Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Kutana na wanawake wa ‘shoka’ Tanzania
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Kutana na wanawake wa ‘shoka’ Tanzania
By Marshy Abdu | Published  09/24/2007
Mwandishi Wetu


KWA miaka mingi, wanawake wamekuwa katika harakati za kutaka usawa katika mambo mbalimbali, yakiwamo madaraka na hadhi katika jamii. Na kweli, tangu Mkutano wa Nne wa Umoja wa Mataifa wa wanawake uliofanyika mwaka 1995 huko Beijing, China, maarufu kama Mkutano wa Beijing, wanawake wengi wanaonekana kupaa katika anga za uongozi kitaifa na kimataifa. Kwa Tanzania, si haba, kuna wanawake wa mfano waliobahatika kushika nyadhifa nyeti kitaifa na kimataifa. Na tuwaangalie;

DK. ASHA-ROSE MTENGETI MIGIRO

Huyu ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Asha-Rose Mtengeti Migiro, aliyezaliwa Julai 9, 1956 mjini Songea, mkoani Ruvuma, ni mwanasheria na mwanasiasa.
Januari 5, 2007, alitangazwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Alianza kazi yake hiyo Februari 5. Ni mke wa Cleophas Migiro aliyebahatika kuzaa naye mabinti wawili.

ELIMU:
Migiro alianza elimu yake ya msingi mwaka 1963 katika Shule ya Msingi Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam. Baadaye alihamia katika Shule ya Msingi Korogwe, Tanga.
Alisomea sekondari katika shule za Weruweru Moshi na mwishowe Korogwe, Tanga alikomaliza kidato cha sita mwaka 1975.
Alijipatia shahada ya kwanza ya Sheria na ile ya pili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Shahada yake ya Uzamivu (Ph.D.) aliipata mwaka 1992 katika Chuo Kikuu cha Konstanz, Ujerumani.
Kabla ya kuwa mwanasiasa, alikuwa Mhadhiri Mwandamizi katika Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

UONGOZI:
Alianza kama utani, akiwa mjumbe wa kata wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanzia mwaka 1994 hadi 2000, na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Utendaji kuanzia mwaka 2000 hadi 2005.
Kuanzia mwaka 2000 hadi 2006, alikuwa Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia na Watoto. Alikuwa Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Januari 4, 2006, baada ya aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Jakaya Kikwete kumteua katika baraza lake jipya la mawaziri kufuatia kuchaguliwa kuwa rais.
Kwa mujibu wa maofisa wa Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Condoleezza Rice, anavutiwa binafsi na Migiro.

UMOJA WA MATAIFA:
Migiro aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UN na Katibu Mkuu wa umoja huo, Ban Ki-moon, anayetoka Korea Kusini, Januari 5, 2007.
Kwa mujibu wa Ban, Migiro ni kiongozi anayeheshimika, aliyeshiriki kikamilifu katika masuala muhimu ya nchi zinazoendelea.
Aidha, Ban alizidi kummwagia sifa Migiro akisema: “Kupitia utumishi wake uliotukuka katika maeneo mbalimbali, ameonyesha ujuzi mkubwa katika masuala ya kiutawala na akiwa na uzoefu mpana katika masuala ya kijamii na maendeleo.”

PROF. ANNA KAJUMULO TIBAIJUKA

Akiwa amezaliwa Tanzania, Tibaijuka alisoma masomo ya uchumi wa kilimo katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Kilimo Sweden huko Uppsala.
Ni mzungumzaji mzuri wa Kiingereza, Kiswahili, Kiswidi na Kifaransa. Ni mjane wa balozi wa zamani wa Tanzania, Wilson Tibaijuka aliyefariki mwaka 2000.

ELIMU:
Kuanzia mwaka 1993 hadi 1998, Tibaijuka alikuwa Profesa Mshiriki wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Wakati huo huo pia alikuwa mjumbe wa msafara wa Serikali ya Tanzania ulioshiriki mikutano kadhaa ya Umoja wa Mataifa, ukiwamo mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu makazi huko Istanbul, Uturuki mwaka 1996; Mkutano wa Chakula mjini Roma, Italia mwaka 1996; Mkutano wa Nne wa Wanawake mjini Beijing mwaka 1995 na mkutano wa dunia wa masuala ya maendeleo ya jamii mjini Copenhagen, Denmark mwaka 1995.
Wakati wa mkutano wa kimataifa wa chakula mjini Roma, alichaguliwa kuwa mratibu wa mtandao wa usalama wa chakula, Biashara na Maendeleo Endelevu kwa Afrika Mashariki (COASAD).
Prof. Tibaijuka, pia amewahi kuwamo katika bodi ya UNESCO katika masuala ya ushauri wa sayansi wa kimataifa tangu Novemba mwaka 1997.

UMOJA WA MATAIFA:
Mwaka 1998, Tibaijuka aliteuliwa kuwa mratibu maalumu wa nchi zinazoendelea juu ya biashara na maendeleo wakati wa mkutano wa UN (UNCTAD).
Septemba 2000, aliteuliwa na Katibu Mkuu wa UN wakati huo, Kofi Annan kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Makazi cha UN.
Wakati wa miaka miwili ya kuwapo kwake madarakani, Tibaijuka aliendesha mageuzi yaliyoulazimu Mkutano Mkuu wa UN kuboresha programu hiyo kuwa UN-Habitat lenye makao yake makuu Nairobi, Kenya.
Tibaijuka alichaguliwa na Mkutano Mkuu kuwa mkuu wa shirika hilo jipya wakala, Julai 2002, wadhifa alioushika kwa kipindi cha miaka minne ya muhula wa kwanza kabla ya kuongezewa tena muhula wa pili mwaka jana na alipewa cheo cha Naibu Katibu Mkuu, na kuwa mwanamke na Mwafrika wa kwanza kufikia kiwango hicho katika mfumo wa UN.
Tibaijuka, mwanamke mwenye cheo kikubwa zaidi barani Afrika katika mfumo wa UN baada ya Migiro, ameendelea kutumikia cheo chake katika chombo hicho alichofanyia kazi tangu 2000.

GERTRUDE IBENGWE MONGELLA

Mbali ya nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika ndani na nje ya nchi, kwa sasa licha ya kuwa Mbunge wa Ukerewe, Gertrude Ibengwe Mongella pia ni Rais wa Bunge la Afrika.
Alizaliwa mwaka 1945, Ukerewe, kisiwa kilichopo katika Ziwa Victoria, mkoani Mwanza, Tanzania.

ELIMU:
Alihitimu katika kilichokuwa Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki mjini Dar es Salaam mwaka 1970.
Kwa miaka mingi alikuwa mwalimu katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu Dar es Salaam.
Mwaka 1974 alikuwa mtengenezaji wa mtaala kwa ajili ya Taasisi ya Elimu Dar es Salaam kazi aliyoifanya hadi mwaka 1978.
Kuanzia mwaka 1977 hadi 1992, Mongella alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Utendaji ya Chama cha Mapinduzi CCM.
Kuanzia mwaka 1975 hadi 1982, alikuwa mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aidha wakati huo huo alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya iliyokuwa Benki ya Ushirika na Maendeleo Vijijini (CRDB). Kuanzia mwaka 1978 hadi 1982 alikuwa mkaguzi wa shule.

SERIKALINI:
Katikati ya miaka ya sabini, Mongella alikuwa mbunge katika Bunge la Afrika Mashariki. Kipindi chote cha miaka ya 1980 na sehemu ya miaka ya 1990, Mongella amekuwa mbunge katika Bunge la Tanzania.
Kuanzia mwaka 1982 hadi 1988, alikuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, kutoka hapo akawa Waziri wa Ardhi, Utalii na Maliasili, wadhifa aliuoushikilia kuanzia mwaka 1985 hadi 1987. Mwishowe kuanzia 1987 hadi 1990 akawa waziri asiye na wizara maalumu katika Ofisi ya Rais.

ANGA ZA KIMATAIFA:
Mwaka 1985, Mongella alikuwa Makamu wa Mwenyekiti wa Mkutano wa Kimataifa uliotathimini masuala ya wanawake chini ya UN.
Mwaka 1989 alikuwa mwakilishi wa Tanzania katika kamishina inayoratibu masuala na hadhi ya wanawake. Kuanzia mwaka 1990 hadi 1993 alikuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini ya Taasisi ya UN ya kimataifa ya utafiti na mafunzo ya uboreshaji hali za wanawake (INSTRAW).
Kuanzia mwaka 1991 hadi 1992, Mongella alikuwa balozi wa Tanzania nchini India, mwaka 1995 alikuwa msaidizi wa Katibu Mkuu UN na Katibu Mkuu wa Mkutano wa Nne wa Wanawake uliofanyika mjini Beijing, China.
Kuanzia mwaka 1996 hadi 1997, Mongella alikuwa mwakilishi maalumu wa UN wa Katibu Mkuu wa UN katika masuala ya wanawake na maendeleo.
Mwaka 1996 alikuwa mjumbe wa kamati ya ushauri kwa Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa Beijing barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara. Pia mwaka 1996 alikuwa mjumbe wa Bodi ya Wakala wa Urafiti na Ushirikiano wa Maendeleo mjini London.
Mwaka 1996 alikuwa mjumbe wa Mradi wa Kupambana na Njaa mjini New York, na mjumbe wa Chuo Kikuu cha UN, Tokyo, Japan. Aidha mwaka 1996 alikuwa rais mshauri wa masuala ya wanawake Afrika.
Mwaka 1997, Mongella alikuwa mshauri mwandamizi wa Katibu Mtendaji wa Kamishina ya Uchumi kwa Afrika juu ya masuala ya Jinsia.
Alikuwa mjumbe wa kamati ya OAU ya masuala ya wanawake kwa maendeleo na amani mwaka 1998. Mwaka 1999 alikuwa mjumbe wa UNESCO, Paris, Ufaransa na mwaka 2000 alichaguliwa bungeni kupitia Jimbo la Ukerewe.
Alikuwa kiongozi wa timu ya waangalizi wa OAU katika uchaguzi wa urais Zimbabwe. Mwaka 2003 ulishuhudia akiteuliwa kuwa balozi wa Shirika la Afya Duniani (WHO)-Bara la Afrika. Aliingia kama mbunge na Rais wa Bunge la Afrika mwaka 2004.

MWANAIDI SINARE MAAJAR:

Ndiye Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.
Mwanaidi Sinare Maajar, ni wakili na mshauri wa masuala ya sheria za madini. Ni mwanzilishi mwenza wa Kampuni ya uwakili ya Maajar, Rwechungura, Nguluma & Makani (Advocates), moja ya kampuni maarufu za uwakili Tanzania.
Februari 2006, Kampuni ya Maajar, Rwechungura, Nguluma & Makani pamoja na kampuni nyingine maarufu ya uwakili Tanzania, Epitome Advocates, ziliungana kuunda Kampuni ya Rex Attorneys kwa ajili ya kutoa huduma bora zaidi za uwakili katika kiwango cha kimataifa.
Alizaliwa Januari 12, 1954 Moshi, Kilimanjaro na alijiunga na kampuni ya uwakili mwaka 1991.

ELIMU:
Alijipatia shahada ya sheria ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam), 1982.
Shahada ya kwanza ya sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam), 1978 na alikuwa makamu wa rais wa serikali ya wanafunzi, Mlimani (DUSO). Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa balozi wa Tanzania nchini Uingereza, mwaka huu.
Majaar ni mtaalamu na mshauri mahiri katika masuala ya biashara, sheria za madini, uanzishaji kampuni, taratibu na sheria za ufilisi, ubinafshaji, ajira, kodi, mikataba na mengineyo. Uzoefu wake wa awali ulikuwa katika sekta za kibenki na udhibiti fedha. Alikuwa mshauri wa kisheria katika Benki Kuu ya Tanzania kwa miaka sita.
Ni mjumbe wa Chama cha Wanasheria Tanzania na alishiriki kuanzishwa kwa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS), mwaka 1995.
Ni mmoja wa wajumbe waanzilishi wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kilichoanzishwa mwaka 1990 kwa ajili ya kuwasaidia wanawake na watoto masuala ya kisheria kwa wale wasio na uwezo wa kuhimili gharama zinazojitokeza.
Alikuwa mwenyekiti wa TAWLA kati ya mwaka 2001na 2003. Kwa sasa ni mjumbe katika Halmashauri Kuu ya TAWLA.
Ni mama wa watoto watatu, lakini kutokana na kukabiliwa na majukumu mengi, daima amekuwa akimshukuru mumewe kutokana na kumwelewa na kumsaidia kwa mengi.

ZAKIA HAMDANI MEGHJI:

MAMA huyu ambaye kitaaluma ni mwalimu ndiye anayeshikilia wizara nyeti ya Fedha. Ni mwanamama wa kwanza kushika wadhifa huo nchini.

AJIRA:
Ingawa kwa sasa ni mbunge wa kuteuliwa na rais na pia ni Waziri wa Fedha, safari ya Meghji katika ajira ilianzia mbali, katika ualimu wa sekondari kati ya mwaka 1971 na 1972.
Baadaye, mama huyo mzaliwa wa Zanzibar, alifundisha katika vyuo mbalimbali, kikiwamo Chuo cha Ushirika Moshi na kufikia mwaka 1988, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya na miaka miwili baadaye Mkuu wa Mkoa.
Kwa mara ya kwanza, alikuwa waziri mwaka 1994, akianzia Wizara ya Maliasili na Utalii. Pia amewahi kuwa Waziri wa Afya. Pia ameshika nyadhifa kadhaa ndani ya CCM.

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.