FAIDA iliyopata Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), baada ya kodi ilishuka kutoka sh bilioni 10 hadi sh bilioni 7.1 kwa kipindi kilichoishia Juni mwaka huu.
Taarifa ya kampuni hiyo iliyochapishwa kwenye magazeti mbalimbali juzi inaonyesha kuwa kushuka huko kwa faida ni sawa na asilimia 29.
Taarifa hiyo pia ilisema kuwa kampuni hiyo ilibidi ikope sh bilioni tatu ili kunusuru hali hiyo ya fedha ya kampuni.
Urari wa kampuni hiyo unaonyesha kuwa ulipungua kutoka sh bilioni 7.4 hadi sh bilioni moja.
Hali pia haikuwa nzuri kwenye gawio la awali, kwani lilishuka kutoka sh 78 hadi Juni mwaka jana; kwa hisa moja hadi sh 50 katika kipindi hicho kwa mwaka jana. Kushuka huko ni sawa na asilimia 35.
Wachambuzi wa mambo ya biashara wanasema kuwa ripoti hiyo ya fedha ya kampuni haitawafurahisha wanahisa wake.
Vyanzo vyetu vya habari ndani ya kampuni hiyo vinasema kuwa hali hii inasababishwa na gharama kubwa za uendeshaji na matangazo.
Sababu nyingine ni fedha nyingi kutumika kwenye promosheni na matangazo.
Pia wafanyakazi kadhaa wanalaumu pia matumizi yasiyo ya lazima kwa kuwalipa wataalamu wa kigeni kwa kazi ambazo zingefanywa na Watanzania.