Wawalaghai wafanyabiashara, watoweka na watoto yatima
Na Rashid Mussa, Mtwara
WATU watatu wanaosadikiwa kuwa raia wa kigeni na matapeli wamewalaghai wakazi na wafanyabiashara kadhaa wa mjini Mtwara na kutoweka na watoto yatima.
Habari zilizopatikana hapa zinasema kuwa watu hao wasiofahamika raia wa nje wameutikisa mji wa Mtwara kwa kufanya udanganyifu mkubwa na kufanikiwa kujipatia watoto yatima, fedha, huduma za hoteli na usafiri kutoka kwa watu mbalimbali mashuhuri mjini hapa.
Kwa mujibu wa waumini wa kanisa moja kubwa la Kiroho mjini hapa, watu hao ambao mmoja anajiita Trojca Sesulu raia wa Afrika Kusini alijitambulisha kuwa ndiye mkurugenzi wa shirika hilo akiwa na mkewe na mwenzao aliyetambulishwa kuwa mchungaji waliingia mjini hapa na kupokelewa na uongozi wa kanisa hilo zaidi ya wiki mbili zilizopita.
Kwa mujibu wa habari kutoka vyanzo mbalimbali, watu hao ambao majina yao hayajathibitishwa, waliingia mjini hapa takriban wiki mbili zilizopita wakidai ni ‘Watumishi wa Mungu’.
Walidai wanaendesha shirika moja la misaada la kusaidia yatima na wajane linalojulikana kama ‘Hope Success International’ ambalo makao makuu yake yapo nchini Marekani.
Habari zinasema baada ya utapeli, waliondoka na watoto wawili, mmoja mdogo na kufanikiwa kutoroka na gari aina ya Mitshubishi Pajero mali ya Peninsula Hotel.
Namba ya usajili ya gari ni T 926 CAN ambayo walikuwa wanaitumia kwa kuendesha wenyewe tangu walipofika hotelini hapo walipokaa kwa siku tisa.
Habari ambazo zimethibitishwa na mmiliki wa hoteli, Zawadi Hamisi maarufu kwa jina la ‘Champion’ na ambaye ameripoti tukio hilo polisi juzi, watu hao wameacha deni kubwa la huduma mbalimbali walizopatiwa kwa siku zote
Tisa walizokaa hotelini hapo.
Huduma hizo ni malazi, chakula na vinywaji walivyopatiwa pamoja na usafiri wa gari hilo kwa siku zote walizokaa na fedha taslimu zaidi ya sh. 300,000 walizochukua kwa mkopo kwa nyakati tofauti kwa madai kuwa fedha zao zilikuwa bado kutumwa kutoka Marekani.
Kutokana na utapeli wao, watu hao wameacha kilio kwa watu wengi maarufu wa mji huu waliotapeliwa fedha kati ya sh. 20,000 hadi sh. 350,000 kwa nyakati tofauti wakitumia mbinu mbalimbali za ulaghai wengine wakiahidiwa kuwasomeshea watoto ng’ambo na kuwapatia kazi.
Inadaiwa kuwa wiki ya kwanza walipoendesha ibada katika Kanisa la Kiroho na kuhubiri injili pamoja na kutangaza madhumuni ya ujio wao kuwa ni kufungua tawi la shirika hilo kubwa duniani, uongozi wa kanisa na waumini walifarijika sana na kuwapatia ushirikiano mkubwa.
Inadaiwa kuwa kuanzia hapo zilianza pilikapilika za kazi ya kuwasaka wajane na watoto yatima ambao pamoja na kuwalea pia, walidai watakaobahatika watasomeshwa Marekani.
Habari zinadai kuwa mama mmoja muumini wa kanisa hilo Sitawa Buriana Mlaponi aliwakabidhi mtoto yatima Faraja Leonard (5) na kijana mmoja aliyekuwa analelewa na kanisa ambaye jina lake halikupatikana mara moja.
Habari za watu hao waliouacha mji huu katika ‘simanzi’ kubwa na wa wengine ‘kushikana mashati’ kwa kushutumiana na kulaumiana wanadaiwa baada ya siku
kadhaa za kukaa kanisani hapo walihamia katika hoteli moja kubwa ya Peninsula kwa madai ya kuwafikia walengwa kirahisi.
Mmiliki wa hoteli ‘Champion’ alithibitisha kwa mwandishi wa habari hii jana kuwa, watu hao waliletwa katika hoteli yake wakiwa na mchungaji wa kanisa hilo ambaye ni ofisa Uhamiaji mmoja Agosti 31, mwaka huu.
Alisema walijitambulisha mmoja kuwa ni mkurugezi wa shirika hilo ambaye alipangishwa chumba cha waheshimiwa cha sh. 40,000 na mwenzie cha sh. 25,000 na kwamba wamekaa hapo hadi Septemba 9 walipotoweka.
Alisema watu hao waliondoka Jumamosi iliyopita wakiwa watu saba pamoja na watoto wawili, Ofisa Uhamiaji alikuwa anadanganywa kuwa angepelekwa kusoma Marekani na kuwa waliondoka wakiwa katika magari mawili ya kwake na waliyokuja nayo ndogo yenye namba ya usajili T116 ALZ.
Akisimulia mkasa huo, mmiliki wa Peninsula Hotel alisema watu hao ambao katika shughuli zao usingeweza kuwatilia shaka kutokana na kuwahusisha watu makini na taasisi nyeti kama polisi ambaye mmoja aliahidiwa kuwa mwakilishi wa ofisi ya Masasi waliondoka kwa kumuaga kuwa wanakwenda katika mji mdogo wa Mnazi Mmoja uliopo kilomita 80 kutoka mjini Mtwara barabara ya Mtwara kwenda Dar es Salaam na wangerudi jioni.
Hata hivyo, alianza kupata shaka juu ya watu hao ambao katika kipindi hicho walifungua ofisi ndani ya hoteli na kuendesha shughuli kama ya mikutano na semina zikigharamiwa na hoteli. Wahudhuriaji wengi walikuwa
wanawake huku wakisambaza fomu za kusajili watoto watakaosomeshwa ng’ambo.
Habari za kuaminika zilizopatikana jana zinasema watu hao wamekamatwa mjini Dar esSalaam juzi na gari lao moja lilipinduka katika kijiji cha Mkwaya karibu mji mdogo wa Mnazi Mmoja katika safari hiyo ya kutoroka na gari la Peninsula Hotel limekamatwa Kibaha mkoani Pwani.