WIKI hii katika taarifa ya habari iliyokuwa ikirushwa na kituo kimoja cha televisheni hapa nchini ilionyesha habari ya kukatamwa kwa kijana mmoja ambaye alikuwa akidhaniwa kuwa ni mpiga debe. Habari hiyo ilionyesha jinsi kijana huyo alivyokuwa amekunjwa na askari wa jiji na huku akiwa amejeruhiwa sana usoni kiasi cha kutokwa damu kwa wingi. Katika mahojiano na kijana huyo yeye alidai kuwa hakuwa mpiga debe ila ni kondakta, na huku askari waliomkamata wakidai kuwa ni mpiga debe.
Askari walisema kuwa walimjeruhi kwa kuwa yeye alikaidi agizo lao la kujisalimisha kwao kwa hiari.
Kitendo hiki na vingine vingi vinavyotokea katika maeneo mengi ya miji yetu hususan nilikuwa jijini Dar es Salaam, yanapaswa kulaaniwa na kukemewa na wale wote wenye nia na mapenzi mema kwa vijana na wanajamii kwa ujumla.
Ni kweli kuwa zoezi la kuwahamisha wapiga debe na wamachinga kwa sehemu moja ama nyingine tunaweza kusema limefanikiwa.
Katika maeneo mengi ya jiji ukipita kwa sehemu kubwa uliona jinsi ambavyo hali ya mji imeanza kubadilika kwani usumbufu uliokuwa unafanywa na wapiga debe kwenye vituo mbalimbali vya usafiri ulikuwa umeondoka.
Kimsingi uliona kweli kazi iliyofanywa na uongozi wa halmashauri ya jiji kwa kusukumwa na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Abbas Kandoro, imekuwa ikifanyika vema, tena kwa juhudi na mafanikio makubwa japo kwa baadhi ya maeneo zoezi hilo bado limekuwa likisuasua.
Pamoja na kupongeza jitihada hizo za uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, bado nilikuwa nina shaka na zoezi hilo ambalo limekuwa likichukuliwa kwa vijana wengi hapa nchini.
Hii ni kutokana na hatua hiyo kuchukuliwa kwa vijana hao lakini bila serikali na wanaohusika kujiuliza kama hao vijana na wapiga debe wanaofukuzwa wanakwenda wapi. Ninasema hivyo kwa kuwa ni zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa tangu serikali ya awamu ya nne iingie madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa tatu ulioshirikisha vyama vingi.
Serikali hii chini ya Rais Jakaya Kikwete iliingia madarakani kwa kaulimbiu kuwa itawawezesha vijana kujiajiri, maisha bora kwa kila Mtanzania, vijana watapatiwa ajira na kadhalika. Kwa hiyo, inawezekana kutokana na kaulimbiu hiyo, ndio maana Kikwete na chama chake waliweza kupata kura nyingi na hivyo kupata ushindi wa kishindo kama wao wanavyojivunia sasa.
Hata hivyo ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa, hali imekuwa ni tofauti na wengi walivyotarajia.
Viongozi walioingia madarakani wamekuwa na kauli zinazokatisha tamaa kwa vijana, wamekuwa wakiwafukuza na kuwaondoa katika maeneo ambayo wamekuwa wakifanya biashara zao na kuwapeleka katika maeneo ambayo hayana miundo mbinu na pia hayana wateja wala hayana nafasi ya biashara. Hivyo wafanyabiashara hao wamekuwa wakilalamika kila kukicha kuhusu hali ya biashara zao katika maeneo waliyohamishiwa. Leo zoezi la kuwaondoa wapiga debe linatekelezwa bila kukaa chini na kutafakari kama ni sahihi tena ni haki kuchukua hatua hizo bila kufikiria kama kuwahamisha wafanyabiashara hao bila mkakati endelevu ni haki.
Kinachopaswa kufafanuliwa na waheshimiwa viongozi wetu hao wenye madaraka ni juu ya hali ya maisha na mtazamo wa vijana na Watanzania kwa ujumla. Kuna msemo ambao umekuwa ukisemwa na vijana wengi kuwa, eti kauli ya Kikwete ya kuongeza ajira milioni moja kila mwaka haikueleweka bayana, wanadai kuwa yeye alikuwa na maana kuwa ataondoa vijana milioni moja kila mwaka mjini.
Hivyo kwa sasa zoezi la kuwaondoa mijini wamachinga, wafanyabiashara ndogo na wapiga debe ni katika kutekeleza adhma yake hiyo. Kama kweli kauli hii ni ya kweli na ndio inatekelezwa, basi yatupaswa vijana kufahamu kuwa kwa kumpigia kura Kikwete na serikali yake, tuliingia mkenge. Kumbe nabii tuliyemtarajia hakuwa yeye, huenda hajatokea yeye au labda mazingira ya ikulu yenye ubaridi wa viyoyozi na umeme usiokatika umembadilisha mawazo na kusahau kuwa huku nje kuna vijana wanaopigika na wala hawafahamu ni kwa namna gani maisha yetu ya kesho yatakuwa.
Kwa hali hii vijana tuna wajibu wa kufanya, ila tujiulize tutafanya nini ili kujikwamua katika hali hii duni ya maisha inayotukabili?
Pamoja na jitihada hizo za serikali kuwahamisha vijana wamachinga, wapiga debe na machangudoa wa Manzese (Uwanja wa Fisi), bila kuwapatia shughuli mbadala ni katika kuhamisha matatizo kutoka sehemu moja kwemda sehemu nyingine. Ninayasema haya kwa kuwa katika maeneo mengi ya miji yetu hali imekuwa mbaya sana kwa kuwa wale wote ambao walikuwa wakitafuta kipato cha kula yao kwa siku kwa shughuli hzo wamehamia kwenye shughuli mbadala. Changudoa wa Manzese wamehamishia shughuli zao Buguruni na kwa sasa wanafanya hadharani tena mchana kweupe.
Wapiga debe nao wameamua kuwa vibaka na wezi kwa wananchi ambao wapo mitaani. Zaidi wengi wao wameamua kujiliwaza kwa kutumia dawa za kulevya. Sasa trunajiuliza kwa hali na mwenendo huu ni kitu gani kimefanyika kweli?
Mara kwa mara nimekuwa nikisema kwa namna tunavyowachukulia vijana wetu leo bila kuwa na sera mbadala juu ya mikakati ya kuwasaidia vijana, tufahamu kuwa tunakuza matatizo makubwa ambayo yatakuwa ni kansa kubwa itakayolimaliza taifa letu siku si nyingi zijazo. Leo ukiiuliza serikali ni upi mkakati wa kuwasaidia vijana, watakwambia ni kuwapatia mikopo ambayo ipo, lakini je, ni kweli vijana wetu wanahitaji mikopo, na kama hiyo mikopo ipo mbona hatuoni matunda yake. Ile mikopo ya mwaka jana iliishia kwenye mifuko ya wajanja wachache na wala hakuna hata asilimia moja (1%) ya vijana waliopata mikopo hiyo.
Zaidi hata kama utawapa vijana mikopo hiyo kama hawana elimu juu ya ujasiriamali na vinginevyo hapo pia ni bure tu, haitawasaidia kitu. Kuna haja ya kutafakari kwa upya juu ya hali halisi ya maisha ya vijana wetu ambao tumekuwa tayari kuwaacha wakiangamia kwa ulevi, ukimwi na matumizi ya dawa za kulevya ambayo huwaletea wengi athari za kuwa wagonjwa wa akili.
Hata hivyo serikali yetu haipo tayari kujiuliza juu ya hali hiyo ila imekaa kimya na kuendesha semina na warsha kwa maafisa wenye dhamana ya kuwasaidia vijana na huku wenyewe hawajui vijana wapo wapi na wanakabiliwa na matatizo gani na ni kwa namna gani wanaweza kusaidiwa.
Ukipita leo hii, katika miji yote ya Tanzania utakutana na idadi kubwa ya wagonjwa wa akili ambayo imezidi kuongezeka, karibu kila mtaa na kitongoji kuna wagonjwa wa akili, kwenye stendi kubwa za mabasi na vituo vya daladala ndio usiseme, kwenye mabaa na migahawa wametapakaa, Muhimbili na Mirembe wamefurika, hivi wote hawa wanatoka wapi?
Mimi nadhani wanatokana na matumizi ya dawa za kulevya, nashawishika kuamini hivyo kwa sababu kwenye maeneo mengi ambayo nimepita, vijana wengi wamepatwa na uchizi kutokana na matumizi ya dawa za kulevya, bangi, heroine na cocaine ambazo zimekuwa zikipatikana karibu kila kona ya kitongoji mbalimbali.
Sote tunajua vijana wengi hapa nchini wanatumia dawa za kulevya, kuwa matumizi ya dawa hizo huwaharibu akili zao na mwisho kuwafanya wawe vichaa, lakini bado hatuoni serikali ikiweka mikakati ya maana ya kuwasaidia kwa tiba. Kwa mwenendo huu kama hatutakuwa makini na kuchukua hatua za tahadhari sasa, ipo siku mitaa maarufu kama Kariakoo itajaa vijana machizi.
Kama nilivyosema hapo juu wazo na nia ya serikali yetu katika kuwahamisha vijana wote waliopo mijini ni vema, lakini kama tusipokuwa makini tutakuwa tunapaka jipu dawa badala ya kulitumbua.
Ni kweli kuwa kuwaondoa vijana Mtaa wa Kongo na kuwapeleka Kigogo Sambusa bila kuwajengea mazingira bora ya kufanyia biashara ni kazi bure. Kuwaondoa wapiga debe vituoni bila kuwaambia ni wapi waende na zaidi wakafanye nini ni sawa na kumwambia mtoto wa kike kuwa uchumi ameukalia, hivyo atakuwa radhi kufanya lolote ili mradi aweze kuishi.
Kuwaondoa changudoa Uwanja wa Fisi bila kuwajengea akili kuwa biashara ya ngono ni hatari kwa maisha yao, ni kazi bure, kwani wao wameona kuwa hiyo ndiyo shughuli halali, kwani inawaingizia kipato bila kudaiwa kodi, hivyo hawataelewa somo lolote jingine.
Yawezekana kuwa kuna upotoshwaji mkubwa unaofanywa na watendaji wetu ndani ya serikali na ndiyo mambo yanayoendelea katika maisha ya jamii ya vijana licha ya kuwa yamekuwa yakipigiwa kelele na wadau mbalimbali kupitia kwenye vyombo mbalimbali vya habari, lakini serikali imekuwa kimya kama vile haioni.
Huu ni ukatili mkubwa, tena wa kutisha. Kwa leo tuna wajibu wa kuwasaidia vijana ili waweze kuwa na malengo bora ya maisha yao ya kesho. La sivyo tufahamu kuwa ipo siku tutailipia gharama ya kudharau kilio cha vijana hawa. Na gharama hiyo itakuwa ni kubwa na wala hatutakuwa na jinsi zaidi ya kukubali makosa.
Nimalizie kwa kusema kuwa mazingira ya nchi yetu kwa malezi na makuzi ya vijana ni mabaya sana. Kwa sasa hatupo makini kwenye nia na mikakati ya kuwasaidia vijana hawa.
Sote tumepumbazwa na dhana ya kuona kuwa kijana anaweza kujisaidia na kujitafutia mwenyewe kama kuku wa kienyeji, yawezekana ni kweli, lakini tufahamu kuwa bado kuna haja ya kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana na wale wote wenye nia ya kujiletea maendeleo.
Mungu ibariki Tanzania! Mungu wabariki vijana wa Tanzania!
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa S.L.P. 743, Arusha. Simu: 0754-000 215, barua pepe: hillarymy@yahoo.com au tovuti: www.hillarymkony.blogspot.com