Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Enyi vijana wa Tanzania, sasa ni wakati wa kuwasuta wabunge wetu
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Enyi vijana wa Tanzania, sasa ni wakati wa kuwasuta wabunge wetu
By Marshy Abdu | Published  09/24/2007
Deus Bugaywa


CHUMVI ni kiungo muhimu sana, kwa umahiri wake wa kutia ladha katika chakula na kuhifadhi vyakula visiharibike, bahati yake mbaya moja ni kwamba pamoja na umuhimu huo ambao pengine baadhi ya mambo yasingewezekana bila kuwepo kwake, chumvi ikiharibika haina namna ya kuiganga irudie katika hali yake.

Wakati mmoja Bwana Yesu aliwaambia wafuasi wake kuwa wao ni chumvi ya ulimwengu, kwa maana kwamba ni chachu ya mabadiliko na kupitia wao jamii yao na ulimwengu wote utabadilika. Lakini akawatahadharisha kuwa wao kama chumvi wasijiruhusu kuharibika, kwa sababu chumvi inapoharibika itatiwa nini mpaka ikolee?

Vijana katika nchi na jamii iwayo yote ni chumvi ya jamii hiyo, kwa sababu uhai na matumaini ya baadaye ya taifa lolote yanategemea sana vijana wake wanawaza, kuamua na kutenda nini. Vijana ndio chachu ya mabadiliko yoyote katika jamii.

Wao wanaweza kuijenga na kuiendeleza jamii yao kama wakitaka, lakini pia kwa upande mwingine na kwa uzito huo huo wanaweza kuibomoa na kuiparaganisha kabisa jamii yao kama wakiamua kufanya hivyo.

Wakati wa ukoloni tulikuwa na vijana shupavu ambao kama tumaini la jamii waliyokuwemo, waliona adha na tabu ya ukoloni na wakamua na kutenda kwa kadiri ya nguvu, uwezo na nia yao ya kuutokomeza ukoloni, ndoto yao ikatimia, leo tuna uhuru.

Uhuru huu haukutokana na hiari ya wakoloni, uhuru uliletwa na moyo wa uzalendo na wa uthubutu wa vijana wa enzi hizo.

Bila moyo wa dhati wa kuipenda nchi yao wa vijana wa wakati huo kina Mwalimu Julius Nyerere, Rashidi Kawawa, Titi Mohamed, Mohammed Abdulahman Babu na wenzao wengi tu, leo tungekuwa tunazungumza habari nyingine.

Wao katika zama zao waliona changamoto iliyokuwa mbele yao wakaikabili na hatimaye tukapata uhuru, hata kama ni wa bendera, lakini ulipatikana kwa juhudi na kutokukata tamaa kwao, kina babu hata walithubutu kupanga mapinduzi katika mazingira magumu na hatari sana ya Zanzibar wakati huo, ili tu kujikomboa.

Hicho ni kizazi kilichopita, leo taifa hili linahitaji ukombozi wa pili na na ambao ni muhimu sana.

Kazi hiyo ni ya kulikomboa taifa hili na minyororo ya kutokufikiri na umaskini. Inawezekana, kama vijana wa taifa hili, tunatambua tunapaswa kufanya nini, lakini sina hakika sana kama kuna kitu tunafanya kukabiliana na changamoto za taifa letu.

Taifa hili sasa linahitaji ukombozi wa pili, huu ni ukombozi wa kifikra, bila kujikomboa na utumwa wa fikra hatuwezi kuwa na matumaini yoyote ya maisha ya baadaye ya taifa hili, tutakuwa tumeamua kuchagua taifa lifie mikononi mwetu, na historia itatuhukumu kulingana na jinsi tulivyo litendea taifa letu bila huruma wala kujali.

Kwa vyovyote vile utakuwa ni muujiza kutegemea ukombozi uje bila kuhusisha vijana, vijana ndio wenye nguvu na akili zenye mitazamo jipya inayoweza kukabiliana na mikiki mikiki ya mbadiliko tarajiwa, wazee nafasi yao sasa ni washauri na wenye kurekebisha hali ya mambo pale kasi ya ujana inapotaka kupindukia hali halisi.

Kama haja ya mabadiliko na ukombozi wa pili ipo, sidhani ni suala la mjadala. Hoja ya msingi hapa ni kama wenye kuwezesha mabadiliko hayo na kuleta ukombozi huo tupo. Ninahisi kana kwamba nchi hii tunaiachia kama haina wenyewe vile, wala hakuna anayeonekana kujali.

Kwa hakika hii siyo staili nzuri kwa majaliwa ya taifa hili, inawezekana mtindo huu unatunufaisha sana kwa sasa kama watu binafsi na taasisi fulani fulani kwa muda huu mfupi, lakini matokeo yake kwa taifa na hatima yake ninaogopa hata kufikiri yatakuwaje.

Ni kama kila mtu amekata tamaa na nchi hii wala hakuna tena anayehisi uchungu kwa lolote linalotokea.

Nilikuwa najaribu kutafakari kama lile sakata la kuuza Msitu wa Mabira nchini Uganda, lingekuwa ni Tanzania nahisi msitu ule sasa ungekuwa tayari shamba la miwa.

Lakini Waganda kwa kuthamni rasilimali zao na nchi yao waliandamana na kukataa katakata kuuzwa kwa msitu ule bila kujali kwamba baraza la mawaziri walishaamua msitu ule uuzwe, na zaidi sana waliweka msimamo wa kutonunua sukari ya kiwanda kilichokuwa kinataka kununua sehemu ya msitu ule.

Leo wameweza kuunusuru msitu ule kwa uzalendo wao wa dhati kwa nchi yao, mambo yanayotokea hapa kwetu tunaishia kunung’unika tu mitaani na vijiweni hata kama yana madhara makubwa kwa taifa letu na vizazi vyake vijavyo.

Si wafanyakazi, wakulima au wafanyabiashara wote tumo kwenye mkumbo wa kutazama mambo yajiendee tu. Kwamba tuna wabunge wetu ambao kimsingi sisi ndio waajiri wao wanakwenda bungeni wanapitisha bajeti tusiyoitaka, halafu mbunge akija hakuna mtu anauliza kwanini alipitisha bajeti ile.

Kukiwa na hoja nyeti na nzito zenye umuhimu wa kipekee katika mustakabali wa taifa, mbunge anaitwa anakalishwa kwenye kamati ya chama anakwenda kuunga mkono au kupinga ili kulinda masilahi ya chama, tunaishia kunung’unika tu, kwa staili hii, mambo hayawezi kwenda.

Tunapaswa tuwakumbushe na kuwaonyesha waheshimiwa hawa kuwa mwisho wa siku sisi ndio wenye nchi, na wao ni watumishi wetu tu, kama mbunge anakwenda bungeni kutetea masilahi ya chama wakati sisi tunaumia akirudi tumwite mkutanoni atueleze anayoyawakilisha huku ni ya nani, na kama anadhani chama ndicho cha muhimu, basi abaki na chama chake sisi aturudishie ubunge wetu, tuweke mtu ambaye wala hatuhitaji takrima yake lakini ambaye atatetea masilahi yetu na ya taifa kwa dhati.

Vugu vugu la aina hii linapaswa lianzishwe na vijana, kila mbunge yeyote au diwani tukiona hana dalili za kutusaidia tumwite kikaoni tumweke kiti moto, atueleze anachagua kumtumikia nani, sisi anaotuwakilisha au vinginevyo kama anaamua kuchangua chama basi maana yake hatufai, kwa sababu hatimaye chama ni cha kupita tu, lakini taifa hili lipo daima.

Bahati mbaya sana leo hatuna vijana wengi wenye uthubutu wa aina hii, hata wasomi wanaotarajiwa kuwa wao ndio hasa watakuwa chumvi na chachu ya mabadiliko ni kama baadhi yao wanaisaliti jamii yao.

Leo utawakuta wengi wamebanana katika siasa si kwa lengo la kuleta mabadiliko, baadhi yao wanafanya siasa kujipatia mradi wao tu.

Ni haki yao kila mwananchi kujiunga na chama chochote cha siasa anachoona kina sera na mwelekeo anaodhani ni sahihi kwa taifa hili. Lakini nina hofu moja juu ya wapiganaji wetu wa kutuletea ukombozi wa kifikra.

Vijana wengi leo na baadhi yao wasomi, wanajiunga sana na chama tawala, ukiwauliza kwa nini wanajiunga huko, jibu ni rahisi sana ili mambo yao yaende safi.

Naomba nieleweke kwamba sina shida na wasomi kujiunga na chama hicho, hofu yangu ni sababu zinazowapeleka huko.

Wengi wa hawa ukizungumza nao unaona kabisa kwamba wana mambo mengi wasiyokubaliana nayo, ndani ya chama hicho lakini kwa sababu ya hofu ya kueleweka vibaya ndani ya chama, wanakuwa wanachama wasindikizaji tu, zile changamoto tunazozitarajia ndani ya chama kutoka kwa vijana ambao ndio tunaamini ni uhai wa taifa hili hatuzioni, tunasikia manung’uniko tu.

Na hii ni kwa sababu hawakwenda kwenye siasa kwa kuvutwa na itikadi au kwa uchungu wa kukomboa nchi yao, baadhi yao wamekwenda huko kwa ajili ya masilahi binafsi, na hapa ndipo hatari kwa taifa hili ilipo.

Kama inafika mahali taifa linakuwa na vijana wasioweza kusimama na kusema hili hatulikubali kwa vile si Utanzania huu au hili halina manufaa kwa nchi yetu, haijalishi nani kasema ilimradi tunaona linakandamiza masilahi ya nchi yetu, hatulikubali.

Kama hatuna vijana wa aina hii sasa, inabidi tuliombee sana taifa hili liepukane na balaa litakalolipata.

Kwa sababu hawa ndio watakuwa viongozi wa juu kesho tu au kesho kutwa, kama wanakuwa ni watu wa ‘ku – compromise’ kwenye masuala ya masilahi ya taifa letu, tunawezaje kuwa na tumaini jema na kizazi kijacho cha viongozi wa taifa hili?
Katika hali ya kawaida tunatarajia kijana wa leo msomi, anapoingia katika siasa lazima ahakikishe kama taifa ni lazima liendelee, basi atetee kwa nguvu zote masilahi ya taifa kokote aliko, asikubali kuburuzwa kwa matumaini ya vifaida visivyo na maana kwa taifa kama kuteuliwa katika nafasi za uongozi.

Tunamtarajia kijana wa namna hii hata akiwa ndani ya CCM, asikubali kuburuzwa, kama amejiunga na nia ya dhati kulisaidia taifa hili hatumtarajii afungwe mdomo kwa kuogopa kufukuzwa kwenye chama kwa kuwa kama kuutetea ukweli na masilahi ya taifa hili ndicho kilichomsukuma kuingia katika siasa, basi akiona hali ya mambo haifanani, asimame aseme hivyo.

Kwa sababu falsafa ya kijana wa taifa hili leo bila kujali itikadi yake inapaswa kuwa Tanzania kwanza, Tanzania daima, na mengine ndiyo yafuate. Kwamba kila jambo linalofanyika ili kijana alikubali na kuridhika nalo, lazima kwanza na daima liwe na masilahi kwa taifa kabla ya kitu kingine chochote.

Lakini inasikitisha kuona kwamba tuna mambo mengi nchini yanayofanywa si kwa masilahi ya taifa, lakini vijana tupo tu tunatazama na wakati mwingine
tunayashabikia kwa mkumbo wa itikadi badala ya kuyakemea.

Ni lazima tujue kuwa kama vijana tuna jukumu la ziada kwa taifa hili, zaidi ya kuwa wanachama wa vyama tu, na hili halina itikadi, hatima ya Tanzania ya leo iko mikononi mwetu, tumerithishwa nchi huru yenye siasa safi na maadili na miiko mizuri kabisa ya Kitanzania.

Leo hii hatuna maadili wala miiko, siasa zetu ni chafu kuliko uchafu wenyewe, na sisi vijana tupo tu tunatazama, mwisho wa siku hili ni deni letu kwa vizazi vijavyo, lazima tuamue sasa kama wazalendo halisi wa nchi hii kutoruhusu uchafu huu, kwa sababu uharibifu mwingi unaotokea vijana ndio wanaotumika kama mawakala wake.

Tukiamua leo tunaweza bila kujali uanachama wa vyama, huu unakuja na kupita lakini sisi ni Watanzania daima, tukatae kutumika kuliangamiza taifa hili kwa rushwa na vijizawadi vya madaraka au chochote kile.

Mtume Yohana katika uzee wake aliwakabidi kazi maalumu vijana, aliwaambia anawaandika wao kwa kuwa wanazo nguvu, na kwa nguvu hizo wamemshinda yule mwovu na wasiipende dunia wala mambo yake yaliyomo.

Nami, hata kama sijazeeka, naomba niwaandikie vijana wa Tanzania wasipende kutumika kuharibu nchi yao, wanazo nguvu na uwezo wa kuifanya rushwa na kila aina ya uozo kutoweka nchi hii, wanaweza kabisa wakiamua kuifanya Tanzania kuwa mahali salama pa kuishi, maisha ya kibinadamu na yenye staha wanaweza. Naomba kutoa hoja.

Mungu ibarika Tanzania, wabariki na vijana wake!

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0734 449 421 au barua pepe: drbugaywa@yahoo.com

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.