Seriakali imesisitiza kuwa, amri ya uingizaji nchini nyama ya kuku bado iko pale pale kwa lengo la kuzuia ugonjwa wa mafua ya ndege kuingia nchini.
Kauli hiyo ilitolewa juzi jioni na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk. Shukuru Kawambwa alipokutana na Kamishna wa Jumuiya ya Afrika ya Uchumi na Kilimo, Bi. Rosebud Kurwijila.
Bi. Kurwijila alimtembelea Waziri Dk. Kawambwa ofisini kwake.
Dk. Kawambwa alisema baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wakiomba kuondoa vikwazo hivyo ili waingize kuku kwa ajili ya mayai, kuangua vifaranga na nyama.
’’Tutaendelea na vikwazo hivyo hadi pale tutakapoona kuwa hakuna wasiwasi wa ugonjwa huo kuingia hapa nchini,’’alisisitiza.
Alisema katika jitihada za kupambana na ugonjwa huo usiingie nchini, serikali inafuatilia mwenendo wake pamoja na kuihamasisha jamii jinsi ya kujiepusha nao na kuwa na mpango wa kitaifa wa kuudhibiti.
Aidha, alisema Tanzania imepewa msaada wa dola za Kimarekani milioni 29.6 kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo.
Alifafanua kuwa, kati ya kiasi hicho cha fedha, dola milioni 25 zinabaki Tanzania Bara na nyingine milioni 4.6 zitapelekwa Zanzibar.
Naye Bi. Kurwijila aliiomba Tanzania kushiriki katika Mkutano Mkuu utakaofanyika Addis Ababa Novemba, mwaka huu.
Alisema madhumuni ya mkutano huo ni kuhamasisha uchangiaji wa fedha kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya milipuko yanyoenezwa na ndorobo na mafua ya ndege.
Alisema hiyo ni kampeni ya kutokomeza magonjwa ya milipuko ya mifugo katika bara la Afrika.
Aidha, ?Bi. Kurwijila alisema anafurahi kuona Tanzania ni miongoni mwa nchi ulimwenguni ambazo zimefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa sotoka.