Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kikwete adanganywa
Kikwete adanganywa
By Habari Tanzania | Published  09/10/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Happiness Katabazi

RAIS Jakaya Kikwete amedanganywa na wajanja katika suala la mikataba ya madini.

Matokeo yake, serikali yake imekubali kutupiwa ‘makombo’ na wawekezaji wa madini, badala ya kurekebisha sheria ya uwekezaji na sheria ya madini.

“Bilioni 9.1 ambazo Kampuni ya Barrick Gold ya Kanada itailipa serikali ni kidogo mno… ilipaswa kulipa zaidi… Mwaka 1999 Barrick ilikuwa na mgodi mmoja wa Bulyanhulu. Ilikubaliana na serikali kuwa badala ya kulipa mrabaha wa asilimia tatu, italipa dola milioni 5 kwa mwaka.

“Dola milioni tano zilikuwa zikitoka kwenye mgodi mmoja wa Bulyanhulu. Sasa kupitia makubaliano mapya kati ya kampuni hiyo na Rais Kikwete, katika migodi mitatu inayomilikiwa na kampuni hiyo, serikali itaambulia dola milioni 7.

“Hii ina maana kwamba kila mgodi utatulipa dola milioni 2.3, hiyo ina maana kuwa badala ya kupata zaidi, rais amekubaliana nao tupate kidogo kuliko ilivyokuwa awali.”

Hii ni kauli ya mwanasheria mahiri wa Chama cha Wanasheria wa Mazingira (LEAT), Tundu Lissu, katika mahojiano maalum na Tanzania Daima wiki hii. Kampuni zinazomilikiwa na Barrick ni Bulyanhulu, Shinyanga; Tulawaka; Biharamulo na North Mara; mkoani Mara.

Lissu pia alisema: “Serikali imeanza kutumia mbinu za hatari, ni sawa na wezi kumtupia mbwa mfupa wa nyama ili wakati akihangaika nao, wenyewe waingie kuiba kiulaini.

“Ni ajabu, Rais Kikwete kwenda kufanya mazungumzo na Kampuni ya Barrick bila kutoa taarifa ya uchunguzi wa tume ya serikali aliyounda mapema mwaka huu kwa ajili ya kuchunguza mikataba ili Watanzania wajue timu hiyo imegundua nini.

“Haya mazungumzo ya Rais Kikwete na Kampuni ya Barrick yalifanyika lini? Ni yeye mwenyewe ndiye aliyeutangazia umma kuwa ameunda tume ya kuchunguza mikataba, sasa nini kilimpeleka Barrick wakati tume aliyoiunda haijatoa taarifa hadharani?”

Kwa mujibu wa Lissu, serikali ya awamu ya nne ilipaswa kujikita katika kudhibiti utoroshaji wa madini, badala ya kukubali kupewa vijisenti vichache kiasi cha sh bilioni 9.1 kila mwaka kutoka Kampuni ya Barrick huku utajiri mkubwa ukiporwa na wajanja.

Alisema sh bilioni 9 ambazo Barrick imekubali kutoa kwa serikali kila mwaka na nyingine sh milioni 260 kwa halmashauri za wilaya ilipo migodo yake, ina lengo la kuifanya serikali kukwepa wajibu wake wa kufanya mabadiliko ya kimsingi ya sera za uwekezaji na sheria ya madini.

Aliyataja baadhi ya maeneo yanayotakiwa kufanyiwa marekebisho kuwa ni umilikaji wa migodi. Kwa mujibu wa Lissu, utaratibu wa sasa unaowapa fursa wawekezaji wageni kumiliki migodi kwa asilimia 100 haufai.

Mengine yanayopaswa kurekebishwa ni utozaji kodi, uondoshaji wa faida na mapato mengine yanayopatikana pamoja na mazao ya madini, na utaratibu wa uhuru wa kuhamisha usio na kizingiti.

Lissu alisema wananchi wanapaswa kuelewa ukweli huu badala ya kubaki kushangilia hatua zilizotangazwa na serikali. Alisema Barrick walikubali haraka kwa kuwa hakuna walichoongezewa kulipa, bali walilipa kidogo zaidi.

Kwa sababu hiyo, Lissu alihoji umakini wa serikali katika makubaliano yake na wawekezaji hao na wengine. Anasema hii inaonyesha kuwa serikali haijui mapato halisi ya wawekezaji hao kwa mwaka kwakuwa imekuwa na desturi ya kukurupuka katika kutoa maamuzi.

Aliishauri kama serikali ingekuwa makini, ingewabana wawekezaji kama ilivyofanya Peru, ambayo ‘iliwatia kabali’ wakalipa dola milioni 774. Miongoni mwa wawekezaji waliobanwa nchini Peru ni Kampuni ya Barrick.

Alisema Peru ilikuwa na matatizo kama ya Tanzania kabla ya kulipatia ufumbuzi suala hili.

Hivi karibuni serikali ilisema Rais Kikwete alifanya mazungumzo na Kampuni ya Barrick, wakakubaliana kwamba kampuni iilipe serikali dola milioni 7 sawa na sh bilioni 9.1 kwa mwaka kutokana na uzalishaji katika migodi yake.

Vile vile, walikubaliana kuwa kila halmashauri au wilaya ulipo mgodi ilipwe sh milioni 260 kwa mwaka.

Mara baada ya serikali kutangaza maafikiano hayo, baadhi ya wadau na mashabiki wa kisiasa wa Kikwete na Chama Cha Mapinduzi (CCM) walisifu hatua hiyo ya serikali. Lakini Lissu anasema ni makosa kushangilia bila kujua kiasi halisi kinachozalishwa na kampuni hiyo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.