BAADA ya umoja wa vyama vya upinzani kutoa orodha ya vigogo wa serikali wanaotuhumiwa kuhusika na ubadhirifu wa fedha za serikali, kumekuwa na hali ya kujikanyagakanyaga kwa viongozi wa CCM na serikali katika kujibu tuhuma hizo.
Tuhuma hizo zilizotolewa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke jijini Dar es Salaam, zimewataja viongozi waandamizi wa serikali iliyopita na ya sasa wapatao 11.
Akijibu tuhuma hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Siasa na Jamii), Kingunge Ngombale - Mwiru, aliwashutumu wapinzani kwa kuwaambia kwamba wameshindwa uhuru wa siasa waliopewa na sasa wamevuka mipaka. Aliendelea kusema kwamba kinachowasumbua wapinzani ni kushindwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2005, na kushindwa bungeni. Hata hivyo Kingunge aliwataka wapinzani kupeleka ushahidi wa tuhuma hizo kwenye vyombo vya sheria ili ushughulikiwe.
Viongozi wengine waliojitokeza kujibu tuhuma hizo ni Katibu Mwenezi wa CCM Aggrey Mwanri, Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Elirehema Mkono, Waziri wa miuondombinu Andrew Chenge na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi.
Wote hao wamekanusha madai hayo na kutaka wapewe ushahidi rasmi.
Lakini tunapoziangalia tuhuma hizi, wala siyo ngeni masikioni mwa Watanzania. Labda kwa kuwa tu watuhumiwa walikuwa hawajatajwa. Alichokifanya Dk. Slaa ni kuwaweka hadharani watuhumiwa.
Ukweli ni kwamba hoja walizotoa wapinzani zimewachoma sana CCM na ndiyo maana wameshaanza kubwatuka ovyo.
Hii ni kwa sababu ukweli siku zote unauma. Na kwakuwa hakuna mtu duniani anayekubali kuitwa mwizi hata awe jambazi, basi kelele zao hazitakwisha. Uzuri ni kwamba tuhuma hizi ziko wazi kabisa, hata wananchi tunazijua fika. Zilikuwa tu zimekosa mlipuaji.
Nani asiyejua kwamba CCM ni chama kilichogubikwa na tuhuma za rushwa? Nani asiyejua mikataba mibovu ya madini na mashirika yetu? Haya yote sasa yamekuwa yakiimbwa si na vyombo vya habari tu hata viongozi wakuu wa serikali kwa nyakati tofauti wamekiri hivyo.
Mwanzoni kabisa mwa utawala wake Rais Kikwete alisema kwamba anawajua wala rushwa nchini ila anawapa muda wajirekebishe. Kauli kama hiyo inamaanisha kwamba, Rais Kikwete alikuwa anajua kabisa waliomzunguka ni wala rushwa (basi hakutaka kuwataja), lakini aliwataka wajirekebishe.
Rais pia alijua jinsi chama chake kilivyogubikwa na wala rushwa, ndiyo maana tumeshuhudia uchaguzi wa CCM ukitawaliwa na rushwa. Na kwa mara ya Kwanza tumeshuhudia TAKUKURU ikiwashughulikia wala rushwa kwenye chama hicho. Huo wote ni ushahidi wa madai ya wapinzani.
Rais Kikwete pia alifahamu rushwa ilivyotawala kwenye mikataba mibovu ya madini, akaagiza mikataba ya madini ipitiwe upya. Lakini cha kushangaza ni pale Waziri wake wa Nishati na Madini alivyomgeuka na kwenda kusaini mkataba wa madini nchini Uingereza kwa utaratibu wa zamani. Ni kashfa iliyofichuliwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe na kusababisha kufukuzwa bungeni kwa madai ya uongo.
Vile vile rushwa imetawala kwenye ubinafsishaji wa makampuni yaliyokuwa ya umma. Mengi ya makampuni hayo yaliuzwa kwa hasara kwa kisingizio cha kufilisika. Mfano, Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), Kiwanda cha Mbolea Tanga, na mengineyo. Hayo yote sasa Watanzania tunayajua hata kabla wapinzani hawajapeleka uthibitisho.
Inapaswa sasa CCM ijisafishe kwanza kabla ya kukurupuka kujibu hoja za wapinzani kwa jazba.
Madoa hayo yote niliyoyataja yataendelea kuisuta CCM popote waendapo. Na hayo ndiyo yanayosababisha Watanzania tuendelee kuwa masikini licha ya kuwa na rasilimali nyingi.
Tumesikia kwamba sasa CCM inajiandaa kuzunguka nchi nzima eti kujibu hoja za wapinzani. Napata shaka, sijui watakapofika huko vijijini watawaambia nini wananchi waliogubikwa na umaskini na huku wakijua wazi kwamba wanaowafilisi ni haohao wana CCM. Badala ya kutumia muda huu na fedha zilizopo kufufua miradi ya maendeleo, wao wanakimbizana na wapinzani, nawahakikishia kwamba wataambulia patupu. Ni bora watulie kimya tu maana kwa kufanya hivyo watakuwa wanatonesha wananchi machungu yanayowaumiza. Kama hawaamini wamuulize Naibu Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alivyozomewa na wananchi huko wilayani Geita alipowatonesha kidonda cha Buzwagi.
Siku zote CCM imekuwa ikitumia upole (umbumbumbu) wa Watanzania kujinufaisha. Na ndiyo maana hata Kingunge katika maelezo yake amewalaumu wapinzani eti wameshindwa kutumia uhuru wa siasa waliopewa na kuanza kuipaka matope serikali. Sijui Kingunge alikuwa anataka wapinzani wafanyeje pale serikali inapokuwa imekosea. Au labda alitaka wapinzani waendelee kuipongeza tu serikali kama alivyofanya John Cheyo wa UDP ambaye sasa anaoenakana kama aliyekigeuza chama hicho kuwa kama kampuni yake binafsi.
Si wapinzani tu, umma wote wa Watanzania sasa umeshabaini kwamba tunaibiwa. Watanzania wa sasa si wale wa zama zile wa kudanganywa kama watoto wadogo.
Huu ni wakati wa kuambizana ukweli tu, walivyofanya wapinzani hawakukosea kabisa lazima ukweli uwe dhahiri.
Badala ya kutumia kauli za kibabe, kejeli, na hoja za nguvu, CCM sasa ingetafakari, ni kwanini wagubikwe tuhuma za rushwa kiasi hicho? Ni kwanini umma wa Watanzania umegubikwa na umaskini kiasi hiki licha ya ahadi nyingi za maendeleo zinazonadiwa kila siku? Haya ndiyo mambo ya msingi kuliko hata kudai ushahidi wa tuhuma za wapinzani.
Hayo ni mambo ambayo Watanzania tutaendelea kuwadai CCM maana wao ndio walioshika hatamu za uongozi wa nchi hii.
Napenda kuwakumbusha CCM kwamba pamoja na kwamba katika uchaguzi wa mwaka 2005 CCM iliibuka na ushindi wa kishindo kwa 80%, kwa sasa umaarufu wake kwa jamii ya Watanzania umeshuka kwa kasi mno, tena kwa muda mfupi sana. Watu wengi wamegundua kwamba kumbe walipotea njia kuichagua CCM.
Hakuna wa kumlaumu katika hili. Matendo ambayo hayaendani na ahadi na dhamira ya chama hicho ndiyo yanawaloga Watanzania wengi ambao walikuwa na matumaini na chama hicho sasa wamekata tamaa na mwenendo mzima wa chama. Wanachofanya ni kukihesabia siku hadi utakapofika wakati wa uchaguzi.
Nawashauri CCM wajisafishe kwanza kabla ya kujibu mapigo ya wapinzani kwa sababu maovu yao yako wazi kila kona na kila mtu anaona. Mwenye Macho haambiwi tazama.