WAKATI tunasisitiza umuhimu wa Serikali za Mitaa katika kusukuma gurudumu la maendeleo katika taifa letu, hatuwezi kukwepa kujadili wajibu wa afisa mtendaji wa kijiji/mtaa kama mlinzi wa amani. Kama tunavyofahamu au kama kuna ambao hawalifahamu hili ni kwamba, mojawapo ya wajibu za afisa mtendaji wa kijii/mtaa ni kuwa mlinzi wa amani.
Programu ya maboresho ya serikali za mitaa inalenga kutoa elimu juu ya jambo hili, ili lifahamike pande zote; kwa wananchi na kwa maofisa wenyewe. Likifahamika dhana nzima ya mlinzi wa amani inakuwa na maana na kuleta changamoto katika jamii zetu vijijini na kwenye mitaa yetu. Mlinzi wa amani ni mtu muhimu sana katika jamii zetu kwa vile bado kuna uhaba wa mahakimu na polisi.
Je, dhana hii ya mlinzi wa amani, ina maana gani? Dhana ya Mlinzi wa amani kama zilivyo dhana nyingine za kisheria hapa nchini ilianzia nchini Uingereza. Dhana hii inahusiana sana na dhana ya “Law and Order” ambayo kimsingi ni jukumu la polisi. Kilichosababisha dhana hii kuwepo ni kutokana na sababu zifuatazo hapa chini:
Kutokuwapo kwa polisi wa kutosha wa kuhakikisha kuwa sheria zinafuatwa na kuwa na utulivu wa kutosha miongoni mwa wananchi.
Haja ya kuwahusisha wananchi ili wajue umuhimu wa kuzingatia sheria kwa ajili ya kudumisha amani na utulivu.
Katika jamii kulikuwapo na watu wa kawaida walioheshimika na kutokana na kuheshimika kwao ilionekana kwamba watu hao wangeweza kupewa mamlaka ya kuwakamata watuhumiwa. Pamoja na kupewa mamlaka haya, kulikuwepo na kanuni za maadili zilizozuia mamlaka haya kutumiwa vibaya.
Ndiyo kusema kwamba, mbali na kudumisha sheria na utulivu, walinzi wa amani pia walikuwa na uwezo wa kusuluhisha mambo madogo madogo katika jamii husika. Watu walioheshimika katika jamii ambao walipewa mamlaka ya ulinzi wa amani walikuwa pia na uwezo kutamka kauli ya kuamua kama raia mmoja ni mtu mwema au la, pale uthibitisho huo ulipohitajika.
Utaratibu wa kuchanganya mamlaka ya ulinzi wa amani na utawala ulianzishwa na wakoloni. Historia inavyoonyesha ni kwamba wakoloni hawakuweza kutumia utaratibu wa kumtafuta mtu mwenye kuheshimika katika jamii ili awe mlinzi wa amani, kwa sababu haikuwa nia yao kuwapa mamlaka hayo wenyeji. Nia ya wakoloni ilikuwa ni kuweka mamlaka za aina mbalimbali katika chombo kimoja na kwa hiyo madaraka ya ulinzi wa amani walipewa watawala wa maeneo husika. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa kuunganisha mamlaka ambayo kwa sili yake ni ya kipolisi pamoja na mamlaka ya utawala. Utaratibu huu wa kuchanganya mamlaka ya ulinzi wa amani na utawala bado unatumika hadi sasa.
Walinzi wa amani ni maofisa na au watumishi wa umma ambao hupewa madaraka na sheria zilizotungwa na Bunge kufanya kazi kama polisi na mahakimu kwa madhumuni ya kulinda amani katika maeneo ambayo wao ni viongozi wa kiserikali.
Kuna sababu mbili muhimu ambazo zinapelekea ulazima wa kuwepo walinzi wa amani. Sababu hizi ni pamoja na:
Kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa katika maeneo yote hata ya vijijini katika nchi yetu ambako mara nyingi huwa hakuna hakimu wala polisi ambaye anaweza kuchukua hatua mara moja panapostahili.
Kuzisaidia mahakama za mwanzo wakati hakimu hayupo au anazungukia mahakama. Walinzi wa amani wanawasaidia mahakimu kwa kuchukua hatua ya kuhakikisha kwamba taratibu za kesi za jinai na za madai zinakuwa tayari kwa ajili ya kusikilizwa na wahusika wameitwa kuhudhuria mahakamani wakati hakimu atakapokuwepo mahakamani.
Kwa mujibu wa sheria ya mahakama namba 2 ya 1984 (Kifungu cha 51), walinzi wa amani ni:
Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, miji, manispaa au jiji;
Katibu tawala;
Watu wengine ambao Waziri wa Sheria atawateua kuwa walinzi wa amani (Maofisa watendaji wa vijiji na maofisa watendaji wa kata wanaingia hapa kwa kuteuliwa na kuapishwa kuwa walinzi wa amani).
Mlinzi wa amani anaweza kumkamata au kuamrisha kukamatwa kwa mtu yeyote ambaye anamshuhudia akifanya kosa la jinai. Aidha, mlinzi wa amani anaweza kupokea malalamiko ya mdomo au ya maandishi kutoka kwa mlalamikaji.
Mlinzi wa amani atamchuguza mlalamikai na kama ataridhika kuwa kuna sababau za msingi atatoa samansi au hati ya kukamatwa kwa mtu aliyetuhumiwa na mlalamikaji.
Mlinzi wa amani hatakiwi kutoa hati ya kumkamata mtu mpaka aridhike kwamba mtu aliyelalamikiwa anapaswa kuwekwa rumande ili kusubiri kesi au kama mlinzi wa amani ataona kuwa mtu huyo hawezi kutii amri ya kuitwa shaurini. Inasisitizwa kwamba Mlinzi wa Amani lazima akumbuke kila wakati kuwa kumweka mtu chini ya ulinzi ni kumwondolea uhuru wake. Kabla ya kumweka mtu rumande au jela mlinzi wa amani lazima kila wakati ajiridhishe kuwa kuna uwezekano mkubwa wa mtuhumiwa:
- Kutoroka au kukataa kuhudhuria mahakamani, au
- Kuvuruga ushahidi, au
- Kuwa kero kwa jamii, au
- Ametenda kosa kubwa na uchunguzi utazuiliwa ikiwa mtuhumiwa hakuwekwa chini ya ulinzi.
Kwa mujibu wa sheria ya Mahakama ya Mahakimu Na. 2 ya 1984 kifungu cha 56(b) (ii) Mlinzi wa amani ambaye ametueuliwa kuwepo mahakamani haruhusiwi kumweka mtu rumande kwa muda wa zaidi ya siku saba kwa wakati mmoja lakini ikiwa utaratibu wa kawaida wa mawasiliano kwenda kwa hakimu aliye karibu utakuwa umevunjika, mlinzi wa amani ataweza kumweka mtu rumande kwa siku zisizozidi ishirini na nane kwa ujumla wake.
Uwezo wa maofisa watendaji wa vijiji/mitaa kukamata watuhumiwa mbalimbali unatokana na sheria mbalimbali kulingana na aina ya madaraka husika. Maofisa watendaji wa vijiji wamepewa uwezo wa kukamata au kuagiza kukamata na sheria zifuatazo:
- Sheria ya Serikali za Mitaa ( Mamlaka za Wilaya) Namba 7 ya mwaka 1982.
- Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) namba 8 ya mwaka 1982.
- Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Jinai Namba 9 ya mwaka 1985.
- Sheria ya Mahakama ya Mahakimu Namba 2 ya mwaka 1984.
Ofisa mtendaji wa kijiji/mtaa anapofikiria au kukusudia kumkamata mtuhumiwa anatakiwa kupima vigezo hivi na kujiuliza kama kweli kuna haja ya kumkamata mtuhmiwa au anaweza kumweleza mtuhumiwa aende polisi au mahakanai yeye mwenye.
Kazi ya ulinzi wa amani na madaraka na uwezo wa kukamata au kuagiza kukamatwa kwa mtuhumiwa ni uwezo uliotolewa kwa mujibu wa sheria, hivyo ni lazima masharti ya kisheria yazingatiwe na kufuatwa katika kutekeleza madaraka haya. Aidha, katika kuyatumia madaraka haya, suala la haki za binadamu linatakiwa kuzingatiwa kwa kiwango cha juu. Kwa kuwa madaraka na uwezo huu ni wa kipolisi, hivyo katika kutekeleza jukumu hili la kuwakamata wahalifu, maofisa watendaji wa kata/vijiji/mitaa wanapaswa kuongozwa na kutawaliwa na masharti, miiko na taratibu zinazoongoza na kutawala Jeshi la Polisi.