Na Furaha Omary
SHAHIDI katika kesi ya mauaji ya wakili wa kujitegemea Eliutherius Kapinga, amekiri kuwa fomu zake zilizotolewa jana mahakamani kama kielelezo cha gwaride la utambulisho zina makosa.
Shahidi huyo Magnus Mugongo (47) alikiri hayo jana baada ya kubanwa na mawakili wanaowatetea washitakiwa watano wanaokabiliwa na shitaka la mauaji ya Wakili Kapinga.
Mugongo ambaye ni Ofisa wa Polisi wa upelelezi wa makosa ya jinai, Mkoa wa Dar es Salaam, alidai hayo katika Mahakama Kuu ya Tanzania alipokuwa akitoa ushahidi wake mbele ya Jaji Juxon Mlay.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Arafa Msafiri, Mugongo alidai Juni 12 mwaka 2002, saa 11.40 jioni, akiwa kazini alipewa kazi na mkuu wake ya kuendesha gwaride kuhusu utambulisho wa washitakiwa wa mauaji ya Wakili Kapinga.
Katika gwaride hilo kulikuwa na mashahidi wawili, ambao ni Salome Fredy na Joyce Charles waliokuwa wafanyakazi wa ndani nyumbani kwa Kapinga.
Shahidi alidai alikabidhiwa washitakiwa wawili ambao walikuwa wakishikiliwa katika mauaji hayo ili waweze kushiriki katika gwaride hilo ambao ni Ramadhani Said, mshitakiwa wa pili na Goodluck Sangawe mshitakiwa wa tatu.
Mugongo alidai katika gwaride hilo ambalo washitakiwa waliunganishwa na watu wengine wenye miili kama yao, mashahidi waliweza kuwatambua washitakiwa kwa nyakati tofauti.
Mugongo alidai baada ya muda aliletwa mshitakiwa mwingine ambaye ni Zakharia Mahushi au Ngosha ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa bustani wa Kapinga ambaye nae aliweza kutambuliwa na mashahidi hao.
Mahojiano kati ya mawakili wa utetezi Rindstone Ezekiel na Cyricus Binamungu yalikuwa kama ifuatavyo.
Wakili Ezekiel: Shahidi ulikuwa unaendesha gwaride la utambulisho ulikuwa unataka nini?
Shahidi: Nilikuwa najua ninachokitafuta na ninachokifanya.
Ezekiel: Unajua kama kwenye fomu yako ya utambulisho ya pili hakuna jina la mshitakiwa Zakharia ambayo unasema alitambuliwa.
Shahidi alikubali kutokuwepo kwa jina hilo baada ya kupewa fomu hizo kuangalia na kusoma.
Wakili Binamungu: Unasemaje Ngosha hakushiriki katika gwaride la kwanza wakati jina lake lipo katika orodha ya washiriki?
Shahidi : Nimefanya makosa katika kurekodi ambapo majina ya gwaride la kwanza la kuwatambua Sangawe na Said yameingiliana na yale ya Ngosha.
Binamungu : Ni lini umegundua makosa katika fomu hizi ambazo ulikuwa umerekodi wewe mwenyewe na kutaka kutoa mahakamani kama kielelezo?
Shahidi: Leo (jana), kutokana na miaka mingi imepita sijawahi kukaa na jalada ili niweze kuzikagua fomu hizo .
Katika hatua nyingine jana mawakili hao wa utetezi waliwekea pingamizi maelezo ya ungamo la mshitakiwa Ally Ngenya mshitakiwa namba tatu, ambalo lilikuwa likitaka kutolewa mahakamani kama kielelezo na shahidi Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Ikwiriri, Moshi Mazola , ambaye awali alikuwa Hakimu wa Mahakama ya mwanzo Kinondoni.