SERIKALI imetakiwa kuangalia upya uwezekano wa kutoa udhamini pamoja na mikopo kwa wanafunzi wa stashahada na shahada za juu katika vyuo vikuu nchini, ili iwe na uhakika wa kuwa na wataalamu wake watakaochangia kupunguza umasikini nchini.
Hayo yalielezwa jana katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam na wanafunzi wa stashahada na shahada za juu waliokosa udhamini katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Udhamini huo hutolewa na Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, lakini kwa sasa, ni wanafunzi wa stashahada na shahada ya kwanza ndio wanaonufaika na mikopo hiyo. Bodi, imetangaza kuondoa udhamini na mikopo kwa wanafunzi wa shahada za juu kuanzia mwaka wa masomo 2006/2007.
Katika taarifa yao iliyosomwa na Bilhuda Shirima kwa niaba ya kamati ya wanafunzi zaidi ya 130 walioingia katika mtego wa Bodi ya Mikopo, ilieleza kuwa suala la mikopo kwa wanafunzi hao linapaswa kuangaliwa upya, kwani linaweza kuleta athari kubwa kwa nchi katika siku za usoni.
Mbali ya kuelezea hofu ya kuminywa katika soko la ajira katika Jumuiya ya Afrika Mashariki inayokusudiwa kuundwa ikiunganisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, wasomi hao pia walielezea hofu yao juu ya hatima ya elimu ya juu nchini.
“Ikumbukwe nchi jirani kupitia mifumo yao ya bodi za mikopo kwa wanafunzi zinasisitiza wanafunzi wa shahada za juu kukopa kwa lengo la kupata wataalamu wengi zaidi katika kada mbalimbali.
“Tanzania isipofuata mfumo huo, itaachwa nyuma na kitakachotokea ni kuona wataalamu wakiletwa kutoka nchi hizo na nyingine za nje kufanya kazi ambazo Watanzania wanaweza kuzifanya endapo watasomeshwa,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Ulitolewa mfano wa tatizo la wawekezaji nchini kudai kukosa wataalamu ndani ya nchi pindi wanapokuja kuwekeza, hivyo kutumia mwanya huo kuajiri wataalamu kutoka nchi za nje.
Kuhusu hatima ya elimu ya juu katika siku za usoni, wasomi hao walielezea hofu ya vyuo vya Tanzania kutawaliwa na wahadhiri wageni, kwani Watanzania walio wengi watashindwa kustahili kwa kazi hiyo kutokana na kunyimwa fursa ya kusoma kwa kukosa mikopo au udhamini.
“Licha ya kufundisha katika vyuo vikuu, kwa kuandaliwa sasa, sisi na wengine wa stashahada na shahada za juu, tuna nafasi ya kuisaidia nchi katika programu kama za MKUKUTA, MKUKUZA na MKURABITA, kwani watalaamu wa fani mbalimbali, watafiti na kadhalika, watapatikana kwa kusoma.
“Dira ya Wizara ya Elimu ya Juu ni kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye misingi imara ya kuifanya kuwa mshindani katika nyanja za elimu ya juu, sayansi na teknolojia. Pia dhima ya serikali ni kuwezesha upatikanaji wa nguvu kazi yenye uwezo wa kutumia rasilimali zilizopo ili kujiletea maendeleo.
“Je, serikali kupitia Wizara ya Elimu ya Juu ina maana wao hawalitambui hili? Au ni propaganda zinazoandikwa tu kwenye sera? Na kama wanalitambua, kwa nini wameondoa mikopo kwa ngazi za stahahada na shahada za juu? Au haitambui kama sisi ni rasilimiali inayotakiwa kuwezeshwa na kuendelezwa ili kusaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo?” ilihoji sehemu ya taarifa hiyo ya kurasa tano