Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Waacheni wapinzani wawaambie wananchi
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Waacheni wapinzani wawaambie wananchi
By Marshy Abdu | Published  09/24/2007
Christopher Nyenyembe


SAUTI ya wengi ni sauti ya Mungu na kilio cha wengi mara nyingi huwa na kishindo, huo ni ukweli usiopingika, wanaolia wengi na ndio waliozama kwenye lindi la umaskini huku wachache wanaocheka wanaishi maisha ya peponi na hawataki ukweli.

Mfumo wa vyama vingi vya siasa ulianza Tanzania kwa misingi ya kujenga taifa lenye kuendeleza demokrasia ya kweli kwa maana ya kuwapa watu sauti ya kukosoana, kushauriana kwa amani na kujenga nchi iliyotawaliwa na upendo.

Mfumo wa vyama vingi si sera ya chama tawala, (CCM), vyama vyote vya siasa vimeundwa kwa mujibu wa sheria ya nchi na si kwa matakwa ya wachache watawala na ndiyo maana kabla ya mfumo huo ilibidi wananchi watoe maoni yao.

Utaratibu huo unawafanya wananchi kuwa na nguvu ya juu kabisa katika utoaji wa maamuzi mazito katika nchi hasa linapokuja suala la masilahi ya nchi na ndiyo maana maoni kama hayo yalitumika katika uundaji wa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Hakuna chama chenye usajili mkubwa zaidi ya chama kingine, na uamuzi wa chama kipi kishike dola nao lazima utoke kwa wananchi kwani hatua hiyo ni ya msingi na inazingatia masilahi ya nchi.

Naamini kuwa hakuna chama chenye watu isipokuwa watu ndio wenye chama, wana sera na wana itikadi zao zinazowashawishi watu wengine hata kama hawana chama, lakini wana haki ya kuchagua kiongozi wanayeona anafaa.

Kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa kikiwemo chama tawala CCM hakuwezi kutoa mwanya wa kuvifanya vyama vingine vilale usingizi wa pono huku vikishuhudia utendaji mbovu wa serikali iliyopo madarakani kwa kukiuka mambo kadhaa ya msingi na yenye maslahi ya nchi.

Hiyo si kazi ya vyama vya upinzani kuendelea kulala vikisubiri uchaguzi mkuu na kuonekana kuwa havina haki ya kufichua ufisadi uliopo ndani ya serikali kwa kuogopa kuburuzwa kwenye vyombo vya dola huko ni kutaka kuunda serikali ya kidikteta ambayo haikuchaguliwa na wananchi.

Siku zote Waswahili wanasema kinyozi hajinyoi na daktari hawezi kujiganga
mwenyewe, hivi CCM na serikali yake inataka ifanye miujiza ipi ya kujinyoa yenyewe na kujiganga yenyewe, sijui huo ujuzi na maarifa hayo yametoka wapi?
Watu wanazidi kufunguka macho hawakudhani wala kufikiria kuwa viongozi wa CCM katika chaguzi mbalimbali zilizopita hadi ngazi za mikoa wamechaguliwa kwa rushwa na mashahidi wakuu wa mchakato huo ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Hakuna aliyepingana na kazi nzuri iliyoanza kufanywa na TAKUKURU ndani ya chaguzi za CCM huo ni ushahidi tosha kuwa viongozi waliochaguliwa kwa rushwa ndio hao hao waliopewa madaraka serikalini na hapo hakuna ubishi.

Kama hilo lipo na TAKUKURU wameweza kuonyesha mifano halisi ya baadhi ya makada kukamatwa na kufikishwa mahakamani na wengine kuhojiwa kutokana na vitendo hivyo licha ya wengine kutokunaswa kutokana na ukosefu wa ushahidi.

Kama hayo yameweza kutokea na inawezekana makubwa yakatokea ndani ya Ukumbi wa Kizota mkoani Dodoma mapema mwezi Novemba wakati wa uchaguzi mkuu wa CCM taifa pale kila mmoja anapohitaji kuingia kwenye kundi la washindi TAKUKURU nao watakuwepo.

Kuwepo kwa wapambanaji hao wa rushwa nje ya Ukumbi wa Kizota siku hiyo kunatokana na vitendo vilivyowashitusha watu tangu kwenye chaguzi za chini na sasa hakuna anayebisha kuwa rushwa ipo, wananchi wanajua na viongozi wa vyama vya upinzani nao wanajua.

Lakini inawezekana viongozi wa kambi ya upinzani wanajua mengi zaidi kuhusu rushwa kubwa kubwa, mikataba mibovu, matumizi mabaya ya fedha za umma, sera ya uwekezaji inavyowanufaisha zaidi wageni na mambo mengine mengi ya ufisadi.

Naamini hivyo kwa kuwa licha ya wananchi kuingiza idadi ndogo ya wabunge wa upinzani ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nao wana haki na wajibu wa kuwaeleza wananchi ni mambo yapi yanayotafuna uchumi wa nchi na kuwafanya Watanzania wengi waendelee kuwa masikini.

Hiyo ni haki ya msingi kabisa ya kambi ya upinzani na sidhani kuwa yote wanayoyasema nia yao ni kuidharirisha serikali, la hasha! Na wala si kukidhalilisha chama tawala CCM isipokuwa nia yao ni kuwafikishia ukweli wananchi ambao kinyozi hawezi kujinyoa mwenyewe.

Msajili wa vyama vya siasa hakufanya kazi ya kuwapima akili viongozi wa vyama vya siasa ili kuona ni viongozi wapi wenye akili timamu na wangapi hawana sifa za kuongoza vyama hivyo, alichokifanya aliangalia masharti na kanuni za kikatiba zinazoruhusu uundwaji wa vyama.

Msajili ndiye mlezi mkuu wa vyama vyote vya siasa, kikiwamo chama tawala na ndiye anayepaswa kuvikemea vyama vinavyokwenda kinyume na maadili ya nchi sambamba na kutokuwatendea haki wanachama wao kwa kushindwa kufanya chaguzi zao na mambo mengine.

Kamwe wananchi walioamua kujiingiza kwenye kambi ya upinzani hawawezi kuhukumiwa kuwa wametenda dhambi kwa kuikataa CCM na hawawezi kukaa kimya na kuonekana kuwa ni wachochezi pale wanapofichua maovu yaliyomo ndani ya jamii kwa kuwa nao ni sehemu ya umma wa Watanzania.

Katika mazingira hayo lazima serikali ikubali kukosolewa na ikubali kupokea ukweli unaolenga kuweka wazi hujuma mbalimbali zinazofanywa na watendaji wa serikali kwa kuamini kuwa wote waliopewa madaraka makubwa si malaika.

Ndiyo maana nasema hivi, waacheni wapinzani wawaambie wananchi ukweli na kama wananchi wanapewa maneno ya uchochezi na uongo na tuhuma zisizokuwa na ukweli wowote mamlaka inayohusika na mashitaka hayo ni mahakama, wanaolalamika waende mahakamani kutakakoweza kupatikana ukweli.

Ni mara ngapi viongozi wa upinzani tangu mfumo wa vyama vya siasa ulipoanza wametinga mahakamani na mahakama iliamua nini dhidi ya Christopher Mtikila na kesi kadhaa zipo mahakamani, ni mara ngapi Augustine Mrema amekuwa na mlolongo wa kesi mahakamani akashinda na nyingine zipo na nyingi zitakuja.

Huo ndio utaratibu na misingi bora ya utawala hivyo ni vyema viongozi wa vyama vya siasa au chama tawala CCM kwa kutokuridhika na yale ambayo watendaji wao ndani ya serikali wanashutumiwa ni vyema waende mahakamani tukiamini kabisa chombo chenye kutenda haki ni makakama.

Narudia kama kuna tuhuma nzito za rushwa, mikataba mibovu, ukiukwaji wa manunuzi, hiyo kazi iachiwe TAKUKURU ifanye kazi zake hakuna haja ya kutishana na kuonyeshana ubabe kwamba wapinzani wanawachonganisha watu na serikali yao wakati wananchi wanaamini kabisa serikali inayokosolewa ni ile waliyoichagua wao.

Sasa mshituko uko wapi, shinikizo la damu (BP) linatoka wapi? Vyombo vya dola vinavyohusika vipo viachiwe vifanye kazi kwa kufuata misingi ya haki na maadili safi ya utumishi bila kupendelea upande wowote wala kuzingirwa na itikadi ya chama kimoja.

Kazi kubwa ya chama tawala ni kurekebisha yale ambayo upinzani wanayasema na hakuna haja ya serikali kuzunguka nchi nzima kupingana na ukweli, kwani ukweli utajieleza pale mambo yatakapowekwa hadharani.

Vyama vya upinzani havina kazi nyingine zaidi ya hiyo ya kuikosoa, kuishauri na kuiasa serikali iliyopo madarakani kwa mambo ambayo yanaonekana kwenda mrama na hakuna Mtanzania mwenye dhamira ya kuishi maisha ya umaskini wa kutupwa huku wachache wanaonekana wakiishi peponi.

Waacheni wapinzani wawaambie wananchi, kazi iliyobaki serikali itekeleze sera zake kama ilivyowaahidi wananchi vinginevyo mvutano uliopo unatoa nafasi kubwa ya kuwafanya wananchi waamini kabisa kipo kinachofichwa ndani ya tuhuma hizo, kwani tayari Watanzania wamefungua masikio.


Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu; 0754 301 864 au barua pepe: cnyenyembe@yahoo.com

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.