Serikali yawapiga tafu vijana wa Mafia
Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana imewadhamini vijana 15 wanaotoka wilaya ya Mafia mkoani Pwani na kupata mafunzo mafupi ya fani mbalimbali za ufundi.
Mafunzo hayo ya fani ya umeme, useremala, uashi, upishi, ushonaji na kilimo yamefanyika kwenye chuo cha maendeleo ya wananchi (FDC) wilayani Kisarawe, yamewajumuisha vijana hao wa mtaani.
Kwa mujibu wa Mkuu wa chuo hicho, Bw, Stephen Msanya, amesema lengo la kutoa mafunzo hayo yatawawezesha kuajiri wenyewe na kujiongezea kipato badala ya kukaa mtaani bila ya kuwa shughuli maalum na kuwa kishawishi cha kutenda maovu.
Amesema chuo hicho kimekuwa kikipokea wanafunzi wa aina mbalimbali ambao wamekuwa wakifundishwa kozi fupi kuanzia wiki mbili kama waliyopata wanafunzi hao na kuendelea hadi miaka miwili ili kuwaezesha kuwapa mwanzo wa kupata uelewa.
Bw, Msanya ameongeza pamoja na mafunzo hayo kuwa mafupi lakini yanaanza kuwapa mwanga wanafunzi hao na hata kuanza shughuli hizo japo si kwa kiwango kikubwa ambapo nyakati nyingine shughuli wazifanyazo huwapa kipato na kuja kujiunga tena na chuo hicho.
Kwa sasa chuo hicho kimekuwa kikitoza gharama ya sh 90,000 kwa mwaka kwa wanafunzi wa bweni kiwango ambacho kipo chini ili kusaidia wazazi wenye kipato kidogo kudunduliza fedha na kuwaleta vijana wao kujiunga.