AHADI ya Rais Jakaya Kikwete kuondoa mpasuko wa kisiasa Zanzibar imeingia hatua mpya, baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kuweka ukomo wa utekelezaji wa ahadi hiyo.
Ukomo uliowekwa na chama hicho katika utekelezaji wa ahadi hiyo ni kabla ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi wa Ramadhani.
Msimamo huo wa CUF ulitangazwa na mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, katika mkutano wa hadhara mjini Chake Chake jana, kuwakaribisha wabunge wa kambi ya upinzani bungeni.
Prof. Lipumba alisema endapo ahadi ya Rais Kikwete haitaanza kutekelezwa hadi mwishoni mwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, mpasuko wa kisiasa Zanzibar utatatuliwa kwa kuzingatia uamuzi wa wananchi.
Alisema baada ya ahadi hiyo ya Rais Kikwete, viongozi wa chama hicho wamekuwa wakikabiliana na shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi, wakihoji hatua za utekelezaji.
“Tumevumilia sana, wananchi wanahoji kila kukicha hiyo ahadi itatekelezwa lini, tunakosa la kujibu. Rais yuko kimya, sasa tunatoa muda wa mwisho, kama ataendelea kukaa kimya mpaka mwishoni mwa mfungo wa mwezi wa Ramadhani, sisi tunajitoa katika suala hili.
“Suala hilo litarejeshwa kwa wananchi ambao tumekuwa tukiwataka kuendelea kuwa na subira kumpa muda rais kujipanga na kuanza kutekeleza ahadi yake. Wananchi wataamua wenyewe namna watakavyolishughulikia,” alisema.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe alimtaka Rais Kikwete kutowaogopa wahafidhina waliomo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema iwapo Rais Kikwete ataendelea kuwaogopa wahafidhina, hataweza kutekeleza ahadi aliyoitoa jambo ambalo litampunguzia hadhi yake kwa Watanzania.
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour, Agustine Mrema alidai kuwa sera za CCM zinawabagua na kuwatenga wakazi wa Pemba, jambo linalozidisha mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Alisema msimamo wa wakazi wa Pemba katika kudai haki yao ni wa kuigwa na Watanzania wengine nchini