Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

 »  Home  »  Blogs  »  Serikali ichambue vyema maoni kuhusu shirikisho
Marshy Abdu
Insured by Mafia Islanders You hit me!! We hit you!!! 

View all blogs by Marshy Abdu...
Serikali ichambue vyema maoni kuhusu shirikisho
By Marshy Abdu | Published  07/16/2007
KAMATI ya Kitaifa ya Kukusanya Maoni Kuhusu Uharakishwaji wa Uundwaji wa Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki, imekamilisha kazi yake jana.

Ripoti ya jumla ya kamati hiyo inaonyesha kwamba, takriban robo tatu ya Watanzania waliohojiwa kuhusu jambo hilo, walipinga kuharakishwa kwa uundwaji wa shirikisho hilo la Afrika Mashariki.

Kwa takwimu hizo, iwapo matokeo hayo ni kielelezo cha maoni ya Watanzania walio wengi, basi kila mmoja wetu anaweza akajionea mwenyewe namna Watanzania wasivyokuwa tayari, japo kwa sasa, kuingia katika shirikisho.

Ni mapema mno kuweza kujua maoni waliyonayo wenzetu nchini Kenya na Uganda kuhusu jambo hili, ingawa iwapo mwenendo utakuwa ni wa namna hii, basi huenda ajenda nzima ya ushirikiano uwe wa kisiasa au kiuchumi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikawa ngumu sana mbele ya safari.

Jambo moja kubwa linaloweza kubeba maelezo ya matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na kamati hiyo iliyoongozwa na Profesa Wangwe, ni kwamba bado imani ya Watanzania wengi kwa majirani zao katika masuala mbalimbali ni ndogo.

Kitendo cha uharakishwaji wa uundwaji wa shirikisho kukataliwa kwa zaidi ya asilimia 50 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na Visiwani, si jambo la kuliona dogo au kulipuuza hivi hivi.

Kwa mfano, taarifa kwamba asilimia 74.5 ya waliohojiwa kwa upande wa Tanznaia Bara walipinga kuharakishwa kwa shirikisho hilo, wakati Zanzibar waliopinga walikuwa ni asilimia 79, ni matokeo ambayo hayana budi kuchukuliwa kwa uzito mkubwa na viongozi wote wakuu wa Tanzania na wale wa Kenya na Uganda.

Kibaya kabisa katika matokeo hayo ni ukweli kwamba, asilimia 80.2 ya wananchi wote waliohojiwa walionyesha kufahamu vyema kuhusu maana ya shirikisho hilo.

Tunasema baya kwa sababu, matokeo ya jumla ya wananchi walio wengi kukataa kuharakisha uundwaji wa shirikisho yanatoa jibu moja tu muhimu kuwa, wamefanya hivyo si kwa ujinga, bali kwa kuelewa kile wanachokikataa, kwani tayari wanakifahamu au angalau wanao ufahamu wa kutosha kuhusu suala lenyewe.

Kwa kutambua hilo, basi tunaamini kwa dhati kwamba, ahadi aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete wakati akikabidhiwa ripoti hiyo jana kuwa serikali itayazingatia maoni ya wananchi walio wengi, itafanyiwa kazi na kuheshimiwa.

Tunasema yataheshimiwa hatuna maana kwamba serikali italazimika kutoa jibu moja la mkato kwamba Watanzania walio wengi hawalitaki shirikisho, la, bali itachambua maoni na kuhakiki iwapo zile sababu za kulikataa zinaweza zikafanyiwa kazi na kurekebishwa haraka kwa kadiri inavyowezekana.

Lakini tunaamini pia kwamba, viongozi na wananchi wa nchi za Kenya na Uganda nao watapaswa kuyahakiki, kuyatafakari na kuyafanyia kazi mapendekezo ya Watanzania yaliyo ndani ya mataifa yao ambayo kimsingi ndiyo yaliyochangia sana kukataliwa kwa uharakishwaji wa mchakato mzima.

Tunasema tukijua kwamba, wengi miongoni mwa wananchi waliotoa maoni yao ya kulikataa shirikisho, walifanya hivyo kwa kutoa hoja nyingi tu ambazo zilikuwa zikielekezwa kwa nchi hizo mbili jirani.

Hivyo hivyo kwetu, Watanzania na sisi tutapaswa kuhakiki, kutafakari na kufanyia kazi mapendekezo yatakayotolewa na wenzetu wa Uganda na Kenya katika kamati zao, hususan yale yanayotuhusu sisi ili kumaliza tofauti zetu na hatimaye siku itakapowadia shirikisho liweze kuundwa kwa wakati wake.

Tunaandika hivyo huku nyuma yetu tukitambua kuwa, msimamo wa miaka mingi ya Watanzania ni kukubali kuwa Shirikisho la Afrika Mashariki na lile la Afrika ndilo ajenda kuu ya mwanzo na kwamba kile kinachogomba hapa si hicho bali wakati na namna ya kufika huko.

Post a comment about this blog
Add comment
Comments


Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
No popular authors found.