Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Kumbe Kingunge mganga wa JK Eleven?
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Kumbe Kingunge mganga wa JK Eleven?
By Marshy Abdu | Published  09/24/2007
Ansbert Ngurumo


KATIKA kikosi cha mashambulizi kilichotangazwa Jumamosi iliyopita pale Temeke Mwembe Yanga, Dar es Salaam, sikuona jina la Kingunge Ngombale -Mwiru.

Waliobahatika kuwamo katika kikosi hicho machachari ni: Jakaya Kikwete (kapteni), Benjamin Mkapa, Edward Lowassa, Nazir Karamagi, Andrew Chenge, Basil Mramba, Daudi Balali, Gray Mgonja, Patrick Rutabanzibwa, Nimrod Mkono na Rostam Aziz.

Hii ni timu ya wachezaji 11, ambayo sasa inajulikana kwa jina la JK Eleven. Ni timu
ya wakongwe na wazoefu. Nakwambia hivi, laiti kikosi hiki kingepambanishwa na Msumbiji, tiketi ya ‘kwenda Ghana’ ingekuwa mkononi mwetu.

Siku tatu zilizopita nilijadiliana na mzalendo mmoja juu ya JK Eleven. Akasema kikosi hiki kina kasoro. Kama mimi, na yeye akahoji: “Mbona simuoni mkongwe na mzoefu Kingunge Ngombale - Mwiru?”

Nikamjibu: “Kwani hujui? Hiki ni kikosi cha kwanza. Hii ni JK Eleven. Imejaa wakongwe na wazoefu. Kingunge ni mkongwe lakini si mzoefu; yeye ni MZEEFU.

Baadaye alinijibu akisema: “Utajuaje? Labda yeye yuko kikosi cha pili. Tusubiri hadi hapo kitakapotangazwa...maana nasikia majina bado yanaendelea kuchujwa.

Nikamjibu: “Nasikia hata yeye imemuuma sana kutokuwamo katika kikosi hiki. Na zipo dalili kwamba nafasi pekee anayoweza kushika hapa ni kushika kibendera. Hata kwenye kikosi cha pili, sitarajii Kingunge awemo. Hana sifa. Hata hivyo, hayuko mbali na kikosi, maana popote kinakokwenda naye yupo, kwa sababu ana nafasi nyeti. Ndiye mganga wa JK Eleven.”

Rafiki yangu akajibu: “Kumbe ndiye mganga wa timu! Sasa mbona yeye anafanya kazi ya msemaji wa timu? Katumwa na kocha, au amemwakilisha kapteni ambaye yuko safarini majuu? Na kocha ni nani, mbona hatukutangaziwa?”

Nikamjibu: “Hata nami nilitarajia kwamba kocha ndiye angetangaza kikosi chake. Badala yake kazi hiyo ilifanywa na MC wa kimataifa, Dk. Wilbroard Slaa. Lakini nasikia timu yenyewe inafundishwa na kocha mchezaji. Si unajua wachezaji wanalipwa vizuri kuliko makocha wao? Hataki kuacha donge hilo. Yumo humo humo. Pitia upya majina yao na sifa zao, utamtambua.

Halafu mwenzangu akataka kunikosoa, akidai nimekosea jina la kikosi. Akasema ni JK Boys. Nikamwambia hiyo haipo tena, iliondoka na Msumbiji. Nikamweleza kuwa hilo ni jina lililopenyezwa na Wanamtandao kwa waandishi na wapenzi wa michezo ili timu ya soka ya taifa iitwe JK Boys kwa sababu za kisiasa, utadhani kampuni ya mtu.

Kwao, JK ni jina tamu kuliko Taifa! Wanaona JK Boys ni bora kuliko Taifa Stars. Halafu tazama wanavyolitumia. Kila wanapokuwa wanaitabiria timu ushindi wanaiita JK Boys. Ikishindwa, wanaiita Taifa Stars! Hapo ndipo tulipofikishwa.

Halafu tunawashangaa Wahindu wanaoabudu ng’ombe wakati sisi tunakaribia kumwabudu binadamu mwenzetu, tena “tuliyemtengeneza’’ wenyewe!

Bado kidogo hata nchi itabadilishwa jina kutoka Tanzania kuwa JK Country! Si ajabu hata Uwanja wa Taifa utanyimwa jina la mzee Mkapa ’aliyeujenga’ na kuitwa JK Stadium! Si unasikia kitu kinaitwa JK billions (Mabilioni ya Kikwete). Ni upuuzi huo huo. Kwani JK hakutoa hela, wala serikali haijatoa hela na kuzipa benki. Ilichofanya ni kudhamini mikopo hiyo, benki zikatoa hela.

Nikamwambia mzalendo huyo kuwa siasa za nyumbani sasa zimekuwa za porojo na mbwembwe. Hazizingatii tena itikadi wala ukweli. Hata waliosisitiza ukweli na uwazi, waliishi gizani, wakacheza na kufunga magoli kwenye nyavu zao - dhidi ya wananchi wao wenyewe, walalahoi. Taabu inakuwa kwamba walizoea kucheza usiku gizani, sasa taa zinawaka, kila mtu anawaona!

Kwa sababu ya giza, wachezaji walishazoea kuchezea rafu na kufunga magoli ya wizi. Sasa kumekucha, taa zimewaka. Wataumia macho. Ni zamu yao kufungwa. Kazi ya mganga wao sasa itakuwa kuokota mipira kwenye nyavu
Wakati nawaza na kusema hayo, nikakumbuka tukio moja la kiibada mwaka jana, ambalo Rais mstaafu alilitumia kuomba Watanzania “wamsamehe” kwa makosa aliyotenda akiwa madarakani.

Nikakumbuka tukio jingine kama hilo lililomkutanisha Reginald Mengi na maaskofu, akaitumia fursa hiyo kukemea wanaoungama dhambi bila kutubu. Mengi akasema Watanzania wako tayari kumsamehe mtu yeyote, lakini “wanataka wanaoomba msamaha warudishe kwanza mali waliyoibia taifa.

Mara kumbukumbu zikanipeleka kwenye kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwa Watanzania, aliposema hana nia ya kumchunguza mtangulizi wake kwa tuhuma zinazotolewa, akisema: “Mwacheni Mzee Mkapa apumzike.

Ndipo nilikumbuka usemi kwamba ‘Waswahili wa Pemba hujuana kwa vilemba.’ Nikabaki kujiuliza: “Waliokuwa wanasisitiza tofauti ya Mkapa na Kikwete kama ya giza na nuru wako wapi leo? Waliomchafua Mkapa ili alegeze kamba wapitishe mtu wao wako wapi leo? Mbona baadhi yao sasa wako timu moja naye?”

Kauli hiyo ya Kikwete ikanifanya nielewe zaidi kwa nini serikali imekataa kuipa meno TAKUKURU. Ndiyo maana inafanya kazi kwa maelekezo ya rais, si ya sheria. Ndiyo maana hata baadhi ya wapambe wa rais wanajisahau na kusambaza uvumi kwamba eti rais ndiye ameagiza TAKUKURU iwakamate wale wabunge wa kafara kwa sababu yuko ‘serious na vita dhidi ya rushwa.’

Lengo lao si kujenga heshima ya taasisi, bali jina la rais! Wanaturejesha kwenye mantiki ile ile kwamba hata kama mambo yote yanaharibika, serikali inanuka rushwa, chama tawala kinaogelea katika ufisadi, wananchi wanalala njaa na kufa kwa magonjwa ya kipuuzi, wafanyakazi wanaandamana na kugoma, Bunge linazomewa, vyombo vya habari vinazibwa ‘midomo’ kwa mishiko, ahadi tamu na sheria dhalimu, uchumi unadorora na jamii inalalamika, jambo la msingi ni kulinda jina la rais!

Mawazo hayo hayo ndiyo yanasaidia kutafsiri ukali wa Waziri Mkuu Edward Lowassa na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, ilipotolewa hoja kwamba Bunge liunde kamati ya kuchunguza ubadhirifu katika Benki Kuu ya Tanzania.

Ndicho kisa cha wabunge wa CCM kushikamana kupinga Bunge lisiunde kamati teule ya kuchunguza mkataba wa Buzwagi. Ndiyo maana serikali inakataa katakata kupeleka mikataba bungeni, na wabunge wananywea. Wanaogopa kishindo cha JK Eleven.

Hata kauli tete za Kingunge si bure. Ukiona mganga wa timu anakuwa msemaji wa timu wakati kocha yupo kimya, ujue kuna jambo.

Lakini ni vema Kingunge na kikosi chake watambue kuwa hakuna mtu anayependa kuwa maskini. Kila mtu anataka kuishi maisha mema. Na kama ni kuchukua chako mapema, watu wengi wana uwezo wa kufanya hivyo; hata kuchukua vya wenzao mapema.

Na si Kingunge huyu huyu ndiye alisema: “Usipong’atuka utang’atuliwa?” Mbona yeye hang’atuki? Wanamtandao wanazunguka kila kona na kutoa wito: “Wazee wang’atuke.” Mbona hawamwambii babu yao, mganga wa timu?

Halafu timu yenyewe makini kweli, hata bila mganga inatisha. Kikwete awe kapteni acheze kiungo kulia; Mkapa kocha mchezaji namba tano; Chenge na Mkono mabeki; Rostam awe mshambuliaji; Lowassa winga wa kulia; Karamagi winga wa kushoto; Balali golikipa; Mgonja na Rutabanzibwa wachukue namba zinazobaki. Nani atawafunga? Ajabu bado wanamtegemea!

Na mbona hata wao hawawezi kugundua kwamba hata mganga wao kaishiwa dawa, na sasa ameamua kuwa msemaji? Halafu anasemea MAELEZO!

Mimi nilitarajia kumsikia Kingunge akisemea mahakamani, ili ‘wabaya’ wake wamkute huko, taifa lianze mapambano haya mapya ya ukombozi na ulinzi wa rasilimali. Vinginevyo, hana hoja, akae awe mtazamaji. Kikosi chake kinajitosheleza na kinaweza kuendelea kujaribu kufunga magoli ya wizi mchana. Tuone kama refa atayaruhusu, na mashabiki watanyamaza.

ansbertn@yahoo.com
www.ngurumo.blogspot.com
+447828696142

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.