Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Serikali ijisafishe na kashfa hizi
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Serikali ijisafishe na kashfa hizi
By Marshy Abdu | Published  09/24/2007

KWA takribani mwezi mmoja sasa, muungano wa vyama vinne vya upinzani, umekuwa na mikutano ya hadhara kuelezea madai mbalimbali, hasa baada ya Bunge la Tanzania kumsimamisha kuhudhuria vikao vya Bunge, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Kabwe Zitto.

Suala la Zitto linafahamika kwa kina, lakini wapinzani hao katika kuzunguka nchi nzima wamekuwa wakiibua mambo mazito yanayogusa jamii, ikiwamo tuhuma nzito ya ufisadi unaofanywa na viongozi mbalimbali serikalini.

Umoja huo ulinguruma kwenye viwanja vya Mwembeyanga, Tandika jijini Dar es Salaam, ambako walianika orodha ndefu ya vigogo 11 wa serikali wanaodaiwa kutafuna nchi.

Baada ya viongozi hao kufanya hivyo, kumeibuka kwa mjadala mkali katika kila pembe ya nchi hii na kwa ujumla kwa asilimia kubwa umma wa Watanzania unaunga mkono hatua hiyo ya upinzani kuanika majina ya vigogo hao.

Lakini katika hali ya kusikitisha kama si ya kukatisha tamaa wananchi, mapema wiki hii serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Siasa na Uhusiano wa Jamii), Kingunge Ngombare-Mwiru, iliibuka na kusema kwamba orodha hiyo ya wapinzani ni ya uzushi na imejaa ungo.

Kingunge hakuishia hapo alikwenda mbali na kusema kwamba wanajitafutia umaarufu na pia wanataka wakamatwe na kuwataka Watanzania wapuuze tuhuma hizo za wapinzani, kwani ni za uzushi.

Kadhalika, juzi, mmoja wa watuhumiwa wa ufisadi, Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM), alikanusha tuhuma hizo na kusema hana mpango wa kumfikisha Dk. Willibrod Slaa mahakamani kwa kuwa hawana fedha za kumlipa kwa kuwa yeye ni wakili ghali hapa nchini.

Sisi wa Tanzania Daima, tunapenda kusema kwamba, tuhuma za ufisadi zilizotolewa na wapinzani ni nzito mno. Bila shaka zinahitaji kutolewa majibu sahihi, ambayo yatawaridhisha wananchi na wafadhili.

Si siri tena kwamba, tangu wapinzani waanze kuibua kashfa mbalimbali dhidi ya viongozi wa serikali, wananchi wengi wamekuwa wakiitazama serikali kwa jicho baya.

Tumeangalia kwa makini hoja zilizotolewa na Kingunge na Mkono, tunaweza kusema ni hoja dhaifu zisizoweza kushawishi umma uache kukubaliana na madai ya wapinzani.

Serikali ya Tanzania ni ya Watanzania wote na si ya viongozi wa serikali, hivyo sote tuna haki na wajibu kusema au kuinyoshea kidole pale tunapoona mambo yanakwenda mrama.

Hivi sasa dunia ni sawa na kijiji, yanayotendeka nchini yanafika nje ya nchi kwa muda mfupi na serikali ikae ikijua wafadhili hivi sasa wapo macho ili kuhakikisha misaada wanayoitoa inawafikia walengwa.

Tayari Serikali ya Uholanzi kupitia balozi wake hapa nchini, imeeleza kukerwa na tuhuma za rushwa na ufisadi zinazoendelea kujitokeza nchini dhidi ya viongozi mbalimbali, zikiwemo za Benki Kuu (BoT) na nyingine zinazohusisha moja kwa moja upotevu wa rasilimali za umma huku serikali ikiwa kimya.

Tunainga mkono Serikali ya Uholanzi kwa kauli yake, pengine serikali yetu inaweza kushtuka na kujitokeza hadharani kujisafisha kwa kuwa vyombo vya habari kila kukicha vimekua vikiandika ufisadi juu ya serikali, lakini imekuwa ikinyamaza kimya.

Na ukimya huo wa serikali sisi wa Tanzania Daima, tunasema una lengo la kukingia kifua ufisadi unaoneemesha wachache, huku mamilioni ya Watanzania wakiendelea kuwa maskini.

Hivyo basi, ndiyo maana tunasisitiza kwamba, serikali inapaswa kuibuka usingizini na kutoa kauli kuhusu madai hayo ili wananchi waendelee kuiheshimu serikali na viongozi wake, wakiwemo waliotajwa kwenye orodha hiyo ya mafisadi.

Zomea zomea kwa viongozi, viongozi kupigwa mawe, viongozi kukaribishwa na mabango kwenye ziara za kikazi, ni ishara kwamba wananchi wamechoshwa na ubabaishaji na udhalimu unaondelea kufanyika ndani ya nchi, ambao unawaathiri wananchi wengi ambao ni maskini.

Tunapenda kuchukua nafasi hii kuiambia serikali kwamba, haina budi kujisafisha kwa kuwa vigogo hao 11 ni watumishi wake, hivyo kitendo cha kukaa kimya hakileti picha nzuri kwa jamii.

Ijisafishe ili iendelee kuheshimika ndani na nje ya nchi kama ilivyokuwa ikiheshimika enzi za utawala wa Rais wa Kwanza wa nchi hii, Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.