Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Balali hajajibu tuhuma, uzalendo ni kujiuzulu
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Balali hajajibu tuhuma, uzalendo ni kujiuzulu
By Marshy Abdu | Published  07/24/2007

KWA mtu ambaye anafuatilia tuhuma zinazomkabili Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Balali, licha ya kushtuka, kusikitika na hata kubaki kinywa wazi kwa majibu aliyotoa, atakubaliana nami kuwa Balali hata kama ameonyesha kujiamini kwa sababu anazozijua, hajajibu tuhuma zinazomkabili.

Tulikuwa na hamu ya kusikia utetezi wake. Lakini kwa alivyojibu hata utaalamu anaosemekana kuwa nao unatia shaka.

Je, anajiamini kwa vile hana hatia au kama Dito, ana mtu nyuma yake?  Maana nchi yetu kwa wakubwa kukingiana vifua hata kuajiri waroho na mbweha wa kuwasafisha inajulikana.

Je, huyu aliyeko nyuma yake ana faida gani na uchafu huu? Je, ni yale yale ya ANBEN?

Kwani kusema niko comfortable hajakosea, kwa vile anajua hayuko peke yake.

Amezidi kutia aibu kujihami kuwa hata waliomtangulia walikumbwa na kashfa! Kama wewe ni mzalendo kwanini usirekebishe walipokosea?

Bado jibu linatakiwa kwa maneno na kuachia ngazi.

Kwanza, kabla ya kuendelea hebu tunukuu baadhi ya maneno ya Balali ndipo tuendelee kuangalia kama amejibu tuhuma au amejigonga na kuangusha porojo.

“Niko Comfortable, moyo wangu mweupe, ari yangu ya kazi iko juu kwani tuhuma hizo ni uongo na uzushi mtupu na siwezi kujiuzulu kwa tuhuma zisizo na ushahidi.” Sawa, huu ni uongo.

Mbona Balali hasemi ukweli ni upi? Maana siku zote uongo huondoshwa kwa ukweli na si udandizi na mitapo.

Gazeti linaendelea, ingawa hakutaja majina ya anaowatuhumu, Balali alisema tuhuma hizo zilizosambazwa kwenye mtandao wa intaneti, zimetokana na watu wenye ugomvi wa kibiashara na kusisitiza kuwa ni uzushi usio na chembe ya ushahidi..

’’Tuhuma zote dhidi yangu ni za uongo mtupu. Kwanza sijui zimetoka wapi, nani mtunzi na kwanini amefanya hivyo, hilo tunawaachia wanaofanya uchunguzi na naamini siku moja atajulikana na ukweli utajulikana, lakini mimi siwezi kujiuzulu kwa mambo ya uzushi,” alisema.

Ukiangalia utetezi wa Balali unagundua kuwa alijichanganya. Kwa mfano anasema hajui aliyetunga uongo huu lakini hapo hapo anasema anajua kuwa watunzi wa uongo huu ni watu wanaogombea biashara!

Je, hapa msikilizaji aelewe ni kati ya Balali kutojua nani na wapi zinatoka shutuma hizi na wafanyabiashara wanaogombea biashara?

Balali anawajua wenzake kuwa ni wafanyabiashara. Zinatoka wapi? Kupunjana masilahi?

Pamoja na kujitenga na kujua zilipotoka tuhuma zinazomkabili, lakini bado anajua kuwa zinasambazwa na watu wenye ugomvi wa biashara.

Je, yeye anaingiaje? Je, kuna aliowapendelea kama kina Mzindakaya na aliowakandamiza kwenye dili zao za ulaji? 

Haelezi kwanini ni wafanyabiashara na siyo wafanyakazi wa benki au raia wema! Kwanini wagombane wafanyabiashara badala ya kumalizana wao kwa wao wamsakame yeye?

 Amejuaje hivyo! Hasemi!  Kusema ukweli bado Balali hajajibu tuhuma.

Ukiachana na utetezi ukaenda kwenye somo la uzalendo ambalo hadi hapa anapotuhumiwa uzalendo wake umeishaingia doa, unashangaa uombaomba wa wananchi na utegemezi unaingiaje kwenye sakata zima?

Je, kwanini auone uombaomba na utegemezi wa wananchi wa chini wakati mtegemezi na omba omba mkuu ni serikali iliyomteua?

Kwanini auone uombaomba hapo hapo asiuone wizi, ufisadi, kulindana na ubabaishaji kama alioufanya?

Au kwa vile ndizo nyenzo zake za kuishi?  Je, kwanini asimweleze bosi wake kuwa nchi inaongozwa kwa sera na uadilifu na si kulindana, kuvumiliana, kuibiana, kudanganyana, na baya katika yote kukosa sera?

Je, kwa kuwalaumu wananchi wadogo wadogo amefikisha ujumbe au amekula muda wa wananchi tu?

Je, kwanini aeleze tatizo hili ambalo ni kikwazo kwa uchumi wetu, kwa mujibu wa Balali, wakati huu anapopaswa kujibu tuhuma zake binafsi?

Issue hapa haikuwa kujua nani mzalendo bali Balali kujibu tuhuma zinazomkabili.

Kama ombaomba anayeongoza ni kiongozi wa nchi anayekwenda kila uchao kwa wahisani hadi watu wanalalamikia ziara hizo.

Makala yangu iliyotangulia nilipomtaka Balali ajiuzulu nilitoa mfano mzuri wa uzalendo anaotaka kutufundisha Balali.

Gavana mwenzake wa Benki Kuu ya Kenya (KCB), Dk. Andrew Mullei alipotuhumiwa kutumia vibaya dola 30,000 alijiuzulu haraka ili kupisha uchunguzi ufanyike kwa uhuru.

Yeye kama Balali ni mzalendo anachoogopa kuachia ngazi ili achunguzwe na asafishwe ni nini?

Je, Balali atakubaliana nami kuwa uaminifu wake umekwisha kuingia doa?

Mwalimu Nyerere alizoea kusema kuwa mke wa kaisari alipotuhumiwa kwa kufanya ufuska, kaisari alifanya uchunguzi na kukuta hakuwa na kosa.

Lakini alisema: “Mke wangu, hata kutuhumiwa ni kosa, achilia mbali kupatikana na hatia.” Na Balali akubali kuwa tuhuma zimekwisha kumbomoa, ziwe na nia nzuri au mbaya.

Kurejesha imani ya umma ni kukaa pembeni achunguzwe badala ya kujitia uprofesa wa uzalendo.

Tungekuwa na viongozi wazalendo kama Mwalimu Nyerere tungefikishana hapa?

Je,  Balali anafahamu kuwa umma unawajua watu wengi waliomzunguka ambao walikuwa makapuku miaka minne iliyopita na sasa ni mabilionea?

Nani hajui kuwa watajwa wote kwenye taarifa anazoziita upuuzi wameukwaa utajiri ghafla bin vu kwa kushinda lotto iitwayo Balali au Anna?

Mjomba au shemeji na shanganzi wanaingiaje kwenye tuhuma zinazomkabili Balali?

Kama wapo ndugu tegemezi basi ni wake Balali mwenye.

Tuna tatizo la kujiona sisi ni wanyonge kwa kila kitu. Mtu akipata tatizo kidogo badala ya kufikiria jinsi ya kutatua, kitu cha kwanza anafikiria mhisani, tena si wa nje, ila mjomba, kaka, shangazi, hatuwezi kupiga hatua kwa kuendelea kuwa tegemezi. 

Hapa Balali anachekesha. Yeye angekuwa si mnyonge angeogopa nini kujiuzulu?

Angekuwa anajiamini kama anavyosema angejibu tuhuma badala ya kujibaraguza. Watu wanataka jibu siyo ngonjera.

 “Hatulindi mali zetu na ukienda kwenye madini utakuta watu wamejichimbia.”

Hapa nakubaliana na Balali kuwa hawalindi mali zetu. Maana wangezilinda na wananchi anaowalaumu kwa utegemezi wangejikomboa na kuwa na maisha mazuri badala ya kina Balali tu na wenzake.

Je, huu ujumbe unamhusuje mwananchi wa kawaida anayelalamika kila siku dhidi ya kashfa kama hii ya Balali, Richmond, ANBEN, ununuzi wa dege ghali, ukubwa wa serikali na matumizi mabaya ya pesa za umma ambayo amekiri kuwepo hata Benki Kuu?

“Tuache kuwa ombaomba, tuwe na uzalendo, tulinde maliasili zetu, tupende kazi na tubadili fikra zetu kwamba kuondoa umaskini inawezekana,” alisema.

Alisema baadhi ya viongozi hawana uzalendo na ndiyo maana wanapopata nafasi za kuwatumikia wananchi, wanafanya ubadhirifu bila kuchukuliwa hatua.

Yeye anataka atajiwe walioandika shutuma zake. Je, nasi tukimtaka atutajie hao baadhi ya viongozi wasio na uzalendo ambao wanafanya ubadhirifu atafanya hivyo?

Inabidi Balali afahamishwe kuwa kupatikana ushahidi kwake si tatizo kama watawala wetu wangekuwa wanawalinda watoa taarifa.

Afahamishwe kuwa walioripoti uchafu wake na wenzake si kwamba waliogopa ukweli na ithibati ya ushahidi wao. La hasha, walihofia maisha yao.

Maana wangekuwa na serikali inayoaminika na ambayo imedhamiria kupambana na ufisadi na kuwakomboa Watanzania, wangetoa ripoti na ushahidi wao wazi wazi.

Nani anataka amfuate Amina Chifupa? Nani anataka apitie njia ya kina Sokoine na Kolimba?  Isitoshe rais angekuwa na nia safi ya kupambana na ufisadi ushahidi kutolewa hadharani isingekuwa tatizo.

Kwa vile tumesalitiwa, hapa ndipo kina Freeman Mbowe wanaposema watu wajitafutie jibu wajuavyo dhidi ya ujambazi huu wa  mchana.

Na Balali kwa kujua udhaifu na uhovyo wa mfumo wetu, ameamua kudai ushahidi akijua wazi kuwa wanaojua uchafu huu ni watu wa chini yake. Hivyo akiwafahamu yeye na genge lake watawamaliza.

Kwanini hataki kuingia kwenye undani wa tuhuma badala yake anajibu kwa jibu la mkato kuwa ni uzushi na kupoteza muda kufundisha somo la uzalendo ambalo kimsingi anapaswa kufundishwa?

Kama Balali hajui hata gharama ya minara miwili ambayo mwenye kuimiliki na kuilipia ni benki yake, hapa kama siyo ulaji ni nini? Isitoshe Balali amepata muda wa kuwajua wabaya wake ambao inaonekana wamegeukana lakini hawezi kupata muda hata kukanusha kwa mfano tuhuma za kuitumia benki kulipa deni la Mzindakaya!

Je, Balali yuko tayari kuachia ngazi ili achunguzwe na asipokutwa na  hatia arejeshwe  kazini kama ilivyofanyika kwa Dk. Mullei?

Je, anaweza kutaja mali zake hadharani ili hawa wambea waumbuke.

Je, mbona haongelei mali zinazodaiwa kumilikiwa na mkewe?

Mbona hakanushi hata huyo Muganda kuwa si mkewe?

Huwezi ukapata muda wa kupiga domo wakati umekabiliwa na tuhuma nzito ukawa hukushiriki. Alichofanya Balali ni kuhakikisha hatoi habari kwa wananchi ili asijichanganye, ingawa amejichanganya.

Siku zake zinahesabika maana umma umechoka.

Licha ya kujaribu kujibu tuhuma na kushindwa, amejibu kisiasa sana.

Maana mwanasiasa kutokana na ubabaishaji kwenye jambo ukimuuliza swali anakwambia nenda kwa aliyekwambia!

Bado Balali hajajibu tuhuma. Na kama ni uzalendo tungemshauri awafundishe  waliomwajiri ambao wanatekeleza sera za ubinafsi wanazozipa jina zuri la ubinafsishaji.

Na aachie ngazi ili achunguzwe vizuri, tena na tume huru.

Kama tukiachana na tabia ya kuwaogopa wenye madaraka tukaangalia ukweli, ni kwamba majibu ya Balali yanaacha maswali mengi yenye kutia shaka kuliko majibu.

Laiti angetoa majibu kama haya mahakamani angefungwa kwa ushahidi wake maana ni ‘purely self-incurpatory’ hata kama kesi yake imesikilizwa ‘ex-parte’, yaani upande mmoja ambapo pamoja na kupewa nafasi hiyo ameshindwa kujibu tuhuma!

Alichofanya Balali, Waingereza hukiita ‘witch hunt and white wash plus ping pong to keep somebody at bay.’

Yesu alisema, utawajua kwa matendo yao. Nami nasema, utawajua kwa kauli zao za kujichanganya.

mpayukaji@yahoo.com

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.