| *Aandaa kesi kutaka sheria zinazomlinda zifutwe *Ataka Bunge liweze kumwondoa rais akikiuka katiba Na Muhibu Said MWENYEKITI wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ametangaza azma ya kufungua kesi mahakamani kuomba kufutwa kwa sheria zinazomlinda rais mstaafu asishtakiwe kwa maovu aliyoyafanya akiwa madarakani na Bunge limwachishe kazi rais aliye madarakani anapokiuka Katiba ya nchi. Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya DP, jijini Dar es Salaam jana, Mtikila alisema atachukua hatua hiyo kwa kuwa anaamini kwamba uamuzi wake huo unaungwa mkono na Ibara ya 46 A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. "Tunaanza kutekeleza kwa makini matakwa ya Katiba ya 'Checks and Balances' ambayo ni kutumia mahakama kusahihisha makosa ya Bunge au Serikali," alisema. Mambo yasiyokwepeka hapa ni kufutwa kwa sheria haramu zinazomlinda rais mstaafu asichukuliwe hatua za kisheria kwa machafu aliyoyafanya akiwa madarakani, na kuachishwa kazi na Bunge la kizalendo rais aliye madarakani kwa mujibu wa Ibara ya 46 A ya Katiba anapokiuka Katiba," alisema Mtikila. Alisema mbali na kudai mambo hayo kwa kufuata mkondo wa sheria, atahakikisha pia yote anayoyadai yanapatikana kwa kuwashawishi wananchi kujitoa mhanga ili kuhakikisha wanarejeshewa nchi na urithi wao kwa ari, nguvu na kasi mpya. "Tumo katika maandalizi ya ukombozi kwa uhanga wa wananchi sambamba na mahakama, dhidi ya machafu, kama kuwapokonya wakulima na wafanyakazi benki yao ya NBC na kuwapa makaburu, kuporwa mashirika ya umma na majumba ya serikali na waliotumia vibaya dhamana waliyopewa na wananchi na mikataba yote ya kihuni iliyouza migodi, raslimali za nchi na heshima ya taifa letu kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya," alisema Mtikila. Mbali na kutangaza azma ya kufungua kesi hiyo, Mtikila alisema anaanzisha upya vita kali dhidi ya wale aliowaita 'magabacholi' kwa madai ya kuingia ubia haramu na Benki Kuu ya Tanzania (BoT). "Tutahakikisha hata kwa kutumia mahakama kwamba tume huru inaundwa na Bunge pamoja na sisi kuchunguza tuhuma zote za uharamia wa kutisha uliofanywa na BoT na magabacholi hatari," alisema Mtikila. Alisema anajiandaa kutumia sheria na katiba ya nchi kurejesha mali zote za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika hazina ya taifa, kwa madai kwamba zilichangwa na wananchi wote chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa. "Tunatafiti pia uhalali wa mabilioni ya fedha za walalahoi yanayoliwa bure kama 'ruzuku ya vyama vya siasa' kinyume na matakwa ya Katiba ya nchi na tangazo la ulimwengu la haki za binadamu, kwamba kila mtu apewe ujira halali kwa kazi aliyofanya na siyo kupewa bure walichozalisha wengine kwa jasho la damu. Huenda wote waliochoteana mapesa ya walalahoi wakalazimika kuyarudisha yote," alisema Mtikila. Alisema sambamba na hatua kali dhidi ya rais na watumishi wengine wa umma wanapotumia vibaya dhamana waliyopewa, anakusudia pia kuwachukulia hatua kali vigogo wa CCM wanaojificha nyuma ya chama hicho na kuteka biashara ya mafuta na miradi mingine ya fedha za umma. Alimtaka kigogo mmoja serikalini na wenzake aliodai kuwa wameshiriki kumpokonya mfanyabiashara aliyekuwa akimiliki mradi wa ujenzi mkoani Mwanza na bomba la mafuta, kumrejeshea kwa amani na kubuni miradi yao wenyewe. Mtikila alisema baada ya kupita siku 90 za notisi alizoipa serikali, anakusudia kufungua kesi mahakamani na kutumia nguvu ya umma ili kurejeshwa majumba ya Shirika la Mafuta nchini (TPDC) na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lililoko Mtaa wa Azikiwe, jijini Dar es Salaam kwa mashirika hayo. Aliwashauri viongozi wa vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, TLP na CUF kupeleka ruzuku ya wananchi wanayopokea kutoka serikalini kwenye chama cha DP ili ifanye kazi ya ukombozi wao. "Waache porojo za kususia uchaguzi wa 2010 kwa sababu wao ndio waliotumiwa kuhujumu maazimio ya Dodoma ya Aprili 18, mwaka 2004, hawaoni aibu? Tunawashauri waungane nasi kwenda mahakamani kupata tume huru ya uchaguzi ambayo haitahusisha Jeshi la Wananchi (JWTZ), Polisi, Usalama wa Taifa, wala wakurugenzi katika chaguzi zote zijazo. "Tupate daftari la kudumu la wapiga kura litakaloandaliwa na tume huru ya uchaguzi baada ya kukamilika zoezi la utambulisho wa raia wa nchi yetu, kama tulivyokubaliana Dodoma, wakatusaliti hawa wasanii. "Hawa ni wadanganyifu kwa sababu hata hizo pesa wanazozungukia mikoani kudanganya wamepeana na CCM kwa kigezo cha kushiriki uchaguzi, kwa hiyo mwaka 2010 watakuwa mstari wa mbele ili wapewe zaidi. Isitoshe hawataweza kulazimisha wagombea wasishiriki wakati uchaguzi wa mwaka 2010 ni wa wagombea huru wasiofungwa na minyororo ya CCM wala mashoga wake," alisema Mtikila. Madai ya Mtikila kuhusu kufungua kesi mahakamani kutaka kinga ya rais mstaafu iondolewe ili aweze kushtakiwa kwa kutumia vibaya madaraka yake, inakuja kufuatia habari ambazo kwa muda wa wiki kadhaa zilitawala katika baadhi ya vyombo vya habari, kumtaka Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa achukuliwe hatua za kisheria kwa madai ya kutumia madaraka yake vibaya alipokuwa kiongozi wa nchi. Vyombo hivyo vilidai kuwa Mkapa alianzisha kampuni yake binafsi akiwa bado madarakani, iliyotafsiriwa kwamba alikuwa anafanya biashara akiwa Ikulu, sawa na kutumia cheo chake vibaya. |