Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  CUF wajitoe katika mazungumzo haya
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
CUF wajitoe katika mazungumzo haya
By Marshy Abdu | Published  07/24/2007
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimewekwa njia panda na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kutafuta suluhisho la kile ambacho Rais Jakaya Kikwete kwa kauli yake mwenyewe alikipachika jina la mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar.

Kwa miezi kadhaa sasa, mwenendo wa mambo umeanza kujionyesha kuwa, CCM wameamua kwa makusudi kuwacheza shere wanachama na viongozi wa CUF katika kutafuta muafaka wa kweli kwenye mazungumzo yao yaliyoanza mwanzoni mwa mwaka huu.

Kauli za ajabu ajabu ambazo kwanza zilianza kutolewa na makada mbalimbali wa CCM Zanzibar kabla hali haijatulia kwa muda na baadaye zikaanza kutolewa na wenzao wa Tanzania Bara, ni ushahidi wa wazi kwamba chama tawala kimeamua kuwapuuza wenzao wa CUF.

Kwa hakika mazungumzo ya CUF yaliyoanza kwa kishindo, yakitoa matumaini ya kuwapo kwa mapinduzi makubwa ya kifikra miongoni mwa viongozi wa juu wa CCM yanaonekana wazi kuwa kumbe ilikuwa ni danganya toto ambayo inaweza ikafananishwa na mchezo wa kuigiza.

Taarifa za sasa kwamba, Rais Jakaya Kikwete ameshindwa kujibu barua mbili alizoandikiwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kuhusu mwenendo wa mazungumzo hayo na hatua ndogo iliyofikiwa, ni kielelezo cha juu kabisa cha namna chama tawala kilivyoamua kukipuuza chama hicho cha upinzani.

Tukiwa sehemu ya Watanzania watetezi wa demokrasia, hali hii ya mambo imetusikitisha kwa kiwango kikubwa kwa sababu, viongozi wa CCM kwa makusudi kabisa wanaonekana wakiwa wameamua kuendelea kuiweka rehani hali ya kisiasa ya visiwani sawia na kuwadhalilisha wenzao wa CUF.

Kwa kulitambua hilo tunapenda kueleza waziwazi msimamo wetu bila ya kutafuna maneno, tukiiasa CUF kujitoa katika mazungumzo hayo ambayo hatua yaliyofikia hakuna lolote jipya linaloweza kupatiwa ufumbuzi zaidi ya viongozi wa chama hicho tawala kupoteza heshima yao machoni mwa wapenzi wao na wadadisi wa masuala ya kisiasa.

CUF wanapaswa kutambua na kuamini kuwa, wakati wakichukua uamuzi huo mgumu wa kujitoa katika mazungumzo hayo, wanatakiwa kutembea kifua mbele wakijiamini kuwa walifanya kila waliloweza kuvinusuru visiwa hivyo katika hatari ambayo ingeweza kutokea kutokana na mwenendo wa uchaguzi wa mwaka 2005 ambao haukuwaridhisha wengi.

Tunaamini hata Kikwete alipokuwa akitumia neno mpasuko wa kisiasa Zanzibar, akilini mwake alikuwa akiiona hali halisi ya mambo visiwani ambayo ni ajabu kuwa sasa anaonekana kutoiona tena.

Kwa kuliona hilo basi, Profesa Ibrahim Lipumba, Maalim Seif na viongozi wengine wa CUF wanao wajibu wa kuwaonyesha Wazanzibari na Watanzania wapenda demokrasia kuwa, wao ni viongozi wa watu na wanaosikiliza maoni ya watu wao ya kuwataka wajitoe katika mazungumzo ambayo yameshaonyesha kuwa hayana manufaa yoyote ya maana.

Wakati wakitafakari kuhusu kujitoa, viongozi hao wa CUF wanapaswa kutambua kuwa njia pekee ya kuiadhibu CCM na kurejesha nidhamu ya kuwatumikia wananchi ipasavyo na kufuta jeuri inayowafanya waamini kuwa nchi hii ni yao, ni kukibwaga chama hicho kupitia katika sanduku la kura.

Sisi wa Tanzania Daima tunaamini kuwa, CUF wakijipanga sawasawa kimikakati, nje ya mazungumzo haya yanayosuasua, wakianza sasa kwa kufuta dhana za kubuniwa na CCM za kukifanya chama hicho kionekane kuwa ni cha Wapemba au cha Maalim Seif, wanayo nafasi ya kuwaonyesha njia Watanzania wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Matokeo yenye utata mkubwa ya chaguzi zote tatu za mwaka 1995, 2000 na 2005 ni chachu kuu ya ushindi ujao wa chama hicho ambao iwapo siku ndoto zao zitatimia, basi Zanzibar inaweza ikaja kuwa chachu ya ushindi wa vyama vya upinzani kwa Tanzania nzima miaka michache tu ijayo. CUF wanapaswa kuwaonyesha njia Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.