MPENDWA msomaji natumaini haujambo. Waamini wa dini ya Kiislamu nawatakia mfungo wenye heri, nanyi Wakristo msikome kumuomba Mungu, na leo ni siku maalumu ya kwenda kanisani.
Wiki hii, Rais Jakaya Kikwete amemteua mwanahabari aliyebobea, Salva Rweyemamu kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano ya Umma Ikulu.
Salva anakuwa Mtanzania wa pili kushika wadhifa huo uliozinduliwa na Balozi Peter Kallaghe, ambaye sasa anaiwakilisha Tanzania nchini Canada.
Sikuwa nikiijua sana historia ya Kallaghe zaidi ya maelezo tuliyopewa siku ya uteuzi wake kuwa alikuwa mwanadiplomasia aliyebobea na wakati wa uteuzi wake alikuwa akiliwakilisha taifa letu katika moja ya nchi za Maziwa Makuu. Basi. Nakuwa mkweli kwa nafsi yangu, hilo ndilo nililijua.
Nilipopata habari za uteuzi wa Salva, sijui nini kiliipeleka akili yangu mbali kukumbuka Salva ni nani. Bila kujali kilichonisukuma, nilikumbuka kuwa Salva amepata kufanya kazi Radio Tanzania, Uhuru Publication Ltd, Habari Corporation Ltd na sasa nasikia kampuni nyingine ya G&S Media Consultancy. Kwangu yote hayo hayakuwa muhimu, pia bila kusahau nilikumbuka kuwa alipata kuwa Mwenyekiti wa Media Institute of Southern Africa (MISA) – Tanzania.
Nikamkumbuka Salva katika mikutano na makongamano mbalimbali.
Nikakumbuka uwezo wa Salva kujenga hoja, maarifa na upeo wake. Pia sikupoteza kumbukumbu juu ya uwezo wake wa kutumia lugha ya Kiingereza. Nitamalizia jingine nililokumbuka si muda mrefu, ila niseme tu kwa hili la kumudu lugha mbili Kiswahili na Kiingereza kwa ufasaha na akawa na uwezo, ushawishi na umahiri wa kujenga hoja, yaliniaminisha kuwa Rais Kikwete hakukosea kumteua kwa wadhifa huu.
Lakini pia mawazo yangu yalikwenda mbali. Nilianza kupitia makala zake za miaka ya 1995 hadi mwaka 2001. Sisemi za kabla au baada ya hapo! Nikakumbuka makala yake aliyoandika ikiwa na kichwa cha habari ‘TTCL wameamua kujinyonga, sisi tuwasaidieje?’ Makala hii ilichapishwa mwaka 2000 kwenye moja ya magazeti ya Habari Corporation.
Salva alieleza alivyokerwa na mchezo wa kubambikiwa bili kutoka TTCL ya wakati huo, na akawa akieleza faida za kuwa na simu ya mkononi. Akaeleza uwezo wa kudhibiti gharama za matumizi kwani unalipa kadiri unavyotumia (TTLC nao wameanzisha huduma hii sasa). Sentensi ya mwisho ya makala yake, ndiyo imenikumbusha makala hiyo na kuihusisha na uteuzi wake. Alisema: “Simu si anasa… mawasiliano ni msingi wa maendeleo, kwani bila taarifa au habari sahihi ni sawa na kuishi kwenye dunia ya giza.”
Nukuu hii ikanikumbusha utendaji wa Balozi Kallaghe. Ikumbukwe kati ya miaka ya 2000 na 2005, nilikuwa mwandishi wa habari za Bunge na Ikulu. Hivyo nilikuwa nikienda Ikulu mara kwa mara na bungeni ‘kama kawa.’ Uteuzi wa Kallaghe ulitokana na kilio cha siku nyingi tulichokuwa nacho wanahabari kuwa kuna urasimu wa upatikanaji wa habari na taarifa kutoka serikalini.
Alipoteuliwa Kallaghe tukajua ugonjwa umepata dawa. Nakumbuka niliandika makala ya kumpongeza Rais Benjamin Mkapa kwa hatua yake ya kusikiliza kilio cha wanahabari, japo alikuwa na utamaduni wa kutudharau na kututukana hadharani, kila tulipomkosoa. Yeye aliwapenda kina Rizi Khan, Tim Sebastian na William Joranji, waliokuwa wakimhoji baada ya kusoma taarifa za Benki Kuu na mtandao wa serikali wenye taarifa rasmi. Taarifa rasmi namaanisha zilizofanyiwa ‘kazi’ na maofisa wa serikali. Kwa vyovyote hizi ziliipamba serikali. Hii ndiyo kazi yao kuonyesha upande wa pili wa shilingi! Siwalaumu.
Hata hivyo, kidogo kidogo nilianza kukata tamaa na Kallaghe. Sijui kama alivyokuwa akitenda ndizo adidu za rejea alizopewa (anisamehe), ila nilidhani kuwa alikuwa akifanya majukumu yasiyo yake. Ghafla Kallaghe aligeuka mpambe wa Rais (Aide de Camp).
Kila tukienda Ikulu nilimuona akiwa amebeba jalada la hotuba za Rais Mkapa wakati ADC ambaye ni kazi yake kubeba hotuba hizo, kushika mihuri na kalamu za rais za kuandikia yupo. Wakawa wanapigana vikumbo. Nikajua hapa kuna mgongano wa madaraka. Kila mmoja anataka kuwa karibu na rais na pengine kupalilia kibarua kisiote nyasi!
Pengine hili lisingekuwa tatizo. Baadaye nilijawa na matumaini kuwa kwa Kallaghe kuwa karibu na rais kiasi hicho, tungekuwa tunapata habari haraka na kwa wakati muafaka kila likitokea lenye kuhitaji ufafanuzi wa serikali.
Mama yangu! Siku moja nikamwendea Kallaghe kumuomba simu yake ya mkononi, jibu alilonipa halina tofauti na alilonipa aliyekuwa Waziri wa Utawala Bora, Wilson Masilingi.
Tukiwa kwenye viwanja vya Bunge Dodoma mwaka 2003 nilikutana na Masilingi.
Tulizungumza kiasi, na baada ya mazungumzo nikamuomba simu yake ya mkononi, akanijibu hivi: “Bwana we rafiki yangu, sijakanunua bwana. Nipe ka kwako nikikanunua nitakupigia nikupe namba.” Hadi leo, labda nisipoteze imani ‘akikanunua’ atanipigia.
Kwa mshangao, Mungu ni mwema, mtu mmoja alimpigia simu hiyo hiyo ya mkononi tukiwa bado hatujaagana. Iliita kwenye mfuko wa koti ‘akaimezea’ kama vile haisikii.
Nikamwambia: “Mheshimiwa Masilingi simu yako inaita,” akasema haikuwa ya kwake alimshikia mtu! Nikacheka, akacheka. Hayo ndiyo yaliyonikuta kwa Kallaghe, alisema hana simu ya mkononi, angenijulisha iwapo angeipata, lakini hadi kesho!
Kilichoendelea baada ya hapo ni mshangao. Nilikuwa na simu ya Spika wa Bunge, Pius Msekwa, Jaji Mkuu, Barnabas Samatta, Rais Mkapa, Katibu Mkuu Kiongozi, Martin Lumbanga, Waziri Mkuu (wakati huo), Frederick Sumaye, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Omari Mahita, Mkuu wa Majeshi (mstaafu) George Waitara (alinipa mwenyewe), mawaziri na viongozi karibu wote niliokuwa nikiwasiliana nao kupata habari, lakini si simu ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma Ikulu-Kallaghe!
Hii ni ajabu. Ni masikitiko. Mtu huyu alipaswa kuwa kiungo na wanahabari, lakini kazi hii hakuifanya. Aliona ni usumbufu kuwasiliana na wanahabari, kumbe hiyo ndiyo kazi yake.
Nimeyasema haya, kumkumbusha Salva umuhimu wa mawasiliano kama alivyotuasa yeye katika makala yake. Dunia ya leo inatawaliwa na kasi ya ajabu katika sekta ya mawasiliano. Sitarajii Salva apigane vikumbo na ADC kubeba majalada ya hotuba za rais. Salva ukifanya kazi kwa utaratibu wa kujificha na kuwakimbia wanahabari, kazi yako itakuwa ngumu, hutaamini! Ukiamua kufungua milango kwa wanahabari na kuwapa habari kwa wakati muafaka, kazi yako itakuwa rahisi.
Nimalizie kwa kukutakia heri, na nieleze matumaini yangu kwako kutokana na historia yako katika vyombo vya habari kuwa utaleta mapinduzi katika sekta ya habari serikalini. Ukichagua ububu, utaididimiza taaluma ya uandishi wa habari.
Mungu ibariki Tanzania.
deobalile@yahoo.com
+44 782 82 85 001.