Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kamati yamwanika Severe
Kamati yamwanika Severe
By Habari Tanzania | Published  09/11/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Mwandishi Wetu

KAMATI iliyoundwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Anthony Diallo, kuangalia uboreshaji wa Idara ya Wanyamapori, imeanika kila aina ya mbinu zinazochochea ufisadi ndani ya idara hiyo nyeti kwa uchumi wa nchi. Diallo aliunda kamati hiyo Aprili 27, mwaka huu, na ilifanya kazi yake kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Kwa miaka 10 hivi, idara hiyo inaongozwa na Emmanuel Severe; ambaye licha ya kuenguliwa, ameendelea kukalia ofisi hiyo. Suala lake sasa linahitaji utatuzi kutoka Ikulu, kwa Rais Jakaya Kikwete.

Tanzania Daima imefanikiwa kupata nakala ya ripoti ya kamati hiyo. Udhaifu wa sheria unaotoa mianya ya ufisadi kwa baadhi ya viongozi wa Idara ya Wanyamapori na Wizara kwa jumla, umeainishwa.

Kamati, kimsingi imekiri kuwa idara hiyo ina matatizo makubwa ya kimuundo na kiutendaji, jambo ambalo linapaswa kufanyiwa marekebisho haraka iwezekanavyo.

Kuhusu kampuni za uwindaji imesema: “Ingawa kati ya kampuni 49 za uwindaji, kampuni 28 zinamilikiwa na wananchi; kamati imebaini kwamba kampuni za kigeni 12 tu zinamiliki vitalu 57 kati ya vitalu 73 vya mapori ya akiba.

“Maeneo haya yana wanyama wengi ukilinganisha na vitalu vya kampuni za wananchi ambavyo viko katika maeneo ambayo hayana wanyama wengi. Mgawanyo wa aina hii wa vitalu unalalamikiwa sana na wananchi.

“…Kamati inaona kuna umuhimu wa kuzifanya taratibu za sasa za kugawa vitalu kuwa wazi zaidi na Kamati ya Ushauri ya Kugawa Vitalu kutambulika kisheria.

“Kamati imebaini kwamba Idara ya Wanyamapori haisimamii kikamilifu tasnia hii, kwa maana haina hata taarifa muhimu kuhusu vitalu na thamani halisi ya vitalu hivi.

“Kamati imepata uzoefu wa nchi jirani, hasa ule wa Botswana, Zimbabwe na Afrika Kusini. Katika nchi hizo, idara au taasisi zinazosimamia uwindaji wa kitalii zinafanya kazi hiyo kwa ufanisi wa hali ya juu na mapato kutoka tasnia hiyo hasa nchini Zimbabwe na Afrika Kusini ni ya juu sana.

“Nchi hizo pia zina mipango madhubuti ya kuwashirikisha wananchi katika uwindaji huo wa kitalii,” imesema ripoti hiyo.

Kamati hiyo iliendelea kutoa mapendekezo katika sekta ya uwindaji wa kitalii.

“Kuboresha utaratibu wa ugawaji wa vitalu kwa kuipa Kamati ya Ugawaji Vitalu nguvu za kisheria na kwa kupanua uwakilishi wake.

“Kuunda Wakala wa Serikali wa kusimamia shughuli za uwindaji wa kitalii badala ya Idara ya Wanyamapori.

“Kuangalia upya umiliki wa vitalu ili kuwawezesha wananchi kushiriki zaidi katika uwindaji wa kitalii kwa njia ya ubia na baadaye kumilikishwa vitalu wakati wageni na wananchi watafanya kazi ya kuwindisha.

“Serikali iwawezeshe Wawindaji Bingwa wa Kitanzania ili waweze kumiliki vitalu na kutumia ujuzi na uzoefu walionao. Serikali inaweza kuwawezesha wananchi kwa kuzungumza na mabenki ili wapunguze riba ya kukopa fedha benki na kuruhusu matumizi ya vitalu kama dhamana. Pia wawindaji bingwa waanzishe bodi yao ya kitaalamu.

“Kuthamini vitalu vya uwindaji wa kitalii na kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ili kuongeza mapato ya Serikali,” imependekezwa.

Kamati hiyo pia imependekeza muda maalumu wa kumiliki vitalu. Mapendekezo hayo yanatokana na ukweli kwamba kuna wageni Wazungu wanaomiliki vitalu kwa miaka 20 sasa, huku wakiendelea kulindwa na viongozi kadhaa bila wasi wasi wowote.

“Muda wa kumiliki kitalu uwe wa vipindi viwili vya miaka mitano. Ukomo wa kumiliki kitalu utakuwa katika kipindi cha pili ili kuruhusu waombaji wapya,” imependekezwa.

Umilikishaji vitalu kati ya idara na kampuni, nao umebainika kuwa na upungufu ufuatao:

“Hakuna mikataba inayosainiwa kati ya Idara na kampuni husika, badala yake Idara hutoa barua ya toleo. Barua za toleo kwa wanaofanikiwa kupata vitalu hutoa masharti tofauti.

“Makubaliano ambayo Idara huingia na baadhi ya wadau hayazingatii sheria. Maelezo zaidi ya mikataba/makubaliano hayo yameelezewa zaidi katika Sura ya Tatu.

‘‘Kamati ya Ushauri ya Ugawaji Vitalu.

Kamati itambulike kisheria kama chombo chenye mamlaka katika ugawaji wa vitalu.

‘‘Idadi ya wajumbe wa kamati iongezwe kuhakikisha ushiriki wa wadau muhimu kutoka Wizara za Ardhi, Maliasili na Utalii, Jumuiya za Watafiti, Serikali za Mitaa pamoja na mashirika yanayojihusisha na uhifadhi.

‘‘Njia nyingine ya kuboresha utawala bora ni kuondoa uendeshaji wa biashara ya uwindaji wa kitalii kwenye Idara ya Wanyamapori, na kuiundia Wakala wa Serikali.

‘‘Mfumo wowote utakaotumika uzingatie ushirikishwaji wa serikali za vijiji katika maeneo ya wazi.

‘‘Muda wa umiliki wa vitalu vya uwindaji uwe wa vipindi viwili vya miaka mitano, na endapo katika kipindi cha kwanza kampuni itafanya vizuri, itapewa kipindi cha miaka mitano mingine bila ushindani. Baada ya hapo kitalu kitakuwa wazi kwa waombaji wote.

‘‘Kamati imependekeza vigezo vya uombaji leseni ya uwindaji wa kitalii. Hali hiyo imelenga zaidi kuwakomboa Watanzania ambao kamati imekiri kuwa si wao, wala taifa, wanaofaidika na utajiri huu wa asili.

‘‘Vigezo vya uombaji wa vitalu vya uwindaji :  Kuwa na mpango wa uendeshaji biashara ya uwindaji wa kitalii na ubainishe vyanzo vya fedha.

‘‘Kampuni ombaji iwe imesajiliwa Tanzania ikiwa na umiliki usiopungua asilimia hamsini na moja chini ya Mtanzania. Kampuni hiyo inaweza kuwa ya Mtanzania tu, ya ubia kati ya kampuni ya kigeni na ya Kitanzania ama kampuni ya kigeni na jumuiya ya jamii iliyoidhinishwa.

“Serikali ichukue hatua za makusudi kuhakikisha kwamba nafasi za kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania, ambazo kwa sasa zimechukuliwa na wageni, zinafanywa na wananchi wenye uwezo.

“Ni vizuri hapo baadaye kuiga utaratibu wa Afrika Kusini na Zimbabwe ambako kampuni za wamiliki wa vitalu vya uwindaji na wawindishaji wanaoruhusiwa ni wananchi wao,” imesema sehemu ya taarifa ya kamati hiyo.

Kutokana na unyeti wa suala lenyewe, Tanzania Daima itaendelea kuwapa yaliyomo kwenye ripoti ya kamati hii.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.