Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Nthelezi Nesaa  »  Serikali inamaanisha nini?
Serikali inamaanisha nini?
By Nthelezi Nesaa | Published  09/14/2006 | Nthelezi Nesaa | Rating:
Na Mwanahabari wa HabariTanzania.com, Canada.
Safu hii inaandika ikiwa na majanzi na simanzi ikishangaa hata kukerwa ni kwanini wananchi wanapata mateso na serikali ikiikalia kimya TANESCO.
 
 Hii ni kutokana na jinai itokanayo na mgao wa umeme unaondelea hapo nchini kwetu.
 
 Hakuna haja ya kutafuna maneno bali kusema kuwa huu ni uzembe na hujuma kwa kwa taifa ambalo mgao unalitia taifa letu msambweni.
 
 Kabla hata vumbi la madhara na mateso ya mgao halijatua, serikali inakuja na mpya kuwa ina mpango wa kuiweka TANESCO tena chini ya kampuni nyingine ya kigeni! Hii ni baada ya Net Group Problems iliyoletwa na shemeji za wakubwa kufanya kazi "nzuri" hadi kunyimwa kuendelea na tenda ya ulaji wa wadanganyika.
 
 Kwanza tuseme wazi kuwa huu ni upuuzi na ni kuendelea kufanya ambayo serikali ya awamu ya nne hakutegemea kufanya.
 Kwanini?
 
 Kwanza , sababu zinazotolewa kuwa menejimenti ya kigeni ina uwezo wa kukusanya madeni toka kwenye taasisi ni upuuzi. Kwanini? Kwa sababu suala la kukusanya madeni toka mikononi mwa asasi za umma na serikali ikiwemo, halihitaji mgeni au mwenyeji bali makali yatokanayo na sheria. Kwa taarifa ya serikali hata mtoto wa miaka kumi akipewa makali kisheria anaweza kukusanya hayo madeni. Hilo moja.
 
 Kama ni kweli kuwa menejimenti ya kigeni ndiyo yenye kuweza kukusanya madeni mbona sasa Net Group Problems inafurushwa? Hapa nani anamdanganya nani?
 
 Kama menejimenti ya kigeni inafaa, basi ni kwa kufungulia maji kupita kiwango na kuacha nyuma mgao.
 
 Pili ni upuuzi kuleta menejimenti nyingine ya kigeni. Je serikali haikujifunza kutokana na kufanya vibaya na kutia aibu kwa Net Group? Ajabu serikali hiyo hiyo inayotushawishi kuona mantiki kwenye utumbo huu haitwambii Net Group ambayo ni menejimenti ya kigeni imekusanya kiasi gani ukilinganisha na kabla ya hapa na chini ya sheria zipi mtawalia.
 
 Jakaya uko wapi hapa? Je haya yanaweza kufanywa na serikali yako! Au nawe umeanza kunywa kwenye kombe la ulevi alilonywea mtangulizi wako akaahidi kupambana na rushwa akaishia kuipamba na kuisimika? Kama hujui basi elewa kuwa hii ni hujuma dhidi yako na wananchi wako. Ajabu na aibu.
 
 Tungedhani kuwa kama menejimenti ya kigeni ndiyo muarobaini basi Net Group ingeendelea na kazi. Hilo tuliache.
 
 Je kazi ya menejimenti ni kukusanya madeni tu au kuendesha shirika kama vile kutoa huduma ambayo kwa sasa tunaambiwa ni bomu. Pia kazi nyingine ni kubuni sera ndogo ndogo na kubwa,mipango ya muda mfupi na mrefu na mengine kama hayo vya kuboresha ufanisi wa shirika na mengine kama hayo?
 
 Tunadhani serikali yaa awamu ya nne inaanza “kulikoroga” bila kujua. Kama kuna washauri wanaoihadaa ifanye jinai hii,inabidi waangaliwe kwa makini hata kuonyeshwa mlango wa kutokea maana wako mahali wasipostahili kwa muda usiostahili kama kweli azma ya serikali ya awamu ya nne bado ni ile ile kutoturudisha nyuma.
 
 Ila hatushangai sana tukizingatia kuwa waliofanya mauza uza haya bado wamepewa nyidhifa nyeti kama uwaziri na kadhalika. Kwani hatuwajui hata kwa sura na majina hata majumba yao maeneo ya Mbezi,Kunduchi na kwingineko? Hapa nani anamfanya mwenzake mpumbavu?
 
 Kinachotaka kufanywa na serikali tunaweza kusema ni kosa kubwa kuliko hata awamu ya tatu. Kwanini? Kwa sababu serikali ya awamu ya nne inataka kurudia kosa lile lile lililofanywa na serikali tangulizi kwa mara ya kwanza. Na yote haya yalitokea kutokana na tabia ya “Bwana mkubwa sana” Benjamin William Mkapa kutoambilika na urushi.
 
 Pia serikali inataka kuwaonyesha wananchi kuwa ni kichwa ngumu tena zuzu lisilojifunza tokana na hata ukweli wa jana ambao hata simulizi zake hazijaisha.
 
 Tunaambiwa hata kuna sakata la kununua hisa za ATCL na kutaka liendelee kuendeshwa na wageni waliolifikisha hapo lilipo hadi serikali ikabidi ifanye abracadabra ya kulinunua. Anywa hili lina makala yake inshallah.
 
 Au tuseme kila serikali itakayokuwa ikiingia madarakani lazima ilete makampuni yake toka nje? Au ni kwa vile mara nyingi makampuni haya huletwa na watu walio karibu na chungu cha madaraka (Powerhouse)? Nani mara hii hakushangaa kuwa Net Group ililetwa na mashemeji wa aliyekuwa mwenye nchi huku mmojawapo wa wakurugenzi wa kampuni lililowaleta akiwa anasoma shule ya msingi?
 
 Je hii haiwezi kufanya watu wadhanie kuwa na awamu ya nne inafanya hivyo ili baadhi ya wateule wapate ulaji laini? Waingereza hujisemea "Monkey see monkey do." Tusingetaka ieleweke hivyo wala serikali kukaribisha mazingira ya kufanya iwe na kueleweka hivyo vinginevyo kwa hatua inayotarajiwa kuchukuliwa na serikali kuleta balaa, jingine ingetolewa maelezo na ufafanuzi wa kina.
 
 Je na bunge letu nalo litakubali kutenda jinai hii? Kulikoni? Tuambiane maana mambo ya bongo wakati mwingine huenda kibongo bongo. Au zile shutuma kuwa bunge la sasa ni la “Ndiyo mzee’ zinaanza kuonyesha ukweli? Au tuseme kwa kujua uoza na tabia hii ya bunge letu ndiyo maana gazeti moja la uchafu liliamua kuwatolea ya mwaka kwa kuwalinganisha na mbwa koko tena kusiri?
 
 Kama Net Group imethibitika kuwa zigo na hasara kwa mlipa kodi,serikali inabidi itwambie ni miujiza gani hilo Kampuni jingine litakaloletwa litafanya. Au ni ule mchezo wa “mbwa ni mbwa hata kama ni wa kizungu”? Isije hilo kampuni litakaloletwa ni Net Group iliyobadilisha jina? Hizo ni shaka zetu.
 
 Yaani Tanzania na ujabali wake wote inashindwa kudai madeni yake! Leo TANESCO inahitaji kampuni la kigeni kudai madeni! Kesho mamlaka za maji nazo ziende nje kusaka makampuni ya kudai madeni! Serikali za mitaa kadhalika! Tunapelekwa wapi? Tukubali kuwa kuna siku hata serikali itabidi iende huko huko kutafuta mgombea urais anayeweza kumeneji nchi yetu maana inaonekana imetushinda. Tungepewa maelezo.
 
 Kabla ya kwenda mbali lazima tuonye kuwa kashfa nyingi za mashirika ya serikali zimeanza kupita bila kuandikwa kutokana na mashirika kutishia kuvinyima matangazo vyombo vya habari vitakavyoyaandika "vibaya". Sasa tunaenda wapi kama hata taaluma ya habari "imeingiliwa" kiasi cha kujigeuza changudoa anayengojea mshiko toka kwa washitiri wake ambao ni wabadhilifu tena wakubwa na wanaonuka?
 
 The media must be told to their face, "Stop going to bed with the devil" Heri kufa kwa njaa ukiwa na heshima yako kuliko kuishi na shibe ukiwa malaya wa kawaida tu.
 Turejee kwenye sakata letu.
 
 Ajabu ya kichwa ngumu ya serikali hata TANESCO, safu hii na wachambuzi wengine wanapotoa shutuma,inakaa kimya wala haitishwi. Hii imekuwa ndiyo uficho na chanzo cha ubadhilifu kwani kukaa kimya mara nyingine kunaweza kuchukuliwa kama kukubali shutuma. Wasomaji wa mtandao huu watatuhukumu. Tunajua TANESCO hata serikali zina watu wake wanaousoma. Ajabu ya maajabu ni kwamba hawatajishughulisha na kujibu tuhuma hizi. Kwani wanawajibika kwa nani? Lakini watawala na watu wao wanasahau kuwa vyombo vya habari ndiyo sauti ya umma. Vox populi vox dei hata The voice of voiceless.
 
 Pia kukaa kimya ni njia ya kuficha aibu na kuwafanya watu wasahau ukichukulia kuwa wananchi wetu wengi wamejengewa mfumo wa maisha wenye kuwahangaisha sana kiasi cha kutokuwa na muda wa kufanya mambo mengine. Anayetaka kujua tunachomaanisha hapa,arejee salamu za watanzania walio wengi. Ukimuuliza hujambo atakwambia anashukuru kumekucha wacha akatafute hela ya kula. Huyu maskini hana mawazo na hela ya kujenga,kusomesha watoto,kustarehe wala kuweka benki.
 Kwa wale wasioridhika na jinai hii wanadiriki kuzamia meli na kwenda wasikojua hadi wengi wao kupoteza maisha.
 
 Serikali kwa kujua hilo huamua kunyamaza ili waathirika hawa wasahau kirahisi. Ukitaka kujua hili. Fuatilia mgawo wa umeme. Utakuta unawaadhiri watu maskini huku watawala wakipa umeme wao kama kawaida. Je kuna anayelalamika? Ajabu utasikia vikundi vya watu fulani wakianikiza wanataka wafanye maandamano kulaani mashambulizi ya Israel na Lebanon ili hali kwao kunawaka moto! Hivi nani kawaroga nyie?
 
 Serikali haitaki kujibu swali kuu la msingi kuwa , kwanini nchi yenye vyanzo vingi vya nishati na mtandao mzuri wa nishati na iliyopata mvua ya kutosha, ina mgawo wa umeme wakati nchi kama Kenya iliyobanguliwa na jangwa na yenye kutokuwa na vyanzo haina? Haitaki kutoa maelezo kwa vile inajua haitakuwa na maelezo yanayoiingia akilini.
 
 Na ni kutokana na tabia hii ya kukaa kimya inayofanya wachambuzi waanze kuhoji udhati na umakini wake. Hulka hii ndiyo inafanya watu waanze kuona kuwa wana mvinyo ule ule kwenye chupa mpya tena yenye umri karibu na ile tuliyoivunja juzi.
 
 Ni kwa hulka hii watu wanaanza kuona kama nchi zetu zinafanyiwa usanii na kiini macho kwenye kila uchaguzi. Kwani hazitoi matokeo yenye kuweza kuleta kile tulichotarajia. Mkapa aliahidi kupambana na rushwa akaibariki. Kikwete ameahidi kuwaletea maendeleo wananchi lakini kama upuuzi wenyewe ni huu atayaleta kwenye kile wataalamu huita kuendelea katika kutokuendelea ua development into underdevelopment.
 
 Hulka hii ndiyo inafanya kuona kuwa wanasiasa siyo watu wa kuamini kwani ahadi zilizotolewa na watawala wetu wapya zilituaminisha kuwa wangeonyesha tofauti.
 Umma hauli maneno hata kama ni mashairi yaliyotiwa nakshi na utuli. Bahati yao kuwa watu wetu wanaishi kwenye nchi waliyopewa na mungu kama hisani! Mungu pisha mbali gonjwa hili la unyafuzi na ukondoo unaotakana na utapiamlo wa kimawazo kwa pande zote yaani wananchi na watawala wao.
 
 Yako wapi? Huwezi ukaamini kuwa mambo yanayotaka kufanywa na serikali hii yanaweza hata kujaribiwa kuingizwa kwenye mawazo na serikali ya awamu ya nne ambayo kwa kiasi kikubwa karata yake ya kuingia madarakani ilikuwa ni utegemezi juu ya mvuto wa mtu badala ya sera. Huenda kwa vile bado wahusika wanazo sura nzuri zao, wahofie nini? Hata zikianza kuchakaa si watatia mkorogo na kufanya plastic surgery na mambo yanaenda tu. Nani kasahau kuwa wale baba wa taifa na mwana mzalendo wa nchi hii,Julius Kambarage Nyerere aliowaambia kuwa wamejilimibizia mali za wizi eti leo ndiyo vinara! Another gibberish and abracadabra.
 
 Je wananchi walitegemea kula mvuto wa mtu au kupata maendeleo waliyoainisha kwenye kuchagua sera tofauti za vyama tofauti vya siasa vilivyogombea uchaguzi wakati ule. Kosa la kufanya mambo kwa falsafa ya pesa ya kula linaanza kujitokeza tena kwa kasi mpya,nguvu mpya na ari mpya.Kalagabaho.
 
 Wahusika tungewasihi sana . Msifanye wananchi waanze kuzomewa na wale waliowaonya kuwa vigezo vinavyofuatwa kupata madaraka ni dhaifu hasa vinapo kuwa ni sura na mvuto wa mtu. Serikali isivuruge mvuto wa Rais wetu kwa kuanza kuchungulia kusikochungulika.
 
 Imebidi tuanze kuambizana ukweli baada ya kuona kuwa sasa mchezo unaaza kuwa ule ule ,janja ya nyani na danganya toto.
 
 Je wananchi wataendelea kukubali uzezeta na ulimpyoto kila baada ya miaka kumi? Je tatizo la wananchi wetu ni nini? Au nao wana tatizo la kutojifunza kutokana na matukio kama inavyotaka kuonyeshwa na watawala wao?
 
 Huwezi kujua, jamii mbovu huzaa na kuchagua viongozi wabovu. Na viongozi wabovu lazima wafanye mambo mabovu kama kurudia makosa.
 Safu hii haiamini kuwa mwongo huu watanzania wamechagua viongozi wachovu na wabovu. Tumalizie kwa kumuelekezea ndugu yetu Rais wetu Jakaya Kikwete salaam zake. Kaka huu ni mzigo wako. Likibirinduka utakuwa na sifa chafu kama zinazowaandama waliokutangulia wakabinafsisha nchi yetu na watu wake kijambazi. Time will surely tell. Yetu masikio na macho

 Tunangojea maelezo utetezi na vitendo dhidi ya shutuma na ushauri huu.
 Kuzidi kutuletea mikampuni ya kigeni hakuna tofauti na ubinafsishaji wa kijambazi.Tutaendelea kutegemea wageni hadi lini? Ajabu pamoja na mchungaji Christopher Mtikila kuonya juu ya magabacholi wanaodhulumu hata biashara ya kuuza juisi pale Tandamti,sasa mnaleta magabacholi wa kulangua roho zetu.AIBU.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by J. Mwaitekete)
    Rating
    Haya ndiyo maneno ya kusoma na kuzingatia. Kikwete anaanza kutuboa maana ni ukweli kuwa huyu mjamaa hana jipya . yeye ni mwana ccm na alikuwapo kwenye cabinet wakati wakibinafsisha na kuitoa sadaka nchi yetu.
    Mwandishi kathubutu angalua kusema ukweli jambo linalowashinda wabongo. kisa hasa ni njaa maana huwezi kuamini kuwa magazeti kama rai yananunuliwa na magabacholi unategemea yataandika lolote dhidi ya Kikwete. Tunajua kuwa mmojawapo wa marafiki wa karibu wa Kikwete ndiye aliyebinafsishiwa habari corp. Kusema ukweli makala hii imenichengua na muzidi kutupa vitu zaidi zaidi.
    Mungu ibariki habaritanzania
    mungu wabariki waandishi wake
    mungu waongezee maarifa na uthubutu
    mungu walaani wevi wetu kwenye kila idara
    aamin
     
  • Comment #2 (Posted by ubwa said)
    Rating
    Kweli serikali inabidi ifanye mambo muhimu badala ya danganya toto
    wonderful comment generally
    US
     
  • Comment #3 (Posted by Steven)
    Rating
    This is an excellent article. It is an eye opener to all those who love this country. Tanzanians are not poor but we are made to believe that we are poor by our leaders. There are two things we as Tanzanians should do. one is to agree to break the culture of silence. No single Tanzanian even a small child who does not realise that our leaders are cheating us in almost all aspects of life. To be precise, it is not only government leadres but also our religious leaders who have accumulated more than they need by using the sewat of the poor. We see it but we are afraid to tell them that we see and know what they are doing. Two, is Tanzanians should develop the habit of loving work ad develop innovation, creativity and accountability. We are being silenced because we are poor. We are poor because we are made to believe we are poor. What we need to do is to work very hard, get wealth and as wealth is power we shall be able to challenge the oppressing system.

    Well done,

    Steven
     
  • Comment #4 (Posted by Kessy JS)
    Rating
    Inauma sana nikisoma vitu kama hivi, kwani ningekuwa na uwezo wa kui distribute hii article kwa wa - danganyika wote ama ingekuwa kiama.

    Good job ,

    Kessy.
     
  • Comment #5 (Posted by SINGO G SINGO)
    Rating
    Huu ndio ukweli na uwazi,makala kama hii inapasa kuandikwa mahali mwananchi wa kawaida anapoweza kuisoma.Tunahitaji wazalendo wengi wa aina hii!!!!!!
     
Submit Comment


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.