Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Mbinu mpya kwa Watanzania kuweza kuhoji viongozi wao (5)
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Mbinu mpya kwa Watanzania kuweza kuhoji viongozi wao (5)
By Marshy Abdu | Published  07/16/2007
Leah Mwainyekule


MIAKA kumi iliyopita Steven alikuwa akidhani kuwa viongozi wote ni watakatifu walioshuka kutoka mbinguni na ilikuwa ni dhambi kubwa kuliko zote kuhoji chochote wakifanyacho.

Aliamini kuwa ‘watakatifu’ hao wanaweza kuuliza, kulazimisha, kuamrisha na kutumia mali ya umma kwa namna wapendavyo na kisha kusifiwa kwa kila wakifanyacho. Lakini sasa, Steven haamini hivyo tena.

Mwezi uliopita alipata mafunzo yanayohusiana na namna ya kufuatilia pesa za umma na kwa mara ya kwanza katika maisha yake aligundua kwamba ni haki yake kuhoji fedha zinapotoka na zinavyotumika.

Alijifunza pia kwamba ni wajibu wake kujua endapo fedha zinazotolewa na wahisani zinatumika ipasavyo na kwa kiwango kinachohitajika.

Kwa sasa Steven hawaoni tena viongozi kama watakatifu, bali watumishi wa umma.

Mpangilio wa Fuatilia Pesa unaojulikana kama PETS (Public Expenditure Tracking) sasa ni sehemu ya maisha ya Steven Noel Lwitiko.

Yeye ni Mratibu wa AFNET katika Wilaya ya Mpwapwa, Dodoma. AFNET ni shirika lisilo la kiserikali ambalo linajihusisha na masuala mbalimbali yanayoigusa jamii, ikiwemo uwezeshaji kiuchumi na utawala bora.

Kwa hivi sasa Steven amejikita katika kazi moja: Kuwaelimisha wananchi wa wilaya yake kwamba wanaweza kuwahoji viongozi wao kuhusiana na jambo lolote, ikiwemo katika mikono ipi pesa za umma zinapoishia. Mlolongo huu ndio unaoitwa Fuatilia Pesa, ama PETS.

AFNET ilipokea msaada chini ya mradi wa MCA-BONGA. Mradi huo unafadhiliwa na shirika la Serikali ya Marekani liitwalo Millennium Challenge Corporation (MCC) kupitia Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na unasimamiwa na Pact Tanzania.

“Nilipozungumza na wananchi kwa mara ya kwanza kuhusiana na suala hili, walichanganyikiwa kidogo kwa sababu kama ujuavyo, wengi wetu tulishazoea kuwaabudu viongozi wetu hata wakiwa wana uozo wa hali ya juu. Lakini baadaye wakanielewa na wakafurahi kuelewa kwamba wanaruhusiwa kuwahoji viongozi wao na kutaka maelezo kuhusiana na suala lolote la kijamii ambalo hawajalielewa sawasawa,” anasema Steven.

Hata hivyo bado yapo matatizo yanayomkwamisha Steven kutekeleza wajibu wake ipasavyo, kwani watu wengi hawana uelewa wa Utawala Bora, na hata wakati mwingine inakuwa vigumu kwao kuwahoji viongozi wao.

Wengine bado wana hulka ya kudhani kwamba viongozi ni viongozi watakatifu tokea awali.

“Lakini hulka hiyo itabadilika muda wake utakapowadia,” anasema Steven kwa uhakika, akiongeza: “Kama tujuavyo Roma haikujengwa ndani ya siku moja, hivyo nitaendelea na juhudi zangu za kuwaelimisha wananchi wa Mpwapwa, na nina hakika kwamba watanielewa na kuanza kufuata masuala ya PETS.”

Kwa hivi sasa AFNET inafundisha masuala ya PETS Dodoma pekee, huku zikiwa zimeteuliwa wilaya tatu kwa ajili ya mpango huo, ambazo ni Kongwa kwa upande wa elimu, Chamwino kwa upande wa afya, na Mpwapwa katika sekta ya maji.

“Tungependa kwenda katika wilaya nyingine zaidi, lakini kutokana na suala la PETS kuwa bado jipya, msaada wa fedha umekwenda katika wilaya hizo tatu kwanza, na zitaongezeka baadaye pindi mpango huu utakapoonyesha mafanikio,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa AFNET, Sarah Mwaga.

Anakiri kwamba kutekeleza mpango wa PETS bado ni tatizo kwa watu wengi, hasa wale walioko maeneo ya vijijini ambao bado wana hofu kuu ya kuhoji wanachofanya viongozi na fedha zao.

“Wananchi wanajua kwamba ni wajibu wao kuchangia maendeleo ya jamii, lakini suala la kuhoji viongozi wao ni jingine kabisa,” anaeleza.

Kwa bahati nzuri, watu wengi wanafuraha ya kupata mafunzo kuhusiana na PETS na wameahidi kujifunza zaidi ili waweze kuelewa hasa ni namna gani wanavyotakiwa kutimiza haki yao katika upande wa utawala bora.

Mmoja wao ni mzee Mathew Mbiji wa kijiji cha Mlanga, kata ya Kongwa. Anapenda kufahamu zaidi kuhusu PETS, lakini tatizo ni kwamba haelewi.

“Sina hakika kama hiki ni kitu kipya kinacholetwa na watu wa nje ya nchi yetu kwa ajili ya manufaa yao binafsi ama ni suala ambalo litatusaidia kweli sisi Watanzania,” anasema wakati wa mkutano wa kijiji.

Lakini suala jema ni kwamba Mzee Mbiji anawahakikishia wananchi wenzake kwamba hataachana na mpango wa kujifunza kuhusu PETS.

Yupo tayari kuwasikiliza wawezeshaji na kukubaliana na suala atakaloona yeye kwamba linafaa kwa upande wake, hiyo ndio demokrasia.

Diwani wa kata ya Mlanga, White Zuberi naye ni msaada mkubwa sana linapokuja suala la kuwaelimisha wananchi wake kuhusiana na utawala bora na PETS.

Anaeleza kwamba wananchi wana sehemu yao katika kuchangia kwenye bajeti ya serikali, na hivyo wana haki pia ya kuhoji matumizi ya fedha.

“Tunakumbuka, kwa mfano, wakati wa uongozi wa Rais Mkapa nchi nyingi tajiri ziliisamehe Tanzania deni lake la nje. Sasa endapo fedha hizi ziko mikononi mwa serikali, tuna haki ya kujua endapo zinatumika kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii ama vinginevyo,” anasema Zuberi, na kuongeza kwamba atashirikiana bega kwa bega na wawezeshaji kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wanaelewa vema somo la PETS.

Chimwemwe Chikusa ni mratibu wa AFNET katika Wilaya ya Kongwa, na anashirikiana na wawezeshaji wawili katika wilaya yake ambao ni Victoria Madinda na Josina Machino.

Anaeleza kwamba suala la PETS kwao halikuibuka tu siku moja asubuhi na kujikuta wanafahamu kila kitu kuhusiana na somo hilo.

“Kwa hakika sisi wenyewe tumepokea mafunzo kuhusiana na suala hilo ambayo yaliratibiwa na makao yetu makuu.

Mafunzo haya yalikuwa kwa ajili ya wawezeshaji wote wa AFNET wanaojihusisha na masuala ya PETS mkoani Dodoma, na hivyo tuko tayari kabisa kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi,” anasisitiza kwa uhakika.

Kila wilaya inajihusisha na idadi fulani ya kata zilizoko, na hivyo kwa upande wa Kongwa, kwa mfano, Chimwemwe anasema wanajihusisha na kata kumi ambazo ni Kongwa, Ugogoni, Sagara, Iduo, Mlali, Pandambili, Segeli, Hogoro, Mkoka na Zoisa.

Kila kata ina mwezeshaji mmoja anayejishughulisha na kuwaelimisha wananchi kuhusiana na suala hilo na hivyo idadi yao ni ya kujitosheleza kabisa.

Paulo Fungulio naye ni mmoja wao. Yeye anajihusisha na Kata ya Sagara, na ana uhakika kwamba suala la wananchi kuwahoji viongozi wao kwa sasa linakubalika.

“Mara nyingi huwa ninawaelezea PETS inahusiana na nini na ni namna gani inavyowaweza kumnufaisha mwananchi wa kawaida ili aweze kujua endapo fedha za umma zinatumika ipasavyo ama la na kuchukua hatua inapobidi,” anaeleza.

“Hapo awali mimi mwenyewe sikuwahi kufikiria kwamba jambo kama hili linaweza kutokea, lakini sasa nimefurahi kujua kwamba nina uwezo wa kuwahoji viongozi wangu na kutaka maelezo katika masuala ya maendeleo,” anasema Paulo.

Anashukuru pia kwamba uongozi wa kata na kijiji wamekuwa wa msaada mkubwa na wapo tayari kushirikiana naye.

Andrew Karama ni mratibu wa AFNET Mkoa wa Dodoma. Anaeleza kwamba hapo awali AFNET ilikuwa ikijihusisha na masuala ya kampeni dhidi ya ukeketaji wa wanawake, na walikuwa wamejikita zaidi katika mikoa inayojihusisha na suala hilo, ikiwemo Dodoma.

“Lakini baadaye tuligundua kwamba suala hilo linaweza kuwa na upana zaidi, hivyo tuongezee programu zingine zinazohusiana na utawala bora.” Kutokana na hilo wakaamua kugawanya programu zao katika makundi manne kwa ajili ya kusaidia jamii kuwa mahala salama zaidi.

Makundi hayo ni ukimwi, Stadi za maisha kwa vijana, uwezeshaji kiuchumi, na utawala bora.

Anasema Karama: “Hapo ndipo PETS nayo ilipokuja kuzaliwa katika shirika letu, na tulianza kwa kuwaelimisha kwanza wawezeshaji wetu namna ya kuwaelimisha watu wengine katika suala hilo, demokrasia, na utawala wa sheria.”

Kwa mujbu wa mratibu huyo wa mkoa, wawezeshaji wao wanatoka katika maeneo mbalimbali zikiwemo shule, zahanati, makanisa, misikiti, viongozi wa serikali na kijiji, na watu wengine wa aina mbalimbali.

“Akina mama wajawazito, kwa mfano, wakienda kliniki kwa ajili ya kuangaliwa afya zao wanaweza kuzungumza na wenzao kuhusiana na PETS, namna inavyofanya kazi na ilivyo ya msaada kwetu.

Wafanyakazi wanazungumza na wafanyakazi wenzao, wafanyabiahsara wanazungumza na wateja,..na kwa namna hiyo, somo hilo linazidi kusambaa,” anafafanua.

Na kwa sasa kutokana na juhudi nzuri zilizofanywa na AFNET pamoja na wawezeshaji wake, neno PETS limekuwa ni neno linalojulikana vizuri mjini Dodoma, na linazidi kusambaa.

Itachukua muda kidogo tu kufikia hatua ya familia kukaa pamoja na kuanza kuzungumzia suala hilo kama wafanyavyo Watanzania wengine katika kliniki na kwenye maduka.

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.