Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Lowassa akataa taarifa ya DC
Lowassa akataa taarifa ya DC
By Habari Tanzania | Published  09/15/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Mwandishi Wetu, Kigoma

WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, jana aliikataa taarifa ya Wilaya ya Kigoma kwa madai kuwa imepitwa na wakati.

Lowassa alikataa kusikiliza taarifa hiyo wakati Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo, John Mongella alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi ya wilaya yake.

Huku akionekana kuchoshwa na taarifa zenye upungufu, Waziri Lowassa alimkatisha mkuu wa wilaya hiyo na kumtaka aache kuisoma huku akimlaumu Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Martin Mgongorwa kwa kutomsaidia DC huyo mpya kuandaa taarifa inayokwenda na wakati.

“Hii taarifa yako imepitwa na wakati, RAS uko hapa siku nyingi, lakini umeshindwa kumsaidia DC wako kuwa na taarifa nzuri. Naona tuishie hapo, tuendelee na ziara,” alisema Waziri Lowassa na kusimama.

Juzi, akiwa katika Wilaya ya Kibondo, Waziri Lowassa alimbana Mkuu wa Wilaya hiyo, Joseph Mzurikwao baada ya kutoridhishwa na taarifa ya wilaya hiyo hasa katika mkakati wake wa kutaka kukuza kilimo.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Lowassa, alimtaka DC huyo kufanya kazi kwa kuzingatia semina waliyoipata Ngurdoto, Arusha baada ya kubaini kuwa mambo mengi waliyokubaliana katika semina hiyo hayajaanza kutekelezwa.

Wakati huohuo, Waziri Lowassa ameagiza Wizara ya Miundombinu kuanza ujenzi wa daraja la Kijiji cha Kibilizi, lililopo katika Kata ya Gungu, Kigoma.

Alitoa agizo hilo baada ya mwananchi mmoja, Peter Almas kutoa kero wanayoipata wananchi hao kwa kukosa daraja hilo kwa miaka mitatu sasa.

Wakati akiwasilisha kero hiyo mbele ya Waziri Lowassa, wananchi wote walipiga kelele za kumuunga mkono, hali iliyomfanya Waziri Lowassa kutoa agizo la kuanza ujenzi huo mara moja.

“Kilio cha daraja la Kibilizi nimekisikia, na serikali kuanzia wiki ijayo itaanza ujenzi wa daraja hilo mara moja,” alisema.

Mbali ya kutoa agizo hilo, Waziri Lowassa pia alitoa mchango wa sh milioni nne kwa ajili ya SACCOS ya Nyakage na Kino. Kila SACCOS imepata sh milioni mbili.

Katika hatua nyingine, Waziri Lowassa amemuagiza Waziri wa Maji, Stephen Wassira kumpelekea orodha ya taasisi za serikali zinazodaiwa ankara za maji.

Alisema anataka aletewe orodha ya taasisi na mashirika hayo ya serikali ifikapo mwisho wa mwezi huu na kwamba lazima madeni hayo yalipwe.

Alitoa agizo hilo alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Mamlaka za Majisafi na Majitaka Mijini, unaofanyika katika Hoteli ya Hiltop, Kigoma.

Alisema mamlaka za maji zinajiendesha kibiashara na ili zijiendeshe zinahitaji kulipwa, na kusisitiza kuwa wadeni hao na wengine lazima walipe madeni yao kwa wakati.

Alitoa agizo hilo baada ya Waziri Wassira kusema kuwa hadi Juni mwaka huu, mamlaka za maji zilikuwa zinadai sh bilioni 3 na kati ya fedha hizo taasisi na mashirika ya umma yalikuwa yakidaiwa sh bilioni 1.3.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.