Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Umeme Jumapili kwa faida gani?
Umeme Jumapili kwa faida gani?
By Manyerere Jackton | Published  09/10/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

TAIFA letu linakabiliwa na mgawo wa umeme. Athari zake zimeanza kuonekana.

Kukosekana kwa nishati hiyo kunaathiri uchumi na kuvuruga malengo mazuri ya kuujenga.

Kwa kiasi kidogo kinachozalishwa sasa, tunapaswa kukitumia kwa busara zaidi ili tuzalishe zaidi.

Katika mgawo huu, awali, Jumamosi na Jumapili zilikuwa siku pekee ambazo umeme ungewaka kwa saa zote.

Lakini ndani ya saa 24, uamuzi huo ulifanyiwa marekebisho. Ikawa sasa umeme utapatikana siku za Jumapili na Ijumaa. Wapo waliohoji, na hata kutaka kutumia dhana ya udini katika uamuzi huu. Hii si hoja, na wala sipendi kuijadili.

Mabadiliko yaliyofanywa, ya kuiondoa Jumamosi, nayapongeza. Swali ninalojiuliza ni moja, kwa nini Jumapili, kutwa nzima, umeme uwake? Kwa nini Jumapili, siku ambayo si ya kazi, kuwe na umeme wakati watu wamestarehe?

Swali hili linanipeleka moja kwa moja kwenye hoja yangu. Nayo ni kwamba, Watanzania tunautumia vibaya sana muda na siku za kazi. Tunapenda sana hii “pumzika, pumzika.”

Nasema hivyo kwa sababu, Jumapili ni siku ya mapumziko, kama ilivyo Jumamosi. Lakini tofauti na Jumapili, walau Jumamosi kuna ofisi zinafanya kazi kwa nusu siku. Benki ni miongoni mwa ofisi hizo.

Jumapili maduka na ofisi nyingi hufungwa. Kimsingi, mahitaji ya umeme kwa siku ya Jumapili ni kwa ajili ya nyumbani, kanisani na kadhalika.

Mimi nilidhani kuwa kwa vile umeme ni wa mgawo, basi ungetumika zaidi siku za kazi ili Watanzania waweze kuchapa kazi kwa lengo la kuboresha maisha yao ya sasa na kwa vizazi vijavyo.

Lakini kama tunaamua kuutumia umeme siku za mapumziko, kwa ajili ya kustarehe majumbani tukitazama filamu za Kinigeria, na kusikiliza vitimbi katika redio zetu nyingi, basi tumefanya makosa makubwa.

Wapo wanaotetea umeme uwepo Jumapili eti kwa sababu Wakristo wengi wanakuwa makanisani. Huu nao ni udhaifu katika uamuzi wetu.

Ni kweli Jumapili makanisa mengi huendesha shughuli za ibada. Kiasi cha umeme kinachohitajika katika ibada, ni cha kuwashia taa na mapangaboi tu.

Umeme unaohitajika ni mdogo. Jenereta inayouzwa sh 200,000 inaweza kununuliwa, ikafanya kazi hiyo. Sadaka za makanisani ni nyingi, zinatosha kabisa kuendesha jenereta ya aina hiyo. Hakuna majokofu wala mitambo mingine makanisani inayohitaji umeme wa gridi ya taifa.

Nasema hivyo kwa sababu makanisa ni ya umma. Umma una haki na wajibu wa kujitafutia umeme. Serikali itakuwa imefanya makosa makubwa kuifanya Jumapili iwe na umeme kutwa nzima, kwa sababu tu ya kutaka kuwafurahisha waamini fulani.

Mungu tunayemwabudu, anapokea maombi yetu hata kama tutakuwa tunayaendesha kwa mwanga wa vibatari, mishumaa au kwa mwanga wa jenereta. Mungu hakusema umeme wa gridi ya taifa ndiyo unaompendeza.

Uamuzi wa kuifanya Jumapili iwe na umeme kutwa nzima, badala ya nishati hiyo kupatikana siku za kazi, ni wa kuliangamiza taifa kiuchumi. Zaka makanisani, hazimalizi umasikini wetu.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika kitabu chake cha “Ujamaa ni Imani (2)”, alisema: “Umasikini hauondoki kwa zaka za Jumapili; umasikini unatolewa kwa kodi, au kwa kila mtu kufanya kazi.”

Kama hivyo ndivyo, tuna sababu gani ya kuwa na umeme kutwa nzima ambao hauzalishi kitu? Kama ni kupata umeme kwa ajili ya kumwabudu Mungu, umeme wa jenereta au wa nguvu za jua, haufai? Kanisa gani lenye waamini linaloweza kukosa fedha za kununua jenereta na mafuta?

Moja ya makosa makubwa kabisa yaliyofanywa na uongozi wa awamu ya pili, ni kuzifanya siku mbili - Jumamosi na Jumapili- kuwa siku za mapumziko.

Taifa masikini kimaendeleo kama Tanzania, watu wake hawapaswi kupumzika kwa staili hii. Tunapaswa kufanya kazi usiku na mchana.

Ulaya, Marekani, Asia na kwingineko ambako wameendelea, hawalali; seuze sisi ambao bado tunaendelea kuvaa mitumba hata ya nguo za ndani?

Nimepitia kalenda ya mwaka huu wenye siku 366. Kati ya siku hizo, siku ambazo Watanzania wanapaswa kisheria kuwapo ofisini ni 226.

Tunapumzika hivi: Siku 105 ni Jumamosi na Jumapili za mwaka tunazopumzika. Siku 17 ni sikukuu kuanzia ya mwaka mpya hadi siku ya zawadi. Siku 28 ni za likizo. Jumla ya siku tunazokuwa nje ya ofisi (kwa watumishi wenye ajira rasmi) ni 140!

Siku hizo 140 tunazopumzika, ni nje kabisa ya siku za udhuru! Kuhudhuria misiba ya majirani, ndugu na kadhalika. Hii ni kawaida yetu Waafrika kuhudhuria mazishi ya watu wanaotuhusu kwa namna moja au nyingine.

Siku hizo ni nje kabisa ya siku ambazo mtumishi anatega kwenda kazini kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo za ulevi au “kutojisikia”.

Mapumziko haya makubwa hayahusishi saa ambazo mtumishi anakuwa ofisini. Anaweza kuchelewa kuingia ofisini, kisha akaenda kunywa supu, na kwa sababu ya ulevi anaoamka nao, akisharejea ofisini atajifungia katika chumba na kuuchapa usingizi.

Kwa vile walevi wengine wanaamini katika kuzimua pombe, wengine huwahi kutoka ofisini ili wapite mahali fulani, wapate fedha za kuzimulia.

Haya yote ni nje kabisa na utaratibu wa siku za Jumatatu na Ijumaa, siku ambazo kimsingi si za kazi, ingawa zinahesabika kama siku za kazi.

Kwa nini si siku za kazi? Si siku za kazi kwa sababu Jumatatu tunaingia ofisini tukiwa tuna mawenge ya ulevi. Kazi hazifanywi vizuri.

Ijumaa tunaiita “siku ya lala salama”. Kama ni mpirani, basi kingekuwa kipindi cha pili. Siku hii ndiyo inayotumiwa na wengi kukwepa kazi, wakiwa katika maandalizi ya wikiendi.

Asiye na fedha, Ijumaa hakai ofisini. Huhangaika huku na kule alimradi apate cha kumwezesha kustarehe siku za Jumamosi na Jumapili. Tunahitaji pesa kwa ajili ya starehe, lakini tunaogopa kuchapa kazi kwa bidii!

Nimezungumzia sana suala la ulevi kama moja ya sababu kuu za kukwamisha maendeleo yetu. Nina hoja za msingi za kuitambua pombe kama kikwazo cha maendeleo.

Nchi za Afrika, Kusini kwa Jangwa la Sahara, ndizo pekee katika ulimwengu huu ambazo watu wake wanakunywa pombe saa 24, na siku saba za wiki. Ndizo nchi ambazo baa na shule vinatenganishwa na kuta! Ndizo nchi ambazo muziki wa baa hupigwa ilhali nyumba ya pili kuna hospitali yenye wagonjwa wa maradhi mbalimbali!

Ndizo nchi ambazo mzazi anamweleza mwanawe ampitie baa, ili amnunulie chips na soda, na hata ka-wine kidogo kabla ya kwenda nyumbani!

Hapa ndipo watoto walio chini ya umri wa miaka 18 wanaweza kwenda kucheza pool, huku wakishuhudia kila aina ya uchafu unaosababishwa na ulevi!

Matokeo ya yote hayo, nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ndizo zenye makabwela wengi wasiopatikana katika eneo lolote la dunia hii.

Makabwela wametanda kila mahali, ilhali ndilo eneo lenye utajiri mwingi na wa kutisha, unaowafanya wazungu wasitake kuona vita ikikoma, ili waendelee kuufaidi.

Viongozi wetu, bila kuona soni, wanajivunia mafanikio makubwa yaliyotokana na ubinafsishaji wa viwanda vya bia na sigara! Tunajivuna kwamba TBL ndiyo kampuni inayolipa kodi kubwa zaidi (zaidi ya sh bilioni 50 kwa mwaka), ikifuatiwa na Kampuni ya Sigara (TCC).

Hii maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba nchi hii walevi na wavuta sigara ni wengi. Ulevi na uvutaji sigara ni madhara. Viongozi wa taifa linaloshabikia watu wake kulewa na kuvuta sigara, ni viongozi goigoi na wauaji wa kizazi cha Waafrika.

Madhara ya pombe, sote tunayajua. Madhara ya sigara, yako wazi kabisa. Kwa ufupi, matokeo ya ulevi wote huu, ni maradhi, na hatimaye kifo.

Taifa gani la watu wenye maradhi ya kansa na wendawazimu linaweza kupambana na taifa la wachapakazi ambao kama ni kunywa, huenda sehemu maalumu, kwa siku maalumu na kwa rika maalumu?

Tumebariki matangazo ya sigara na pombe, tena kwa kuyawekea maneno kama, “haya ndiyo maisha”. Wanafunzi wanayaona. Watoto wanayaona. Kitu gani kitamzuia mtoto kuvuta au kunywa pombe, kama hayo ‘ndiyo maisha’?

Hatuwezi kupata maendeleo kwa kuendekeza haya tunayoyaona sasa. Wazungu wana mbinu nyingi sana za kutumaliza. Tusipokuwa makini, siku moja Waafrika hatutakuwapo, na tukiwapo duniani, tutakuwa watumishi wao tu.

Kuhusu nini kianze kati ya raha na kazi, Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha ‘Ujamaa ni Imani (2)’, alisema: “Tunajidanganya sisi kufikiri kwamba tunaweza kuanza na raha halafu ndiyo tuendelee. Hata kidogo. Kwanza kazi, halafu sigara baadaye.” Mwisho wa kunukuu.

Haya ni ya kweli kabisa. Hata katika mataifa yaliyoendelea, hakuna mahali pombe zinauzwa kama ilivyo Tanzania. Hakuna upondaji raha wa aina hii! Huwezi kuwa Washington au London, ukakutana na aina ya ulevi huu wa hadharani, usiozingatia maadili. Haupo. Walevi wapo, lakini serikali za huko haziushabikii kama hapa kwetu. Sigara wanavuta, lakini si kwa matangazo kama haya barabani, kwenye TV, sokoni na kila mahali!

Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imekuja na neno tamu mno la, “maisha bora kwa kila Mtanzania”. Maneno haya ni matamu. Ni mepesi mno kuyatamka, lakini ni magumu kuyatekeleza.

Kwa mwenendo halisi tulionao sasa, umasikini wa Tanzania hautaondosheka. Kama tunajidanganya kwa kuamini kuwa sh bilioni moja katika kila mkoa ndiyo njia ya kujikomboa, tunajidanganya! Njia sahihi ya kujikomboa kiuchumi ni kubadili tabia zetu katika utendaji kazi. Tupunguze mapumziko na starehe.

Kama tunaweza kufanya kazi mchana pekee, kisha usiku tukawa ni watu wa kupiga soga na kulala, kamwe hatuwezi kuendelea.

Kwa mfano, kuna sababu gani sasa ya msingi ya kuyazuia mabasi kusafiri usiku? Usiku ungeweza kutumiwa vizuri sana kwa wafanyabiashara wanaotumia magari hayo.

Mathalani, mfanyabiashara anaweza kuondoka Arusha jioni, alfajiri akawa ameshafika Dar es Salaam. Duka likafunguliwa akiwapo. Mchana kutwa akafanya shughuli za ununuzi, kisha jioni akalala ndani ya basi akirejea Arusha.

Hii maana yake ni kwamba mchana atakuwa ametekeleza wajibu wake, na usiku inakuwa zamu ya dereva na wasaidizi wake kufanya kazi. Ndivyo nchi inavyojengwa.

Taifa linaloendelea ni lile ambao sauti za watu husikika muda wote-mchana na usiku. Walioendelea, hutokwa jasho muda wote-usiku na mchana. Hufanya kazi kwenye mwanga wa jua, na wa mbalamwezi.

Maisha bora kwa kila Mtanzania hayawezi kuja kama mfumo mzima wa utendaji kazi wetu ni wa kutaka kupumzika zaidi.

Hatuwezi kupata maendeleo kama tunapumzika nusu nzima ya mwaka au zaidi! Madai ya mishahara ni halali. Lakini ni ukweli ulio wazi kwamba kuna makundi ya watumishi wa umma wasiostahili kudai nyongeza za mishahara.

Ni ukweli pia kwamba nyongeza za mishahara zinatokana na tija iliyopatikana. Anapopatikana sungura, tugawane kutokana na ukubwa wake. Anapopatikana mbogo, atakayegawiwa ukubwa ule aliogawiwa kwa sungura, alalamike. Lakini ni fedheha kudai nyama zaidi, kama mawindo yenyewe ni sungura. Tufanye kazi zaidi, ili tupate zaidi.

Mapendekezo yangu yako wazi. Jumamosi iwe siku ya kazi kama kawaida. Kuna sikukuu za kiimani ambazo haziwezi kubadilishwa. Hivyo, Jumapili na siku hizo za sikukuu, pamoja na likizo ya siku 28, ndizo ziwe siku za mapumziko.

Warusi wanao utaratibu mzuri. Siku za sikukuu zinazoangukia siku za kazi, hupumzika, lakini huzifidia siku hizo kwa kuongeza muda wa kufanya kazi katika siku nyingine. Nasi tufanye hivyo.

Unapotokea mgawo wa umeme, uwe kwa siku zisizo za kazi. Siku za kwenda ofisini, umeme uwashwe, tuchape kazi. Jumapili, tununue majenereta. Umasikini haumalizwi kwa porojo au kukaa tu na kusema, “one day yes!”

e-mail: manyerere@hotmail.com
selula: 0713 33 54 69


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.