CHAMA cha Wananchi (CUF), kimempa muda maalumu, Rais Jakaya Kikwete, kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, jana alinukuliwa akisema Rais Kikwete amepewa hadi mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, awe ametoa jawabu la matatizo ya kisiasa visiwani humo.
Alisema kama hatafanya hivyo, wananchi wataamua hatua zinazofaa kuchukuliwa.
Kwa bahati mbaya, profesa huyo hakusema wazi mwezi wa Ramadhani wa mwaka gani ambao Rais Kikwete anapaswa kuwa amemaliza matatizo ya kisiasa visiwani humo. Hata hivyo, tunaamini kuwa Ramadhani hiyo ni ya mwaka huu.
Pamoja na kutambua umuhimu wa kuwapo suluhisho la kisiasa katika Visiwa vya Unguja na Pemba, hatukubaliani na vizingiti alivyowekewa Rais Kikwete.
CUF wanapaswa watambue kuwa matatizo ya kisiasa Zanzibar si ya mwongo mmoja au miwili. Yamekuwapo hata kabla ya mapinduzi ya mwaka 1964. Vitabu vya historia vipo, vinaonyesha mlolongo wa matatizo ya kisiasa katia visiwa hivyo.
Hivyo basi, kumtega Rais Kikwete kwa kumpa wiki kumaliza matatizo ya kisiasa Zanzibar, si kumtendea haki.
Mtafaruku huo unahitaji kiongozi atulie, apange timu ya ushauri, apembue athari za kufanya hili na kuacha lile; ajue athari zinazoweza kujitokeza kwa kuleta mabadiliko haraka haraka, na kadhalika.
Sisi si wasemaji wa Rais Kikwete, lakini katika utashi wa kawaida, tulidhani kiongozi huyu angepewa muda zaidi wa kushughulikia mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Hotuba yake ya kwanza wakati akizindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilitosha kumfanya kila mmoja wetu kutambua dhamira nzuri aliyonayo kwa ajili ya ustawi wa taifa hili.
Kumshinikiza atoe majawabu ya matatizo ya kisiasa Zanzibar, ambayo yamekubuhu kwa miaka mingi, ni kumuonea.
Lakini huu unaweza ukawa mwanzo mwingine kwa viongozi wa CUF kuanza kuhamasisha vurugu.
Watanzania bado wanakumbuka maumivu makali ya mwaka 2001. Kulitokea mauaji yaliyolitia aibu taifa letu. Mara zote, kwenye mapambano kati ya wanachama wa vyama vya siasa na polisi, wanaoumia ni wanachama wa kawaida.
Hakujatokea Profesa Lipumba, Augustine Mrema, Seif Sharif Hamad, au kiongozi mwingine wa ngazi ya juu, akapigwa na kudhalilishwa kama inavyowatokea wanachama wa kawaida.
Wito wetu kwa wafuasi wa CUF ni kuwa makini na uchochezi huu wa kupeana kalenda za kumaliza matatizo. Matatizo ya kisasa kama haya ya Zanzibar, hayamalizwi kwa kalenda.
Yatamalizwa na viongozi walio na dhamira ya kweli. Rais Kikwete ameshatangaza dhamira hiyo. Apewe muda basi wa kushughulikia. Hajamaliza mwaka ofisini, watu wameanza kumshutumu. Tumpe muda walau hadi mwakani, ili tuone ataibua nini baada ya kimya cha mwaka mmoja.
CUF wasituingize tena kwenye matatizo mengine. Wanachama na wananchi wawe macho.