NAIBU Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Diodorus Kamala, amepigwa butwaa kwa taarifa ya wafanyabiashara wa Kitanzania waishio mkoani Arusha.
“Tanzania inamalizwa, Tanzania inaliwa, wageni wanaliangamiza taifa,” ndiyo maneno aliyopewa Dk. Kamala katika mkutano wake na wafanyabiashara hao uliofanyika katika Hoteli ya Golden Rose.
Lengo la mkutano huo, lilikuwa kupata maoni na mapendekezo yao, juu ya nafasi ya Tanzania na Watanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mmoja wa wafanyabiashara hao alimweleza naibu waziri kwamba imefikia hatua sasa hata biashara ya vinyago katika hoteli za kitalii, inafanywa na wageni, hususan Wakenya.
Alisema serikali inaweza kulibaini hilo kwa kwenda kwenye hoteli nyingi, hasa zinazomilikiwa na wageni.
Naibu Waziri alipatwa na mshangao, baada ya kuelezwa kwamba imefikia hatua ya hoteli nyingi zilizopo katika ardhi ya Tanzania, kuendeshwa na mamluki kutoka Kenya.
“Wapo mameneja Wakenya hupokea wageni, usiku hukutana nao na kuwaeleza kwamba wamefika Tanzania kufuata nini? Kwa nini wanaacha Kenya ambako kuna hoteli nzuri, barabara safi na huduma nyingi nzuri na za kisasa,” alisema mfanyabiashara huyo.
Alisema Wakenya wengi waliopo katika hoteli za hapa nchini, ni mawakala wa kuua biashara ya utalii Tanzania, kwa vile ndiyo njia pekee waliyoona inafaa baada ya Tanzania kujitangaza.
“Athari za haya zitaonekana baada ya miaka kadhaa, miaka 10 ijayo. Hakuna mtalii atakuja Tanzania, kwani wakirudi wanawaeleza wenzao kuwa sehemu nzuri ni Kenya,” alisema mwingine.
Dk. Kamala aliendelea kusikiliza mengi kutoka kwa wafanyabiashara hao waliosema wameamua kuzungumza kwa uwazi kutokana na imani yao kwa serikali mpya.
Mfanyabiashara mwingine alisema kuna hujuma kubwa mno inayofanywa na hoteli za wageni zilizopo katika mbuga mbalimbali.
Alisema Watanzania wakienda kuweka miadi kwa ajili ya wageni wao, hawapati nafasi; hali inayowafanya wakose wageni.
“Hoteli zote zinaendeshwa na Wahindi (si Watanzania) na Wakenya, wameajili Wakenya ambao kila tukienda kuweka miadi ya vyumba, tunaambiwa hoteli zimejaa Januari hadi Januari - mwaka mzima.
“Tena kule wanakotoka, wanatuambia kuwa kama hatukuchukua hotel fulani, hawatupi wageni. Hizi hoteli zilizopo mbugani, nyingi makao yake yako Kenya.
“Wakati hapa tunaambiwa zimejaa, ukiweka booking kutokea Kenya, unapata chumba, unapata kwa sababu wanataka pesa ziishie kwao, na kweli hili wamefanikiwa.
“Nakuambia Mheshimiwa Waziri, Wakenya na Wahindi wamejenga mtandao wa kutumaliza, serikali ichukue hatua haraka.
“Tena wameamua kuweka huduma mbaya katika hoteli zetu, chakula kibovu, na kinacheleweshwa sana. Wakati mwingine hakuna maji, ni shida, wageni walalamika hawataki tena kurudi.
“Haya yanayofanywa ni njama za kuharibu kabisa biashara ya utalii Tanzania, lazima serikali imalize matatizo haya haraka,” alisema.
Kampuni kubwa zenye hoteli nyingi Serengeti, Ngorongoro na kwingineko ni TAHI, Sopa na Serena. Zote hizi zinaendeshwa na wageni.
Kwa upande wake, Dk. Kamala, alisema hoja za wafanyabiashara hao ni nyeti, amezisikia, na serikali itazifanyia kazi haraka iwezekanavyo.
Alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki imeundwa ili kunufaisha pande zote, na kwamba vitendo vya hujuma vitachunguzwa, na kama vipo, vitashughulikiwa kwa mikondo sahihi ya kisheria iliyowekwa.