JUMUIYA ya wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini wameonya kwamba iwapo serikali haitakuwa tayari kufanya majadiliano ya wazi kuhusu tuhuma zinazowaandama baadhi ya watendaji wake, hawatasita kuwaunga mkono wanaharakati na wanasiasa wa vyama vya upinzani katika madai yao.
Walitoa tamko hilo jana, baada ya kufunga lango kuu la kuingia Chuo Kikuu cha Ardhi (zamani Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi), Dar es Salaam wakishinikiza kuruhusiwa kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, kuruhusiwa kuingia chuoni hapo kushiriki mdahalo wa nafasi ya mwanafunzi wa elimu ya juu katika jamii.
Walisema wamefuatilia kwa kina tuhuma za ufisadi zinazotolewa sasa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa na wanaharakati dhidi ya viongozi kadhaa wa serikali na kwamba wameona kuna haja ya kutoa mchango wao kama wasomi wanaotegemewa na jamii ya Watanzania katika maendeleo ya taifa.
“Taifa sasa liko katika malumbano makali na mabaya yanayowahusisha viongozi wetu ambao wamepewa dhamana ya uongozi, lakini wanadaiwa kujinufaisha wao na familia zao kwa nyadhifa hizo tulizowapa.
“Madai yanayotolewa ni makubwa na kwa msomi yeyote, lazima ukisikia tuhuma hizi utazifuatilia tu, kwa sababu zinahusu uhai wa taifa letu, sasa tumeamua kuanza kukutana na hawa viongozi wetu, wanaotuhumu na wanaotuhumiwa, tuzungumze nao katika midahalo, wametuambie kuhusu mambo haya na sisi tuwahoji, wanao wajibu wa kutujibu, kwa sababu mchango wetu ni muhimu kwa maendeleo ya taifa hili,” alisema Makune Cosmas, mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).
Hata hivyo mjadala uliokuwa umeandaliwa na Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) kwa kushirikiana na Umoja wa Wanafunzi Wanaosoma Sayansi ya Siasa na Utawala (DUPSA) jana, ulishindwa kufanyika baada ya uongozi wa chuo hicho kumpiga marufuku kuingia chuoni hapo, mtoa mada katika mdahalo huo, Kabwe Zitto.
Tangazo la kupigwa marufuku Zitto lilitolewa na Mratibu wa Mahusiano wa (TSNP), Dady Igogo, akieleza kuwa Zitto amezuiliwa kuingia katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa sababu uongozi huo ulikuwa unahisi kuwa anaweza kuwashawishi wasomi hao kuiasi serikali.
Igogo alisema kabla ya kumwalika Zitto kuhudhuria mdahalo huo, taratibu zote kwa ajili ya kufanya mjadala huo zilifuatwa, ikiwa ni kuandika barua kwa uongozi wa chuo, kuhusu kufanyika kwa mdahalo na kupewa ruhusa ya kufanya mkutano katika Ukumbi maarufu wa Nkrumah, uliopo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, sehemu ya Mlimani.
Alisema walipewa kibali cha kutumia ukumbi huo Septemba 25, jioni na walianza kubandika matangazo ya kuwepo kwa mdahalo katika eneo la UDSM.
Alisema Sept 26, waliarifiwa kubadili ukumbi wa kufanyia mdahalo huo na wakitakiwa kujiandaa kwa ajili ya kukutana katika Ukumbi wa Theatre One.
Kwa mujibu wa Igogo, Septemba 28 uongozi wa wanafunzi uliitwa tena na uongozi wa chuo na kuelezwa kuwa kama Zitto atafika katika mjadala huo hatatakiwi kuzungumzia mambo ya siasa, na juzi asubuhi, ilitolewa amri nyingine kuwa wanafunzi hawaruhusu kutumia ukumbi huo, kwa sababu ukumbi wa jirani unatumiwa na mabalozi, na kwamba walitakiwa kuacha kufanya mjadala huo.
Mratibu wa haki za wanafunzi (TSNP), Fute Imani, alisema kufutwa kwa mdahalo huo katika hatua za mwisho, ni usumbufu kwa washiriki ambao walialikwa kutoka vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini.
Taarifa ya DUPSA imeeleza kwamba, nia ya wanafunzi, wanajamii ya vyuo vikuu si kuvunja sheria na taratibu za chuo, lakini uongozi wa chuo umekuwa ukiwalazimisha kufanya hivyo.
Baada ya Zitto kuzuiliwa kuingia chuoni hapo, wanafunzi waliokuwa wamefurika katika Ukumbi wa Theatre One waliandamana hadi lango kuu la kuingia chuoni karibu na Chuo Kikuu cha Ardhi, ambako alikuwa amezuiliwa, na kukuta tayari amekwisha arifiwa kuondoka.
Wanafunzi hao waliwatimua walinzi wa geti hilo na kushika doria wao wenyewe, huku wakizuia magari na pikipiki kupita katika eneo hilo, isipokuwa watembea kwa miguu na waendesha baiskeli.
Mmoja wa wanafunzi waliokuwa wakilinda doria getini hapo, Gastor Florence, wa mwaka wa tatu, UDSM, alilieleza gazeti hili kuwa walikuwa wamejiandaa kumhoji Zitto dhidi ya tuhuma zinazotolewa na viongozi wa kambi ya upinzani ili wazipime na kujadiliana naye mambo mbalimbali yanayohusu ustawi wa taifa.
Alisema baada ya Zitto, walipanga kuendelea kukutana na viongozi wengine wanaohusishwa katika kashfa ya ufisadi ili kuwahoji na kujadiliana nao kama Zitto, lengo likiwa kupata ukweli kuhusu tuhuma hizo.
Florence alisema jumuiya ya wanafunzi imeshangazwa na hatua ya chuo kuonyesha udhaifu mkubwa kwa kumuogopa Zitto kuwa anaweza kuamsha ari ya kimapinduzi kwa wanafunzi iwapo angekutana nao na kujadiliana nao.
Waliapa kuendelea kulifunga geti hilo hadi hapo Zitto atakaporuhusiwa kuingia chuoni hapo na kujadiliana nao.
Hata hivyo walitawanyika baada ya askakri polisi wenye silaha kuwasili katika eneo hilo na kuanza kufanya doria huku wakiruhusu msururu wa magari uliokuwa umezuiliwa kupita katika geti hilo.
Ofisa Uhusiano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Julius Saule, alisema kuwa uongozi wa chuo uliamua kuzuia mdahalo huo baada ya kubaini kuwa Zitto atahudhuria.
Alisema wakati kibali kinatolewa, barua ya kuomba kufanyika kwa mdahalo haikuonyesha ni nani atakayezungumza katika mdahalo huo. Alisema sababu nyingine ya kuzuiwa kwa mdahalo huo ni kujaa kwa kumbi zote, na wanafunzi walitaarifiwa kuwa wanapaswa kuahirisha mdahalo wao au kuusogeza mbele.