FAMILIA nane za wapangaji zilizoondolewa kwa nguvu kwenye nyumba na mahakama kuuamuru zirudi ndani bado zinasota nje.
Wapangaji hao walitimuliwa Jumatano iliyopita katika nyumba namba 30 mtaa wa Nzasa, Ilala, Dar es Salaam hazijaingia ndani pamoja na uamuzi wa Mahakama ya Ardhi na Nyumba kutoa hati ya kuzirudisha ndani ya nyumba hiyo.
Hati ya kuzirudisha ndani familia hizo ilitolewa juzi na Mahakama ya Ardhi na Nyumba ya wilaya ya Temeke lakini ilishindikana kuingia ndani baada ya kudaiwa kuwa polisi hawakuarifiwa kazi ya kuhakiki mali zao na kuwarudisha kwenye nyumba jambo ambalo hata jana halikufanyika.
Mwandishi wa habari hii alipofika katika nyumba hiyo jana alasiri aliambiwa kuwa Mahakama ya Ardhi na Nyumba imeamua kuwatumia madalali wake ili kuifanya kazi ya kuhakiki mali za wapangaji haoo leo bila kuwatumia polisi kwa maelezo kwamba hati hiyo inatosha kutekelezwa bila hata kuwatumia polisi.
Wapangaji hao walionekana jana saa 9.30 alasiri wakizungumza na mmoja kati ya madalali hao waliofika katika Mtaa huo wakiwa na gari ndogo na baadaye ilielezwa kuwa walikubaliana kuifanya kazi hiyo leo asubuhi wakiwa na hati ya Mahakama ya Ardhi na Nyumba ya Ilala.
Mpangaji mmoja alisema kwamba utaratibu wa kuwarejesha ulikuwa ufanyike jana lakini ilionekana kuwa ungeweza kuendelea hadi usiku kutokana na utaratibu wa kuhakiki mali za wapangaji kuonekana ungechukua muda mrefu na kuamiliwa kazi hiyo ifanyike leo.
Wakati wapangaji hao wakiendelea na mazungumzo hayo, askari wa kampuni binafsi ya Ulinzi ya Mbelwa 05 ya jijini Dar es Salaam walisikika wakisema kwamba hawatakuwa tayari kupokea hati ya mahakama yoyote zaidi ya amri ya mwenye nyumba aliyewaweka hapo.
Walidai kwamba hatua hiyo inafuatia kuwekwa katika lindo na mtu aliyenunua nyumba na kwamba wasingekuwa tayari kumruhusu mtu wala mamlaka nyingine yoyote kuifungua nyumba hiyo.
Baadhi ya wapangaji walisema hawana nguo za kubadilisha kutokana na milango ya vyumba vyao kufungwa isitoshe ulinzi uliowekwa hauwaruhusu kuvigusa vifaa vyao vilivyowekwa nje.
"Unatuona hivi tulivyo hatuna nguo nyingine za kubadilisha labda tununue mitumba na kuihifadhi kwenye viloba, tunateseka sana unawaona watoto hawa wadogo wanaumwa na mbu wanapigwa na jua, baridi na hatujui hatma yetu itakuwaje"alisema mpangaji mmoja.
Uamuzi wa kuwaondoa wapangaji hao kwa nguvu ulifanyika Jumatano wiki iliyopita baada ya nyumba hiyo kununuliwa na mtu aliyefahamika kwa jina la Mpemba aliyewaondoa kwa amri ya Mahakama ya Mwanzo bila kuwapa notisi.
Kutoka gazeti la Uhuru
ISSN 0876-3896 NA.19318
Na Mbazigwa Hassan