yake waseme. Lakini tusiwazuie wanaotaka kuzungumzia mabaya yake, ambayo tunapaswa kuyatumia kama somo, ili wengine wasianguke katika mtego ule ule.

Hata historia ya Warioba imeshaandikwa na inaandikwa. Na sasa ameongeza ukurasa mpya katika historia yake, kwa tamko hili la wiki hii.

Viongozi wetu ni binadamu. Wana makosa. Mengine ni ya makusudi, mengine ni ya bahati mbaya. Mengine wamesababishiwa, na mengine wameyatafuta wenyewe, tena kwa ushawishi wa hoja na kwa nguvu ya madaraka yao – na kwa tamaa zao. Mengine wanayafanya kwa dharau na jeuri, wakizitegemea sheria zinazolenga kutubana tusiwahoji.

Tukubaliane kwamba udhaifu wao si utetezi wa makosa yao. Hatuwezi kuyaacha makosa yao yaende tu na yawe mfano wa kuigwa.

Tutawakosoa, tutawakemea na kuwatuhumu. Kwa kufanya hivyo, hatuwachafui bali tunasema kwamba wamechafuka; wajisafishe.

Warioba anamwonea Dk. Willibrod Slaa aliyetangaza orodha ya watuhumiwa. Anasema Dk. Slaa anawachafua aliowatuhumu. Hivi Dk. Slaa ndiye alisuka mipango yao ya ulaji ambao anawatuhumu kufanya?

Warioba anathibitishaje kwamba walikuwa safi kabla ya Dk. Slaa kuwataja? Mbona sasa Warioba mwenyewe anadai tuhuma hizi si mpya? Kumbe alikuwa anawajua? Mbona hakuwakemea? Mbona hakuwashauri? Au mbona hakuwasafisha? Kutokuwa jipya kunaondoa makosa yaliyofanyika huko nyuma? Alitarajia ziletwe mpya wakati hizo za zamani hazijashughulikiwa?

Mzee Warioba alipewa jukumu la kuongoza tume ya rushwa miaka 10 iliyopita.

Alitoa mapendekezo kwa serikali, na amekuwa akilalamika kwamba hayatekelezwi. Alipoombwa majina ya waliotuhumiwa kwenye tume yake, akaruka hatua 100.

Woga! Sasa si awaache walio na ujasiri watamke majina waliyo nayo? Si aache mahakama ishughulikie madai yao?

Hata kama yeye ni jaji, kesi hii haijapalekwa kwake. Haruhusiwi kutoa hukumu. Na hata kama anatoa hukumu si ofisini mwake katika mkutano na wanahabari. Kile anachowalaumu kina Dk. Slaa kufanya kwa kuwatuhumu viongozi wenzake hadharani, ndicho anachofanya yeye kuwahukumu kina Dk. Slaa hadharani.

Zaidi ya hayo, Warioba anakwenda mbali. Anakejeli ushahidi wa wanaotoa tuhuma hata kabla haujatolewa. Je, anajuaje kiwango cha ushahidi kilicho mikononi mwa Dk. Willibrod Slaa na wenzake hata kabla hajaenda mahakamani?

Nadhani Warioba anaanza kupitwa na wakati. Wananchi hawawezi kulazimishwa kuwa na ‘imani.’ Imani inapaswa kujengwa na watawala mioyoni mwa wananchi. Rais Kikwete alianza vizuri na alianza pazuri. Mtangulizi wake alimjengea mazingira mazuri ya kuongoza nchi. Yanayompata sasa hivi hayatoki nje ya serikali yake. Hayaletwi na wananchi wake. Yawezekana ni sehemu ya matokeo ya majivuno waliyoingia nayo madarakani.

Wananchi wamempenda kweli; lakini yeye ameanza kuwakataa taratibu. Wamekuwa na matumaini makubwa naye, sasa wanaishia kuonyesha moyo wa kukata tamaa.

Rais wetu hataki kupendeka. Wananchi wameamini kauli zake, hawajaona matendo yake. Wameamini nafsi yake, hawajawaamini wasaidizi na maswahiba wake. Kama watu leo wanamgeuka, basi ni kwa sababu ameshindwa kushikamana nao.

Warioba anawaeleza nini wananchi waliofurahia kauli ya rais kwamba serikali ingepitia mikataba ya madini ili iwe na manufaa, na sasa wanasoma habari za mkataba mpya wa Buzwagi kwamba nao ni yale yale!

Lakini sababu ya pili ya matatizo ya serikali ya Kikwete inatokana na hoja ya pili inayotolewa na Jaji Warioba. Anasema: “Mwaka 2005 niliyasema haya ya kupakana matope, ukianza dhambi hii huwa haiishi, wakati huo wapo waliokuwa wakisema oh huyu Mwarabu! Dhambi hii ndiyo inaendelea sasa.”

Hapa nakubaliana na Warioba. Harakati na kampeni za Kikwete kuingia madarakani zilifanywa kwa kuwaandama na ‘kuwachafua’ vigogo kadhaa ndani ya CCM na serikali. Nilishaandika huko nyuma kwamba miongoni mwao walikuwamo kina Frederick Sumaye, Profesa Mark Mwandosya, John Malecela, Iddi Simba na wengine waliodhaniwa wangeutaka urais.

Baada ya kuwaondoa hao katika mioyo ya wananchi, harakati hizi zilimalizikia kwa akina Benjamin Mkapa na Dk. Salim Ahmed Salim. Mkapa aliguswa ili alegeze kamba, amtupe ‘mtu wake’ akumbatie mtu wao. Walifanikiwa.

Wengi tunajua kuwa Mzee Warioba alikuwa mmoja wa waathirika wa kampeni hizi kwa sababu mtu wake hakupita. Nilimtazama Warioba kwenye luninga siku Kikwete aliposhinda na kutangazwa mgombea wa CCM, Dodoma. Warioba alishindwa kuficha hisia zake. Alinuna na kuchukia waziwazi kwa sababu alijua sababu za mtu wake kushindwa.

Najua itamchukua muda kusahau hili. Ndiyo maana amelizungumzia hata wiki hii. Lakini hilo limepita. Yeye, kama wengine, amekuwa majeruhi wa siasa za kurushiana mabomu. Anajua walioyarusha. Sasa imekuwa zamu yao kurushiwa kutoka upande mwingine.

Kinachowaumiza ni kwamba kwa kuwa wameanza kurushiwa mapema mno. Wanajua pia athari ya mabomu waliyowarushia wenzao kwa miaka kadhaa.

Wanaona mazingira magumu yanayowakabili sasa na huko waendako. Tofauti na zama zao, mabomu ya sasa yanarushwa kutoka nje ya CCM, lakini yana vyanzo ndani ya serikali yao.

Tena mingine yana mizizi mirefu. Wanaogopa kwamba mizizi hii ikiendelea kuchimbwa, mwishowe ukweli waliouficha kwa muda mrefu utagundulika. Kwa hiyo, kinacholindwa na kauli za kina Warioba si uhai wa Watanzania; si amani ya taifa, bali ya viongozi wa sasa na waliostaafu.

Kama Warioba angekuwa na busara ya uzeeni, asingewashutumu wanaorusha mabomu haya, kwa sababu tayari ameshakiri kwamba wanaorushiwa mabomu walitengeneza njia hiyo wao wenyewe.

Angepaswa kuyatarajia hayo. La msingi, awashauri hao anaowatetea wajisafishe. Na kuna tofauti kati ya kujitetea na kujisafisha. Kujisafisha ni kuishi na kutenda kwa uadilifu na uangalifu katika nafasi walizo nazo. Wakati mwingine, ni vema kukubali ukweli, kuomba radhi, kurekebisha mambo na kusonga mbele.

Lakini kama hawezi kuwashauri wanaotuhumiwa, akae kimya ashuhudie mabadiliko ya kifikra.

Ajue kuwa mbinu za kisiasa zimebadilika. Atambue kuwa umma umeamka. Ajue kuwa sasa harakati na ulinzi wa rasilimali zimepamba moto. Na Watanzania wa leo wanajua fika kwamba Tanzania yenye neema inawezekana bila Mkapa, Warioba wala Kikwete.

ansbertn@yahoo.com +447828696142 www.ngurumo.blogspot.com

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.