MAJAMBAZI wawili, mmoja akiwa na bastola, wamenusurika kifo kutokana na kipigo, na mwingine baada ya kuruka toka ghorofa ya tatu katika jengo lililopo kona ya Mtaa wa Nkrumah na Uhuru eneo la Mnara wa Saa baada ya jaribio lao la ujambazi kushindikana, Dar es Salaam, jana.
Sakata hilo la namna yake lilitokea asubuhi wakati watu wakiwa katika shughuli zao za kawaida, ndipo wapitia njia waliposikia kelele za kuomba msaada zikitoka ghorofani na wakiwa hawana hili wala lile, wakashtukia mtu anaanguka kutoka juu ghorofani na kushindwa kuinuka.
“Tulisikia kelele za kuomba msaada na tukiwa hatujui kitu gani kinaendelea, tukaona mtu anadondoka toka ghorofa ya tatu kwa kupitia dirishani kisha anashindwa kunyanyuka,” alisema mtu aliyeshuhudia tukio hilo.
Alibainisha kuwa, wakati mtu huyo anajizoa zoa kutaka kunyanyuka, wakaendelea kusikia kelele kutoka ghorofani zinazoomba msaada ndipo wapita njia na watu wengine wakabaini aliyedondoka ni jambazi, wakaanza kumpa kipigo.
Wakati wakiendelea kumkung’uta mtuhumiwa huyo, watu waliokimbilia juu kutoa msaada wakashuka huku wakimpa kipigo mtuhumiwa wa pili ambaye ilibainika baadaye kuwa alitaka kukimbia baada ya jaribio kushindikana, kwa kutumia ngazi.
“Mmoja aliamua atumie njia ya mkato kwa kuruka kutoka ghorofani ndio yakamkuta aliyokutana nayo na mwezake alibambwa wakati akijaribu kutoroka kwa kutumia ngazi,” alisema mmoja wa walioshuhudia.
Mwanamke aliyeingiliwa na majambazi hao, aliyejitambulisha kwa jina moja la Gulzar, akizungumza kwa wasiwasi mara baada ya tukio, alisema kuwa aliingiliwa na majambazi hayo, wakamfunga kamba mfanyakazi wake, huku mmoja akimtishia kwa bastola na kabla hajajua afanye nini, alipigwa ngumi ya uso hivyo kuamua kupiga kelele za kuomba msaada.
Polisi walifika muda mfupi baadaye na kuwanusuru majambazi hayo na kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira na walipopekuliwa mbali ya bastola, walikutwa na hirizi na pia walikuwa na chale walizochanjwa tumboni ambazo zinahusishwa na masuala ya ushirikina.
Mwanamke huyo aliyevamiwa alikimbizwa hospitalini kwa matibabu zaidi baada ya kulalamika kuwa anasikia maumivu makali usoni.
Kamanda wa Polisi Kanda ya Ilala, Masindoki Masindoki hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo.