WENGI walimdharau na kumbeza wakati alipokuwa akiomba nafasi ya uwakilishi bungeni kwa tiketi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), kwa madai kuwa hana uwezo.
Walimdharau pia kwa madai eti hakusoma na hawezi kuwa mwakilishi wa vijana katika Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa kuwa pia hakuwa na sifa zinazotakiwa kwa nafasi aliyoihitaji.
Kinyume cha matarajio yao waliombeza, kumdharau na hata kumtusi, sasa anafanya mambo makubwa na ya kutia moyo kwa Watanzania wote hususan vijana, watoto na wanawake, akiwa Mbunge wa Viti Maalumu (UVCCM).
Si mwingine bali ni aliyekuwa mtangazaji wa Clouds FM, Amina Chifupa Mpakanjia, ambaye sasa anaitwa Mheshimiwa machachari sana bungeni, ambaye amekuwa akionyesha uwezo wake, ni kwa jinsi gani anawawakilisha waliompendekeza.
Akiongea na mwandishi wa makala hii mjini Dodoma, Chifupa anasema kabla hajaitwa mheshimiwa alikuwa akikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo nyingine zilikuwa ama zikimkatisha tamaa kabisa na nyingine zilikuwa zinamfanya aendelee kutafuta kupata nafasi hiyo.
Anasema kitendo cha kuandikwa vibaya katika baadhi ya vyombo vya habari na hasa magazeti ya udaku kuonyesha kuwa yeye ni mdogo na hana uwezo wa kuwa bungeni akiwakilisha vijana vilikuwa vikimkatisha tamaa kwa kiasi kikubwa.
Akielezea hatua alizopitia wakati wa mchakato, Chifupa anasema kuwa katika kipindi hicho alichokuwa akizunguka mikoani akitafuta wadhamini katika mikoa 26 yote ya Tanzania alikuwa akifunga na kusali.
Anasema alikuwa katika wakati mgumu sana katika kipindi cha uchaguzi ambapo siku ya uchaguzi wa majina katika Ukumbi wa NEC, CCM makao makuu mjini Dodoma, alikuwa akijisikia vibaya, jambo ambalo lilimfanya kushindwa kuomba kura kwa wajumbe akiwa nje ya ukumbi.
“Nilikuwa nafikiria jinsi nilivyochafuliwa katika magazeti halafu nikashindwa sijui itakuwaje, lakini pia nilikuwa naomba Mungu nipate nafasi hii ili nionyeshe uwezo wangu kwa jamii ya Watanzania, siku moja kabla ya uchaguzi sikulala kwa kweli, nilikuwa naomba kura kwa wajumbe hadi saa 1 asubuhi,” anasema mbunge huyo.
Anasema pia aliwaomba wanawake wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili ashinde katika uchaguzi huo ambao ulimchanganya kwa kiasi kikubwa.
“Nilikuwa najisikia kulia lakini silii, nikawa najifikiria nitajielezea vipi kwa wajumbe na wanipe kura zao nikiwa ndani ya ukumbi, lakini baadaye nilipiga simu nyumbani nikaomba kuongea na mwanangu Abdulahman Mpakanjia (4), akaniambia mama nakutakia kila la heri utashinda tu, alivyoniambia hivyo nilijisikia uchungu nikalia lakini baadaye kina mama wa UWT wakanipa moyo nikasali hicho kitu kikatoka,” anasema.
Chifupa anasema baadaye waliitwa mmoja mmoja ndani ya ukumbi kwa ajili ya kujieleza ambapo walikuwa tisa ambao walikuwa wakiomba nafasi mbili tu, baada ya wengine kujieleza hatimaye muda wake uliwadia na akajieleza kwa wajumbe na kuomba kura.
“Kwa kweli niliongea pale jukwaani nikawaomba wajumbe wanichague ili niwatumikie, nikawaomba kura zao, nikaondoka,” anasema.
Baadaye matokeo yalitangazwa na Mwenyekiti wa UVCCM ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuwa Amina Chifupa Mpakanjia na Lucy Mayenga ndio walioshinda nafasi ya uwakilishi bungeni upande wa UVCCM.
“Mume wangu alitumiwa ujumbe mfupi na mmoja wa wagombea ambao tulikuwa nao, ujumbe ambao ulisomeka hivi: “Pamoja na kuwa Amina alikuwa na nguvu kubwa ya ushindi tangu mwanzo, nguvu zaidi iliongezeka katika kipindi cha kujieleza, yaani aliongea vizuri sana tena pointi tupu kutushinda wagombea wote nadhani, hivyo kura nyingine alizizoa kwa hotuba yake tu, Meddy, jisifu mke unaye,” ulieleza ujumbe huo ambao ulitumwa na Mejiti, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dodoma.
Chifupa anasema alikuwa anampa ushindi zaidi Lucy Mayenga kwa kuwa tayari alikuwa mjumbe wa Baraza la UVCCM taifa.
Akielezea siku yake ya kwanza kuwamo bungeni akiwa mheshimiwa, anasema alikuwa akiogopa kwanza kuongea, pili alikuwa akiwaogopa watu wakubwa ambao zamani alikuwa akiwaona katika luninga wakiwamo watunga sheria.
Anasema kwa mara ya kwanza kuongea bungeni ilikuwa ni Bunge la kwanza, ambapo alichangia hoja ya rais aliyoitoa bungeni wakati alipozindua Bunge la Serikali ya Awamu ya Nne, ambapo aliongelea mambo mbalimbali ikiwamo kujengwa kwa hospitali ya kutibu magonjwa ya moyo kwa kina mama na watoto.
“Nilikuwa natetemeka moyoni lakini nilijitahidi kuongea bungeni huku watu wazima na wengine wasomi kuliko mimi wakiniangalia na kunisikiliza kwa makini,” anasema.
Anasema baada ya kuongea alipata ujumbe mwingi ndani ya Bunge kutoka kwa wabunge mbalimbali ambao walimpa hongera kwa kuongea vizuri, na wengine walikuwa wakikataa kuwa si Amina yule ambaye walikuwa wakimsoma katika magazeti.
Chifupa anasema kuwa siku hadi siku amekuwa akipata uzoefu kutoka kwa wabunge wengine ambao wamekuwa wakimshauri namna ya kujenga hoja na kuziwasilisha bungeni na kusikilizwa na mawaziri.
Anasema tofauti na alivyokuwa akifikiria kabla hajawa mbunge kuwa Bunge ni la watu wakubwa tu, sivyo, sasa anajiona kama yuko shule anajifunza kutoka kwa watu mbalimbali, wasomi na watu wazima ambao wanamzidi umri.
“Pamekuwa kama shule, watu ambao sikuwahi kutegemea kukaa karibu nao na kubadilishana nao mawazo au kuchangia mawazo sasa nakaa nao na tuko wamoja, hakuna tofauti” anasema Chifupa.
Anasema sasa anajihisi tofauti kwa kuwa mbunge, kwa kuwa anaona kuwa amepanda hadhi kutoka hadhi aliyokuwa nayo zamani, kwa kuwa Bunge ni kitu kikubwa na kinafanya maamuzi makubwa.
Anasema ahadi ambayo alitoa kwa vijana kuwa akipata nafasi ya uwakilishi wao atakuwa akisikiliza ushauri kutoka kwa vijana wote ndani na nje ya CCM, ni ya kweli na tayari ameshaanza kuifanyia kazi na haikuwa ya kuombea kura.
Anasema amekuwa akipata malalamiko mengi sana kutoka kwa vijana ambayo mengi tayari ameshayaongelea bungeni, kwa kuwa huwa hasimani kuongea bungeni bila kufanya utafiti.
Amina Chifupa anasema anawazimia sana wabunge vijana wachapakazi ambao ni pamoja na Lazaro Nyarandu (CCM), Halima Mdee (CHADEMA), William Ngeleja (CCM), Zitto Kabwe (CHADEMA), Pindi Chana (CCM), Martha Mlata (CCM), na Grace Kiwelu (CHADEMA).
Kama walivyo watu wengine pia, Amina Chifupa anawazimia wabunge watu wazima wenye hoja za kufa mtu bungeni, ambao amemtajia mwandishi wa makala hii kuwa ni Chrisant Mzindakaya (CCM), Harith Mwakyembe (CCM), Agrey Mwanri (CCM), Dk. Wilbroad Slaa (CHADEMA), Phales Kabuye (TLP), Gertrude Mongella (CCM) na Anne Kilango Malecela (CCM).
KITU AMBACHO AMINA HATAKISAHAU MAISHANI
“Hii ni ile siku ambayo Rais wa Ireland alipokuja kuhutubia Bunge la Tanzania, niliamua kuvaa kofia kwa kufikiria kwamba hiyo ingekuwa ya tofauti labda,” anasema mbunge huyo.
Anasema kabla ya kuvaa alisoma kanuni ambapo alielewa kuwa anatakiwa kuvaa kofia, na gloves za mikononi si lazima sana, ambapo aliamua kuvaa kofia bila gloves mikononi, jambo ambalo lilimletea mushkeli bungeni.
“Nilipofika katika viwanja vya Bunge waheshimiwa wabunge wengi walinisifia kuwa nimependeza, na wengine waliniandikia ujumbe wa ndani ya Bunge kuwa nimependeza sana lakini baadaye Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alitangaza bungeni kuwa natakiwa kutoka nje kwa kuwa nilikuwa nimevunja kanuni za Bunge kwa kuvaa kofia bila gloves,” anaelezea mbunge huyu kwa machungu.
Anasema hawezi kumulaumu Spika kwa kuwa alifuata kanuni na sana anailuamu nafsi yake kwa kutoelewa kanuni vizuri, jambo ambalo lilimfanya kujisikia vibaya sana kwa siku hiyo ambayo walikuwa na mgeni bungeni.
Chifupa anasema kitendo cha yeye kuandamwa na magazeti anajisikia vibaya kwa kuwa magazeti yamekuwa yanamwandika kupita kiasi, kwa kuwa yeye ni binadamu wa kawaida, amegeuzwa kuwa sehemu ya maisha yao, jambo ambalo linamkwaza sana.
Mbunge huyu ambaye hakuwahi kufikiria kuwa mwanasiasa hata siku moja zaidi ya kuota kuwa mwalimu, pilot na mtangazaji, ni mbunge mwenye umri mdogo kuliko wabunge wengine bungeni, ana miaka 24 tu!
Anasema kutokana na yeye kuwa na majukumu mengi mengine ya kitafa anamwomba sana radhi mwanaye Rahman Mpakanjia (4), kwa kukosa mambo mengi ambayo angeyapata kutoka kwa mama yake.
Chifupa anasema anatamani sana kuwa mwanasiasa mkubwa na mwenye uwezo wa kushawishi jamii na hasa kina mama, ambao kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakinyanyaswa na mfumo dume.
Pia mbunge huyu anamshukuru Mungu kwa kumfikisha hapo alipo sasa, mama yake mzazi Julie Solomon, baba yake mzazi, Luteni Khamis Chifupa kwa kumlea na kumsomesha, pia anamshukuru mumewe Mohamed Othman Mpakanjia kwa kumpa moyo kwa magumu yote ambayo alikuwa akiyapata na kumvumilia katika kipindi ambacho amekuwa hayupo.
Chifupa pia anawashukuru wajumbe wa Baraza Kuu la UVCCM taifa na Watanzania wote ambao walishiriki kwa namna moja ama nyingine kumchagua na kumfikisha hapo alipo.