KARIBU msomaji, mpenzi wa muziki na shabiki wa historia ya mitindo mbalimbali ya muziki duniani.
Hii ni makala mahsusi inayokuchambulia kwa kina na kukujuza yale usiyoyafahamu kuhusu ilikotokea mitindo hiyo ya muziki, jinsi gani ilijiunda na kwa nini inaitwa majina iliyo nayo.
Utapata fursa ya kujua pia ni kwanini uchezaji wa mitindo hiyo uko kama ulivyo, kwanini pia mashabiki na wanamuziki wa mtindo husika huvaa katika namna wanayovaa, kuongea au hata kutembea.
Yote hayo yanatokana na sababu mbalimbali za kihistoria ambazo zinasababisha kuwepo kwa sifa hizo katika mitindo ya muziki.
Basi baada ya kumalizana na mambo ya ‘dancehall reggae’ wiki iliyopita, leo tunaanza mambo mengine mapya kabisa, haya ni mambo yanayopatikana kwenye mipini ya muziki wa dansi, zamani yakifahamika kwa majina mengi maarufu kama ‘chemka, sungura mtie moto’ nakadhalika.
Nazungumzia kile kipande cha pili cha mirindimo ya muziki wa dansi ambapo wimbo hupamba moto, gitaa la solo hukung’utwa kwa makali na ‘marepa’ huhanikiza kwa chozochozo zao huku wanenguaji wakifanya vitu vyao na mashabiki wakipagawa, ni mambo ya sebene.
Tena msomaji, kwa sasa kuna zile nyimbo mahsusi za ala tupu, yaani ‘ma-sebene’ matupu bila uimbaji, ni marepa tu ndio hunogesha vionjo kwenye masebene haya ambayo huwa ni mahsusi kwa ‘show’ au ‘pasha moto’ kabla ya ‘ka-dance’ lenyewe halisi halijaanza kuporomoshwa.
Huko ndiko tunakojikita kuanzia leo kwa safari ya uchambuzi hadi pale tutakapomaliza mambo haya ambayo wengi hudhania kimakosa, kuwa ni ya juzi juzi tu kumbe msingi wake ulianzia siku nyingi sana kihistoria kwenye miaka ya 1950.
Usistaajabu msomaji, ungana nami tuianze safari hiyo ya uchambuzi wa kihistoria na kufahamu ilikotokea hiyo sebene.
Leo msomaji nakuweka sawa kwa kukupa dibaji na mwelekeo wa mwendo wetu utakavyokuwa, ili tutakapoanza kutiririka kwenye safari yetu tuwe sambamba pamoja bila kupotezana.
Awali ya yote nikuambie kwamba katika kuchambua hayo masebene ni lazima tutajivinjari kwa kina sana kwenye historia ya muziki wa dansi, japo si kwa ujumla wake. Si kwa ujumla wake kwa kuwa hapo awali tulishauchambua mtindo huo kwa ujumla wa historia yake.
Tulitiririka kwenye uchambuzi wa kina wenye jumla ya vituo kumi na tuliona mambo mengi sana yanayohusu mtindo huo wa muziki.
Ni siku nyingi kidogo zimepita tangu tulipouchambua mtindo huo, kwa hiyo kurudia kuigusa kwa uchache historia ya muziki huo, kutakupa fursa wewe ambaye hukuisoma kuifahamu vyema.
Lakini pia kama uliisoma historia hiyo, utapata fursa ya kujikumbusha na kuunganisha vyema uelewa wako kuhusu mabadiliko ya kiteknolojia yaliyosababisha kupatikana kwa ‘sebene’ iliyo katika hali ya sasa.
Mtiririko wetu wa uchambuzi utakuwa katika mwenendo ufuatao: kwanza ni vyema ukafahamu kuwa mtindo wa muziki wa dansi ni mchanganyiko wa mirindimo uliotokea kwa muda mrefu sana kutoka pande mbalimbali za dunia zikiwemo Marekani ya kaskazini na kusini, Afrika ya kaskazini, Afrika ya kati, mashariki na kusini.
Pamoja na hayo, muziki wa dansi ulioko nchi hivi sasa wenye hayo masebene ni awamu kama ya nne hivi tangu muziki huo uanze rasmi hapa kwetu.
Tunaposema awamu ya nne, tunaanzia kwenye miaka ya nyuma sana ambapo teknolojia ilikuwa duni hadi kufikia hivi sasa ambapo kuna maendelea makubwa sana ya teknolojia. Unapozungumzia teknolojia, naomba nikufahamishe kuwa, hiyo imehusika kwa sehemu kubwa sana kusababisha kuwepo kwa sebene hivi sasa.
Ugunduzi wa zana mpya umesababisha mabadiliko ya kimsingi ya mapigo ya muziki huu wa dansi wenye kubeba sebene. Msomaji, nikutaarifu pia kuwa kile chombo kinachochukua sehemu kubwa ya kuongoza sebene, yaani ‘drums’ hakikuwepo hapo awali wakati muziki huu ulipoanza. Kazi yake ya kuongoza kasi ya wimbo na kutoa ishara ya kuruhusu vyombo kutamba kwa kupishana nafasi ilifanywa na ngoma nyingine za aina ya tumba.
Tumba ni ngoma mbili zilizosimama wima zinazopigwa kwa viganja vya mikono huku mpigaji naye akiwa amesimama wima, wakati ‘drums’ ni ngoma zinazopigwa kwa vijiti viwili. Mpigaji wa ngoma hizi hukaa chini akiwa amezungukwa na jumla ya ngoma nne hadi tano, kutegemena na aina ya seti anayotumia.
Ngoma moja kubwa anaipiga kwa mguu, hii ndio hasa hutunza mwendo ‘Tempo’ wa wimbo, huzungukwa pia na visahani vikubwa viwili au vitatu ‘Cymbals’ au ‘Crash riders’ pamoja na kisahani cha kufunga na kufungua ‘Hi hats’ anachokidhibiti kwa mguu mwingine wa pili.
Mapigo ya ‘drums’ yaliyofahamika zaidi miaka ya nyuma kama ‘kavasha’ ndiyo hayo hayo yaliyopunguzwa kasi, kuwekewa uzito na kuongezewa mapigo ya fimbo ya kuburuza na kugeuka sebene la kisasa.
Muziki wa dansi ni wa pili kwa umri hapa nchini tangu uanze, umepitwa umri na muziki wa taarabu tu ambao ni wa kwanza. Kutokufahamika vyema kwa historia ya muziki wa dansi ndiko kunakosababisha sebene ionekane kama ni kitu cha nyongeza tu.
Lakini ukweli ni kwamba mtindo huu ulipoanza, wanenguaji wanaocheza kama ilivyo kwenye sebene ndio watu wa kwanza kuwepo kwenye muziki huo kabla hata ya wapigaji wa vyombo waliokuja hapo baadaye sana.
Jambo lingine ambalo ningependa ulifahamu katika dibaji yetu ya leo ni kuwa, muziki wa dansi ulikuwa wa ‘uasi’ dhidi ya mirindimo ya kikoloni iliyokuwa ikitamba kwenye vilabu vya starehe ‘social club’ vilivyotumika kuwafanya wazalendo kuwa ‘wazungu koko’ kwa kulishwa kasumba na kuukumbatia uzungu huku wakiutelekeza uafrika wao.
Baada ya kuingia kwa mirindimo ya Kiafrika na wazalendo kuikumbatia na kuibwaga ile ya Kizungu, wakoloni walikasirika sana na kudai kuwa wanamuziki wa ‘kizazi kipya’ wanaharibu starehe yao.
Najua kwa sasa neno kizazi kipya linahusishwa sana na muziki wa kisasa wa vijana ‘Bongo Fleva’ Lakini msomaji, kwa uhakika halisi ‘kizazi kipya’ ni neno lililoanza kutumiwa mara ya kwanza kwenye muziki mnamo miaka ya 1950.
Nisimalize uhondo kwenye dibaji, lakini nikupe kipande cha mwisho kwa kukufahamisha kuwa mpaka tunapata muziki huo wa dansi ulioshutumiwa kuwa wa kizazi kipya, ni matokeo ya mchanganyiko wa safari ndefu sana kutokea ‘Latin America’ Marekani ya kusini kwenye mambo ya charanga al-maarufu kama ‘Latino Fever’ Halafu macharanga hayo yakaja kuchanganyikana na mirindimo ya ‘Tembo la mnazi’ huko Afrika ya kaskazini.
Baadaye mseto huo wa kimuziki ukashuka huko Congo yanakotokea mambo ya kavasha, kabla ya kuja kuchanganyika na mbio za ‘Benga’ la Kenya.
Halafu mchanganyiko huo ukarudi tena Afrika ya kati huku ukiwa umeongezeka uzito wa mapigo ya ngoma, kionjo kutoka Afrika ya kusini pamoja na kuchanganya vionjo vya ‘kurepu’ vya mipigo ya ‘Soul’ la Marekani Kaskazini na kuzaa hicho unachokijua hivi sasa. Msomaji, nisikupeleke kasi sana, tuweke kituo hapa kwa leo.
Usikose nakala yako Jumapili ijayo tutakapoanza rasmi safari ya kuitafuta sebene ndani ya historia ya muziki wa dansi.
Mwandishi wa makala hii ni mwanamuziki mkongwe wa miondoko ya reggae hapa nchini. Kwa maoni na ushauri anapatikana kwa simu namba +255 752 227 594, barua pepe: rasinnonganyagwa@yahoo.com