Na Mwanahabari wa HabariTanzania.com, Canada
Katika kuangalia namna Rais Jakaya Kikwete alivyoshupalia suala la filamu ya Darwin's nightmare, mtu yeyote mwenye akili anashangaa ni kwanini Rais anapoteze muda wake na wa taifa,heshima na mengine kama hayo kujiingiza kwenye kutafuta majibu ya maswali ambayo yaliishajibiwa.
Documentary hii nzuri ilitengenezwa na mtenezaji filamu Hubert Sauper ambaye anajulikana kwa umaarufu wake kutengeneza filamu za kusisimua ili kujipatia riziki yake.
Kwanza filamu inayomuhangaisha Rais haikutengenezwa jana wala juzi. Ina muda mrefu kwani ilitengenezwa akiwa waziri wa mambo ya nchi za nje. Hivyo kama kweli alikuwa na nia ya kuitetea hadhi ya nchi yake kama anavyotaka aonekane baada ya kuwa rais, tunadhani angefanya hivyo muda mfupi baada ya filamu kutoka kwani ilikuwa kwenye eneo lake la utendaji kazi kama waziri wa mambo ya nchi za nje.
Si mpya kwa sababu baadhi ya vyombo vingi vya habari hasa magazeti vilishaelezea kilichomo humo. Hata waandishi wengi wa humo nchini wameishaandika sema kutokana na katabia kabaya ka jamii kusahau mapema machapisho,usishangae sakata hili kuonekana kama kitu kipya.
Pia ifahamike kuwa hasara au taathira inazopata Tanzania na watanzania kutokana na madhara ya kadhia hii,yavilinganishwa yale yanayosababishwa na matatizo ambayo yako ofisini mwake na asifanye kitu,tena kwa kuwauliza wananchi,tunadhani suala la documentary litaonekana kama upuuzi Fulani.
Kwa mfano sifa ya Tanzania ni nini na ina maana gani ikilinganisha na madhara yatokanayo na sera nzima ya ubinafsishaji kama ilivyotekelezwa kijambazi na kibububusa na serikali iliyopita?
Hatuoni kama Darwin's Nightmare, kwa mfano ina madhara sawa na IPTL,Net Group Problems, Makampuni ya madini yanayoipa serikali mrahaba wa asilimia tatu ilhali kwa madini kama hayo hayo Nchi kama Botswana inapata zaidi.
Hatuoni kama madhara yatokanayo na filamu hii yanaweza kulinganishwa na madhara yanayotokana na hujuma zinazofanywa na makampuni ya uwindaji na utalii huko mbugani.
Kimsingi filamu hii inaongelea sehemu ndogo ya nchi yetu tofauti na madhara tajwa hapo juu yanayoikabili nchi yetu.
Tunadhani Rais angeshughulikia masuala yanayoingia akilini mwa wananchi kwanza ya kupambana na uoza uliopita kiasi alioukuta ofisini mwake badala ya kufanya waingereza waitacho "witch-hunt and white wash"
Hatuoni madhara yatokanayo na filamu tajwa maana inachosema ni ukweli kwani kama ni kuwepo kwa unyonyaji wa kiuchumi upo pale mwanza. Nani kasahau kuwa hata zile kashfa zilizowafukuzisha kazi akina Profesa Joseph Mbilinyi, Kilontsi Mpologomyi na Dr. Juma Ngasongwa inatokea huku.
Japo siyo hoja katika mjadala huu, hata yakitakiwa maelezo kwa mfano ni kwanini wale waliokuwa wanaonekana kuwa mangapi na mizigo kwa serikali iliyopita amewarudisha maofisini tena kwenye idara nyeti, tunadhani jibu litakuwa gumu. Haya kimsingi ndiyo mambo ya maana ya kuweza kumshughulisha Rais ili awape majibu watanzania na siyo ubabe.
Ukifuatilia filamu ya The Darwin's Nightmare, utakuta kuwa mtengenezaji licha ya kuonyesha umaskini wa waswahili wa pale mwanza, alitaka mataifa makubwa ambayo ndiyo wanunuzi wakubwa wa sangara waone ni kwa kiasi gani wanachangia katika jinai hii ya umaskini kwa kununua kitu ambacho nadhani tafsiri ya haraka ni haramu.
Hapa mtengeneza filamu licha ya kuwa mkweli, alikuwa makini kutaka kuwashawishi wanunuzi wa sangara kujua ukweli kuwa hawana haja ya kutumia pesa nyingi kiasi hicho kununua kitu ambacho kimezalishwa kwa bei nafuu hata kwenye mazingira machafu.
Anayekana kuwa kilichosemwa na mtengeneza filamu si ukweli, ajiulize jina mapanki kwa mfano limetungwa na nani? Ni wananchi wenyewe. Je lina maana nzuri kiuchumi na kijamii?
Hivyo kimsingi mtengenezaji wa filamu hakuwa na nia mbaya kama watawala wetu wanavyoiangalia. Hivi kwa mfano mtu akionyesha mayatima walioko Makete na mateso wanayo yapata utasema ameidhalilisha nchi?
Juzi hapa Canada Televisheni ya CBC, usiku ilionyesha picha ya waathirka wa ukimwi huko nchini Zambia. Kwa bahati nzuri documentary hii ilitengenezwa na mtengenezaji filamu na mwandishi mashuhuri Sorius Somirwa, kutoka Afrika Magharibi.
Ni aibu na uchungu ukiangalia watu kwanza walivyo maskini na wajinga ukiachia mbali mateso wanayopewa na ukimwi. Ukiwalinganisha kwa mfano na aliyekuwa Rais wao Fredrick Chiluba, picha yao ni aibu kwa Zambia lakini ni ukweli.
Je kwa mfano wenye viwanda Mwanza hawanyonyi wananchi wanaoshughulika kwenye industry ya uvuvi?
Hilo tuache, ukija suala la umalaya. Ni kweli kuwa si jambo la kutia chuku kuwa nchini Tanzania na Kenya wanaharakati wa ukimwi wanapata kibarua kigumu kupambana na ongezeko la waathirika wa ukimwi kwenye visiwa vilivyomo kwenye ziwa Nyanza.
Visiwa vimevuta hisia za wanaharakati wa ukimwi kutokana na ukweli kuwa kuna umalaya wa kupindukia kwenye visiwa hivyo.
Filamu ikisema kuna umalaya Mwanza tunadhani siyo kutukana wala kuidhalilisha Mwanza wala Tanzania. Ni hali halisi na ni ukweli mtupu.
Hivi kwa mfano mtu akisema kuwa maeneo ya Kinondoni na Ohio jijini Dar es salaam na Kwa Macheni yanaongoza kwa vitendo vya kimalaya atakuwa anaaibisha jiji na nchi?
Je kwa mfano mtu akitoa documentary kuonyesha watanzania japo si wote, walivyopoteza utu kiasi cha kufanyia ngono kwenye makaburi ya Kinondoni bila aibu wala utu, atakuwa anaidhalilisha nchi na jiji.
Au hata mtu akitoa documentary kuonyesha ubomu wa wasomi wa kitanzania kutokana na kukithiri kwa wizi wa mitihani ataambiwa anaihujumu nchi? Ni nani anahujumu nchi kati ya yule anayetenda na yule anayeandika. Hii ni sawa na kulaumu chombo cha habari kwa kuandika uchafu wako wakati hutaki kujilaumu kwa kufanya uchafu huo.
Tunadhani Rais hapa aachane na masuala madogo ashughulikie masuala ya muhimu na nyeti kwa faida anwai ya wananchi badala ya sifa za juu juu.
Tumalizie kwa kumshauri Ndugu Rais arejee kuiangalia na kufikiria upya juu ya filamu husika,hatuna shaka ataungana nasi kuwa kinachoelezwa mle siyo uongo bali ukweli.
Kwa madai ya Mwanza kupitisha silaha, jibu la ukweli na uongo ni upi laweza kutolewa na swali fupi tu.
Je unapobinafsisha hata mamlaka za kusimamia bandari na viwanja vya ndege unategemea nini kuhusu hili?