Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Sheria ya makosa ya kujamiiana inawapendelea wanawake?
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Sheria ya makosa ya kujamiiana inawapendelea wanawake?
By Marshy Abdu | Published  09/24/2007
Daniel Misheto


TANZANIA kama ilivyo kwa nchi nyingine zinazoendelea imekuwa na makosa yanayotendwa na jamii na juhudi za kuifanya jamii ijirudi mara nyingi imekuwa ni tatizo lililogeuka kuwa kero.

Historia ya binadamu inaonyesha kuwepo kwa hali ya mtu kupenda au kutamani kitu fulani hata kama si chake na matamanio hayo yanapozidi huweza kutwaa kitu hicho pasipo ridhaa ya mwenyewe, huo unakuwa wizi au unyang’anyi.

Makosa hayo ni pamoja na makosa ya kujamiana, ambapo baadhi ya watu katika jamii yetu wamekuwa wakiyafanya ili kufurahisha nafsi zao bila kujali usumbufu au maudhi, au maumivu ayasababishayo kwa mwenzie.

Kwa karne nyingi makosa haya ya kujamiana yamekuwa yakihusishwa na wanaume, maana kwa kadiri ya muonekano wao kimaumbile na kiasilia, wamekuwa wakiwaka tamaa zaidi ya jinsia ya kike.

Hata wataalamu wa saikolojia na kibaiolojia wanakubali kuwa jinsia ya kike hisia zao za kimatamanio (ashiki) haziko nje nje kama za wanaume ambao zao zipo kwenye macho yao.

Kwa sababu ya mtazamo huu, imeaminika kuwa aghalabu wanaume ndio wenye kutenda makosa haya na hivyo sheria ya makosa ya kujamiiana ikaelekeza hasira zake kwa jinsia ya kiume tu.

Ndiyo maana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali hususan Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na haki za binadamu, mwanzoni mwa mwaka 1998 walipeleka muswada bungeni ambao ulipitishwa kuwa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998 ambayo ilianza kutumika Julai mosi, 1998 nchini.

Sheria hii ilipita kirahisi bungeni kwani ilipambwa na vipengele vya haki za binadamu ambazo zilikuwa zina msukumo mkubwa kutoka Umoja wa Mataifa na Tanzania ni moja ya nchi zilizoridhia kanuni hizo.

Kutokana na sheria hii kukubalika kumelazimisha mabadiliko kadhaa kufanyika kwenye sheria ya kanuni ya adhabu (Penal Code Cap 16); Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka ya Jinai (Criminal Procedure Act, 1985); Sheria ya vijana na watoto wadogo (Children & Young person Ordinance Cap 13) na zinginezo.

Nafurahi kuelewa kuwa mabadiliko hayo yalilenga katika kuboresha na kulinda maadili na mahusiano ya kijamii.

Kubaka ndilo kosa kubwa linalotawala mazingira ya makosa ya kujamiiana ambalo kwa bahati mbaya kabisa, limeonyeshwa kuwa linafanywa na watu wa jinsia ya kiume tu wakiwafanyia watu wa jinsia ya kike.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wamekuwa na swali katika mtazamo huu na wakahoji kama kweli mtu wa jinsia ya kike hawezi kutenda kosa hili kwa mtu wa jinsia ya kiume!
Habari gani kwa mwanamke kumlaghai au kumlazimisha kwa kumshawishi au kumtishia mwanamke mwenzake kutenda tendo la kusagana, je, huu si ubakaji?

Katika maandiko matakatifu hususan Biblia (Agano la Kale), tunamuona mke wa Potifa (kiongozi mmoja katika serikali ya Farao au Firauni aliyekuwa mfalme wa Misri) akimtamani mtumishi wa nyumbani (house boy) kwake na akajitahidi kumshawishi, hata kufanya juhudi za kumkamata na kumvutia kitandani akimwambia ‘Lala nami’!
Hata hivyo kijana huyu mtumishi alijitahidi kujichomoa kwa kukimbia hata kanzu yake ikachanika na akaiacha mikononi mwa mama yule.

Hivi tusemeje katika tukio kama hili licha ya kwamba tendo tarajiwa halikukamilika, lakini dhamira ya mama ilikuwa kujamiana na kijana yule, kwangu mimi naamini huu ulikuwa ubakaji kamili. Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria zetu mama yule hata leo asingepata kashikashi yoyote kwa vile yeye ni mwanamke.

Habari gani kwa kina mama wakubwa ambao nao huwatamani vijana wadogo wakiwadanganya kwa kuwapa vizawadi hadi wanalala nao?

Kidhana, kubaka ni kosa la jinai kwa mtu wa jinsia ya kiume kumwingilia (kujamiiana) msichana au mwanamke katika mazingira yafuatayo:
Kwanza, endapo atafanya hivyo kwa mwanamke ambaye si mke wake au kama ni mke waliyetengana bila ridhaa yake.

Pili, kama atafanya tendo hilo kwa ridhaa iliyopatikana kwa matumizi ya nguvu au vitisho.

Tatu, kama atajamiiana kwa ridhaa ya msichana au mwanamke wakati mwanamke huyo akiwa hana akili timamu au akiwa katika hali ya kulewa.

Nne, pale atakapojamiiana na mwanamke kwa ridhaa au bila ridhaa na binti wa miaka chini ya 18.

Pengine tulitafakari hili pia. Kwamba kama mwanaume mwenye madaraka au fedha huweza kutumia nafasi yake kumhadaa na kumpata mwanamke kwa kumuahidi kwamba atamuajiri au atamjengea nyumba, ama kumpa mapesa endapo ataridhia kutoa huduma ya kujamiana. Je, mama ambaye yuko kwenye nafasi kama huyo mwanaume hapo juu hawezi kumtaka kijana kwa njia ya kumuahidi kumpatia hiki au kile na akafanikiwa?

Habari gani mganga wa kienyeji wa kiume haiwezekani ikawa sawa kwa mganga wa kienyeji wa jinsia ya kike?

Sina shaka kila mmoja anaelewa mazingira ya usiri yanayozunguka kosa la kubaka kwamba kuna mchezo mchafu unaochezwa na baadhi ya kina dada maarufu kwa jina la mashangingi na wengine kama Changudoa waliokubuhu katika utafutaji wa pesa kwa kutumia miili yao ambapo huweza kumsingizia mwanamume kuwa amembaka ili mradi walikubaliana awali kuwapo katika sehemu fulani ya uficho ili kuhudumiana au kwa mazungumzo, lakini punde mwanamume asipokubaliana na matakwa ya huyo mwanamke ghafla huzusha madai ambayo mwanamume hakujitayarisha wala kuyatarajia. Kwa hali hii mtu wa tatu akija huweza kuamini na kumbana kijana amlipe mwanamke huyo.

Pia mara kadhaa tunashuhudia vitimbi vya vikundi vya kina dada wakimvamia mwanaume na kulazimisha afanye mapenzi nao wote au na mmoja wao. Rejeeni kina dada wanaojipanga barabarani katika mitaa kama ya Ohio, Dar es Salaam kwa shughuli hizo ambapo kina baba wengi hulizwa kila uchwao.

Hili hufanywa pia na wanaume hivyo nadhani taratibu za kisheria ziwe kama sime iwezayo kukata kuwili.

Inashangaza kuona mara nyingi watuhumiwa kwa kosa la kujamiana au kubaka wakichukuliwa mzobe mzobe kwenye kuchukua kipimo sehemu za siri za binti ili zikapimwe kuthibitisha.

Hata hivyo sheria imeumbwa kwamba kujamiana kwa minajiri ya kiushahidi kuthibitisha kosa la kujamiana inahesabika tendo hilo limefanyika iwe kimaumbile au kinyume cha maumbile ikithibitika mwingiliano tu na si mpaka kuonekana kwa mbegu za kiume.

Lakini hebu tafakarini pale ambapo awali palikuwapo na makubaliano ya wawili kushiriki tendo hilo ila baada ya tendo kukatokea kutoelewana, kwa nini kuwe na dai la kubaka?

Hivi kweli msichana anapomtembelea mwanamume nyumbani kwake kisha tendo hilo likakamilika, kosa la ubakaji linatoka wapi hapo tena?

Tazama mwanamke na mwanamume wamepatana kwenda kufanya dhambi ya uzinzi katika nyumba ya wageni, na baada ya hapo kunazuka dai la ubakaji pengine baada ya mwanamume kushindwa kulipa bili husika, hivi huu ni ubakaji na siyo kesi ya madai!
Kwa kesi hii, mwanamke akienda hospitali kupimwa ni wazi atathibitishwa kuwa ameingiliwa na huenda ikawa ni ushahidi utakaotumika maana walikuwa wawili.

Mazingira kama haya yananishawishi nione mapungufu fulani katika sheria ya kujamiiana na hakika kuna haja kubwa ya kuirejea sheria hii ili ilete maana kuliko uonevu.

Baada ya kuichambua sheria na maudhui yake na pia mazingira yaliyosababisha ikawepo hivyo, ni kwamba imetungwa ndani ya kipindi hiki cha vuguvugu la kumkomboa mwanamke kutoka madhalilisho na unyanyasaji kupitia kile kisemwacho kuwa ni mfumo dume, ndipo ikashinikizwa iwekwe pengine bila uchambuzi mpevu.

Leo tunaona wanaume wananyeshewa mvua za miaka 30, lakini wanawake hatujasikia yeyote, kwani imejengeka akilini kwa mazoea kuwa makosa ya kujamiana husababishwa na wanaume tu. Tafakarini hilo!

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.