Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Bw Mahmoud Thabit Kombo, amemtuhumu mbunge wa Jimbo la Mpendae kuwa ni kikwazo cha maendeleo kwenye Jimbo hilo.
Akizungumza na Nipashe jana, Waziri Kombo alimtaja mbunge huyo kuwa ni Bw. Issa Kassim Issa (CCM), na kwamba kila mara amekuwa kikwazo cha maendeleo jimboni hapo kwa kutoshirikiana na wananchi wake.
’’Huyu mbunge hana ushirikiano na wananchi wa jimbo lake? Amekuwa kikwazo cha maendeleo kwa kutoa ahadi hewa zisizotekelezeka,’’ alisema Waziri Kombo.
Kauli ya Naibu Waziri Kombo kumlaumu mbunge huyo, imekuja kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wanachama wa Ushirika wa Maendeleo ya Kinamama katika Jimbo hilo.
Wanawake hao walimlalamikia Mbunge Issa kwa kushindwa kuwapa Sh. 250,000 alizowaahidi katika kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita.
Alisema japokuwa yeye si mwanachama wa kikundi cha wanawake hao, anaona uchungu jinsi mbunge Issa anavyowazungusha kwa kutotimiza ahadi aliyowapa.
’’Kweli mbunge huyo anazorotesha maendeleo katika jimbo letu,’’ alisema Waziri Kombo.
Alipoulizwa juu ya shutuma hizo, Bw. Issa alisema nia yake ya kuwasaidia wananchi bado ipo pale pale, kinyume na madai ya baadhi ya wakazi wa jimbo hilo.
’’Ahadi yangu bado ipo pale pale na sababu ya kutotimiza ahadi niliyoahidi ni siri yangu binafsi, wala haina haja ya kutangazwa katika vyombo vya habari,’’ alisema mbunge Issa.
Aidha alisema Ushirika wa wanawake unatumiwa vibaya na baadhi ya wanasiasa wasiomtakia heri ndiyo maana wanaongea mambo wasiyoyajua.
Ushirika huo, unashughulika na kilimo cha umwagiliaji, biashara ndogo ndogo na ukodishaji wa vifaa katika shughuli mbali mbali za utamaduni na jamii.