“SASA wananchi tunanufaika na Umoja wa Soko la Mazao Masakta (USOMAMA), ukiangalia ghala letu lina hifadhi ya chakula cha kutosha na kiasi kingine tunauza nje ya wilaya yetu. Tumepata fedha iliyotusaidia kuanzisha ushirika wa kuweka na kukopa (SACCOS).”
Hii ni kauli ya Hamis Athuman Alute mkazi wa Kata ya Masakta, wilayani Hanang’, mkoani Manyara.
Alute alikuwa akielezea juu ya umoja wao waliouanzisha mwaka 2005. Umoja huo unawasaidia kupata mitaji, ajira na uhakika wa soko la mazao yao.
Alute ambaye pia ni mwenyekiti wa SACCOS hiyo anafafanua kuwa mkakati wao ni kila kata wilayani humo kuwa na SACCOS inayojihusisha na ununuzi wa mazao ya kilimo na chakula.
“Mpango huu ukitekelezwa vizuri utakuwa ni ushirika wa kuigwa nchini kote na hautakuwapo umaskini wa kipato tena katika eneo hili,” anasema.
Kunufaika na mpango huo unaoelezwa na Alute kunatokana na mipango shirikishi ya Mkoa wa Manyara unaotumia fursa na vikwazo walivyonavyo wananchi kuwafikishia huduma vijijini na kuwapa elimu na maarifa ya kutumia mazao wanayolima kuondokana na umaskini.
Kata ya Masakta ni moja ya kata za Wilaya ya Hanang’, ambazo huzalisha mahindi kwa wingi, lakini kabla ya kuanzisha umoja huo, kulikuwapo tatizo la soko la mahindi na sehemu ya kuyahifadhia.
Awali wananchi walikuwa wanauza mazao yao katika Chama Kikuu cha Ushirika cha Rift Valley (RIVACU), lakini kwa sasa chama hicho kina matatizo makubwa ya ukosefu wa mtaji.
Mkazi mmoja wa Masakta, Dodo Mimbisambu, alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Kanali mstaafu Anatoli Tarimo, aliyefika Masakta kukagua shughuli za maendeleo hivi karibuni, kuwa umoja huo ulianzishwa mwaka 2005 baada ya viongozi wa wilaya kuwaeleza wananchi jinsi ya kuanzisha miradi kwa kutumia fursa na vikwazo walivyonavyo.
Viongozi hao waliwaeleza wananchi kuwa Mradi Shirikishi wa Maendeleo ya Kilimo na Uwezeshaji (PADEP), utasaidia kutoa mtaji iwapo wananchi watakuwa tayari kuunda umoja wao.
“Baada ya hapo tuliunda vikundi mbalimbali vya vijana, wazee na kina mama na kuangalia matatizo yetu pamoja na fursa tunazoweza kutumia kutatua matatizo hayo,” alisema.
Mimbisambu alifafanua kuwa: “Kwa pamoja tuliamua kutoa kipaumbele kwa mradi wa Soko la mazao la Masakta baada ya kugundua kuwa watu wa Masakta wana uzalishaji wa ziada wa mazao ya chakula na biashara lakini soko kwao ni tatizo.”
Anasema waliamua kutafuta soko na kisha kuwashawishi wananchi kuuza mazao yao katika ghala lao huku wakisubiri bei iwe nzuri ili waweze kupata faida zaidi.
Mwananchi huyo alibainisha kuwa utaratibu huo uliwasaidia kujiwekea tahadhali ya njaa kabla.
Mvua ilipokuwa adimu, wananchi hao wa Masakta hawakupata shida ya chakula. “Sasa tuna ziada ya chakula, tumepata soko, mtaji na baadhi yetu wamepata ajira kutokana na umoja huu,” anasema.
PADEP ilihaidi kuchangia asilimia 80 ya fedha zote za mradi huku wananchi wakichangia asilimia 20. Kwa mujibu wa Mimbisambu, PADEP ilitoa sh milioni 18, kati ya fedha hizo, milioni kumi zilitumika kununulia mazao, sh milioni tano zilikarabati ghala la kuhifadhia mazao na sh milioni tatu, zilitumika kutoa mafunzo kwa wanachama jinsi ya kuendesha mradi.
USOMAMA ilianzishwa na wananchama 66 wanaotoka katika vitongoji vya Tippiri, Mohetu, Bohoo, Buba, Howari, Gatindagaw na Gorosirone.
Wananchi hao walikubaliana kuchanga gunia moja la mahindi na kulipeleka katika ghala ili kukuza mtaji.
Awali wanachama hao walichanga magunia 500 na kisha kuuza magunia 200 wakati magunia 300 yalibaki katika ghala kama ziada iliyowasaidia wakati wa shida ya chakula.
“Mwanzoni mwa mwaka 2006, tuliuza gunia moja la mahindi kwa sh 28,000, watu mbalimbali wakiwamo waliotoka Kanda ya Ziwa walikuja hapa kununua mahindi. Tulipata faida mara mbili,” anasema na kuongeza kuwa faida hiyo iligawanywa katika sehemu mbili, ambapo kiasi kilitumika kuwapa fidia wanavijiji waliouza mazao yao na kiasi kingine sh milioni 14, kiliwekwa benki.
Kiasi kilichowekwa benki hakihusishwi na fedha za PADEP.
Baada ya mafanikio hayo USOMAMA ilianzisha SACCOS yenye zaidi ya wanachama 70 hivi sasa. Kiingilio katika SACCOS hiyo ni sh 5,000 na wanauza hisa kwa sh 20,000.
Hata hivyo Alute alieleza kuwa uanzishaji wa SACCOS hiyo haukuwa rahisi, kwani watu wengi walikuwa wanasita kujiunga na ushirika huo kutokana na kumbukumbu ya maduka ya ushirika yaliyovunjika.
“Wengi walikuwa wanategea kujiunga kwa sababu walikuwa na kumbukumbu za maduka ya ushirika yaliyoanzishwa na kuvunjika kutokana na viongozi wengi walioongoza ushirika huo kutokuwa waadilifu,” anasema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara, alitoa wito kwa viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza ushirika huo kutowaangusha wananchi bali watende kazi kwa uaminifu na uangalifu mkubwa.
Kanali Mstaafu Tarimo aliyeambatana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa, Dunstan Mrutu katika ziara hiyo aliuliza: “Kama hili limewezekana, Masakta na mazingira ya Tanzania ni yaleyale, kwanini mpango huu usifanyike kwingine?”
Anasema Watanzania wakiiga mfano wa Masakta na kuhifadhi chakula katika ngazi ya chini kwa kuimarisha maghala, hakutakuwa na tatizo la chakula nchini.
Kwa upande wake Mrutu anasema: “Mwanzo wa maendeleo ya Taifa hili ni ushirikishwaji kama walivyofanya wananchi wa Masakta.”
Aidha, alitoa changamoto kwa wananchi kujenga msingi wa ushirikishaji tangu ngazi ya chini badala ya kuanzia juu. “Msingi huu utasaidia uongozi katika ngazi mbalimbali kuwa karibu na wananchi. Kama hakuna ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na uongozi wao hakutakuwa na maendeleo,” alisema.
Kwa mujibu wa katibu huyo wa Baraza la Biashara la Taifa, ushirikiano wa namna hii utawasaidia Watanzania kujitegemea kiuchumi, na hii ndiyo njia pekee itakayowawezesha kujitawala.
Mwanzoni mwa mwaka huu (2006) Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Ali Mohamed Shein, alitembelea mradi wa USOMAMA na kutaka uwe mfano kitaifa wa miradi endelevu iliyobuniwa na kuendeshwa na wananchi.
Hivi karibuni Waziri wa Mipango, Uchumi na uwezeshaji Dk. Juma Ngasongwa alitembelea USOMAMA na kuwashauri kupeleka taarifa za fedha walizozipata kutoka PADEP ili wapate fedha nyingine.
Kulingana na makubaliano kati ya USOMAMA na PADEP, wakipeleka taarifa hiyo watapata sh milioni 17 kwa ajili ya kununulia mazao.