Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Ole wenu siku yenu ikifika!
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Ole wenu siku yenu ikifika!
By Marshy Abdu | Published  09/24/2007
Juvenalis Ngowi


SINA raha kila ninapotambua kwamba siku yangu itafika. Sina hamu ya kufikiria kwamba nitakabiliwa nayo. Nafsi yangu inapata msononeko nikijua kwa hakika siku hiyo inafika na hapo mamlaka yangu na enzi za dunia hii zitatoweka.

Nina hofu kuu pale ninapowaza na kugundua kwamba utukufu wa ulimwengu huu hautadumu daima na milele. Nasikitika na sitaki kuifikiria siku hiyo.

Kwamba ipo siku nitatakiwa kutoa hesabu kwa yale yote niliyoyafanya nikiwa juu ya uso wa sayari hii. Natamani niondoe mawazo hayo kichwani mwangu ili niweze kufurahia kwa kuponda mali bila mtikisiko kwenye akili yangu. Nataka kuiua dhamiri yangu ili isijenifanya nikose uroda wa wizi ninaoufanya. Sitaki nafsi yangu ijue ubaya wa mikono yangu. Sitaki kufikiri kwamba ipo siku kila kilichofunikwa kitafunuliwa na kilicho gizani kitakuwa kwenye mwanga. Sitaki siku hiyo ifike.

Bahati mbaya kwamba nia zangu za kuzuia siku hiyo hazina nguvu kuliko ile itakayokuja kunitwaa na kunipeleka mbele ya hukumu ya haki. Natamani huko ningekutana na wala rushwa ili wageuze yale niliyoyafanya juu ya sayari hii bila hofu wala woga.

Nikikumbuka mambo niliyoyafanya na ninayoendelea kuyafanya naona kinyaa. Natamani wenzangu nao wangejisikia kama nijisikiavyo mimi ili waachane na ubatili wao kabla siku haijafika. Siku hiyo inakuja tena kila dakika ikatikapo, siku hiyo inasogea. Inatisha.

Sitaki siku hiyo niwe katika lile kundi la wanyang’anyi wa uchumi wa nchi. Nani atalipa hasara ya fedha na hali waliyoisababisha kwa maguvu yao? Yuko wapi wa kuwaokoa na hasira itakayoshuka juu yao kwa wizi na kufuru walizofanya? Fedha za wizi na madawa hazitatosha kuhonga ili kuzuia adhabu ya haki itakayoambatana na mwisho wa ufedhuli wao.

Siku hiyo ya mwisho itakuwa ni siku ya mwisho wa vitisho na kebehi kwani wakati huo mwili utakuwa dhaifu. Maungo yatakuwa yamelegea na bila shaka nuru ya macho itafifia kabla haijazima kabisa. Mwisho moyo utakoma kudunda, pumzi itaziba na damu itakataa kuzunguka mwilini. Nini kitabaki licha ya yote mliyojikusanyia? Ni kiwiliwili baridi kisichoweza tena kufurahia haramu iliyokusanywa, kwani hicho kitawekwa katika kaburi lenye kiza cha kutisha katika kimya kikuu. Siku hii inanitisha na inanifanya nitubu. Nani ataikwepa siku hii? Yuko wapi ambaye anadhani hila na ujanja vitamfanya anusurike na haya niyasemayo? Hayupo nawaapia!

Fedha za dhuluma hazitakuwa na faida tena. Madawa haramu hayatakuwa na nafasi ya vyeo havitamudu kuninusuru maana hapa lazima hesabu ya kila tendo ifanyike pasi kuwa na nafasi ya kutoa mlungula kama mlivyozoea. Hakuna kulalamikia kughushi wala kudanganya. Ukweli utakuwa hadharani na umaarufu utaaribika katika udongo.

Yuko wapi wa kuwaponya mafisadi na siku hii ya kuhukumiwa kwa dhihaka waliyofanya dhidi ya mwanadamu, ubinadamu na ardhi?

Makusanyo ya amana na mlundikano wa sarafu hautakufanya usiifikie siku hii. Mbaya zaidi hutakwenda nazo mbele ya Mzee wa Siku! Hizo utaziacha nyuma au zikigombaniwa na mafisadi wenzako au wenye chao watachukua na kugawana. Utatangulia kimya bila nyongeza ya kiwiliwili chako. Wachache wataweza kwenda na kipande cha sanda au jeneza litakalooza baada ya muda. Kama hivi ndivyo, iko wapi faida ya kuiba ili ujijengee majumba makubwa kwa jasho tamu la wenye nchi?

Mbona mwisho wa yote ni mwili kuoza na kurudi udongoni? Hakuna kalumanzila anayeweza kukuepesha na siku hii. Yote utayaacha hapa wakati mwili wako ukitafunwa na funza ardhini. Ole wako!

Bahati mbaya kinga za ulimwengu huu hazitoshi kuzima haki. Ubabe wa dunia hii hauna nguvu zaidi ya pumzi iliyojaa ukweli. Mbwembwe na kejeli za sasa hazitaweza kuzima sauti ya unyoofu itakayokuwa ikikuhukumu siku hiyo. Naam! Wingi wa suti kutoka Ulaya hautasaidia, maana sana sana mwili wako utavikwa sanda sawa kama mwili wa hohehahe. Hapo ndipo waliosalia watajiuliza: “Kumbe mbwembwe zote zile haziwezi kumtoa kaburini? Na watakufa pia hao wenye kuzodoa wengine kama vile ndio waliopewa ulimwengu huu waumiliki na kuutumia watakavyo.

Bahati mbaya wakati wa kuifikia siku hiyo hakuna kupigiwa kura na wana wa ulimwengu huu ili kujua nani abaki na yupi aende!

Ingekuwa hivyo hatuna shaka mngetumia takrima kuzuia yeyote ambaye angependekeza siku yenu ifike. Takrima, rushwa, mlungula, bahasha, hongo na chochote unachoweza kuwazia hakitakuwa na usaidizi muda ukiwadia. Hakuna walinzi watakaomudu kukulinda na saa ile inayokusubiri ile ukaseme ulifanya lipi duniani na kwa faida ya nani.

Ole wao waliotumia rasilimali za ulimwengu huu kuuharibu kwa faida ya matumbo yao ambayo nayo lazima yaozee udongoni! Watajibu nini siku ikifika? Mimi naijutia siku hiyo maana najua inatisha. Makusanyo na ufisadi wote hautakuwa na maana kwa kuwa hakuna kitakachoingia na wewe kaburini.

Hakuna haja ya wakati huo kujua ulipokea ‘cha juu’ kwa kiwango gani maana hiyo haitakuwa kinga ya kuzuia kaburi lisijifungue na kukupokea.

Mwisho, unafika, na mamlaka, uwezo, kejeli, mbwembwe, kuzodoana na kudharauliana kutafikia ukomo kwani mdomo wako hautakuwa na uwezo tena wa kufunguka ili ulimi uruhusiwe kuumba maneno kama ulivyozoea kutumia ulimi huo kudanganya na kujipatia maisha kwa jasho tamu la watu wako. Ole saa hiyo itakapofika.

Wakubwa wenzako watakuzunguka na kukutazama lakini hawataweza kubadilisha chochote. Hakuna kanuni itakayoweza kukuamsha utakapokuwa umelala kimya kwenye jeneza lako. Hakuna. Utakwenda mwenyewe na wengine tutafuata. Magari ya kifahari hayawezi kuzuia yule anayenyofoa roho yako ashindwe kukufikia. Asiyeamini atazame historia. Wako wapi kina Mobutu Sese Seko? Tena nani anaweza kutuambia ikiwa Sani Abacha yuko wapi leo? Kwani Botha yule kaburu aliyefanya kufuru dhidi ya binadamu wenzake ameweza nini mbele ya siku yake? Nani anadhani yeye atayakwepa yote hayo? Asiyejua kufa atazame kaburi. Historia ni mwalimu asiyekosea.

Mbona Mwalimu Nyerere anapata heshima hadi leo baada ya kuondoka duniani bila kuwa na mali za ‘kutisha’? Nani hakumbuki machozi ya watu yalivyomwagika wakati Mama Theresa wa Calcuta alipoaga dunia?

Huyu mama hakumiliki chochote zaidi ya roho yake ya kuhudumia wasiojiweza. Historia inafundisha kwamba mbwembwe hazina mwisho mzuri. Laiti wangeelewa haya wala wasingeshindana katika kuhujumu. Huko simo!

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0784 265 072 au barua pepe: kevinmakyao@hotmail.com

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.